Saturday, June 6, 2015

TANZANIA IMECHAGULIWA KUWA MJUMBE KATIKA BARAZA LA UTENDAJI (EXECUTIVE COUNCIL) LA SHIRIKA LA HALI YA HEWA DUNIANI–WORLD METEOROLOGICAL ORGANIZATION (WMO), GENEVA, USWISI, 4 JUNI 2015



Dr. Kijazi amechaguliwa tarehe 4 June 2015 bila kupingwa wakati Mkutano Mkuu wa kumi na saba wa Shirika la hali ya Hewa Duniani(WMO-Congress wa 17) ulioanza tarehe 25 Mei ambao unatarajiwa kumalizika tarehe 12 June,2015 jijini Geneva, Uswis

Dr. Kijazi amechaguliwa tarehe 4 June 2015 bila kupingwa wakati wa Mkutano Mkuu wa kumi na saba wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO­ Congress wa 17) ulioanza tarehe 25 Mei ambao unatarajiwa kumalizika tarehe 12 Juni, 2015 jijini Geneva, Uswisi


Kuchaguliwa kwa Dr. Agnes Kijazi kumetokana na jitihada kubwa za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kupitia Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Ubalozi wetu wa Kudumu Umoja wa Mataifa, Geneva,

 Dr. Kijazi anaongoza ujumbe wa Tanzania katika ushiriki Mkutano huo ambao una washiriki kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Maji na Ubalozi wa Tanzania, Geneva.

WMO ni Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya hali ya hewa duniani na mabadiliko ya tabia nchi. WMO inatekeleza majukumu na maamuzi kuhusu maendeleo ya sayansi ya hali ya hewa na uboreshaji wake ikiwa ni pamoja na kusimamia viwango katika upimaji na utoaji wa huduma za hali ya hewa kwa nchi wanachama.

Hadi wakati wa Mkutano huu unaoendelea nchini Uswisi, WMO ilikuwa na nchi wanachama 191. Katika Mkutano huu nchi za Sudani ya Kusini na Tuvalu zilikaribishwa rasmi kama wanachama wapya wa WMO. Kati ya nchi hizi 191 Wanachama wa WMO ni nchi 37 tu ambazo zina wajumbe katika Baraza hilo kuu. Hivyo hii ni nafasi adhimu na heshima kwa Tanzania, TMA na Dr Kijazi ambaye ni msomi mwenye utaalamu wa kutosha akiwa na shahada ya Uzamivu (Ph.D) katika sayansi ya Hali ya hewa.

Kazi kuu ya Baraza la Utendaji la WMO, ambalo Tanzania imefanikiwa kuwa mjumbe ni kuchukua hatua zinazostahili, kwa kushirikiana na Katibu Mkuu wa Shirika hilo kutekeleza maamuzi yanayotolewa na Mkutano Mkuu (WMO-Congress) ambao hukutana mara moja kila baada ya miaka minne.

Akizungumza baada ya uchaguzi huo Balozi Celestine Mushy, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa alielezea sababu ya Tanzania kugombea nafasi hiyo muhimu ni kutaka kuwa ndani ya chombo cha maamuzi na hivyo kushawishi maamuzi yatakayoinufaisha jamii nzima ya kimataifa ikiwemo Tanzania katika masuala ya hali ya hewa ikiwa ni pamoja na kutoa mwelekeo wa kisayansi katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa yanayoendelea maeneo mengi Duniani. Aidha, Dkt. Kijazi alieleza kuridhishwa kwake na jinsi ambavyo nchi wanachama 190 walivyoridhishwa na utendaji wa Tanzania katika kipindi cha miaka mitatu (2012­-2015) ambacho alikuwa mjumbe wa Baraza hili na
hivyo kumchagua tena katika kipindi kingine cha miaka minne.
 “Hii ni heshima kubwa kwa nchi yangu ya Tanzania na ninaahidi kutumia uwezo wangu wote kutekeleza majukumu ya nafasi hii” alisema Dkt. Kijazi.



Dr. Agnes Kijazi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ndiye aliyechaguliwa kuwa mjumbe katika Baraza la Utendaji (Executive Council) la Shirika la Hali ya Hewa Duniani–World Meteorological Organization (WMO) kwa kipindi cha miaka minne kuanzia 2015 hadi 2019.


Imetolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...