Wednesday, November 12, 2014

Rais Kikwete katika Mkutano wa Jinsia wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO)

Mkutano wa Jinsia kuhusu huduma za hali ya hewa ulioandaliwa na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) ulifanyika Geneva Uswis kuanzia  tarehe 5-7 Novemba 2014. Mkutano uliazimia mambo mbalimbali ikiwa pamoja na jinsi ya kuhakikisha wanawake wanajiunga kwa wingi katika fani ya sayansi ya hali ya hewa na maji. Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania alialikwa kutoa hotuba katika ufunguzi wa mkutano huo.
Katika hotuba yake ambayo imenukuliwa katika hadidu za mkutano Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete alisema upo uhusiano wa wazi kabisa kati ya athari za mabadiliko ya hali ya hewa na usawa wa kijinsia. Alisema,  wanawake wanaoishi katika maeneo ya vijijini ndio ambao kwa kiwango kikubwa wanakumbwa na athari za mabadiliko ya hali ya hewa. Hii ni kutokana na ukweli kwamba wanakabiliwa na changamoto zinazotokana na mazingira au mila ambazo zinawazuia kuwa na uwezo wa kumiliki rasilimali na pia kuwanyimwa haki na sauti ya kushiriki katika kutoa maamuzi mbalimbali. “Ni muhimu masuala ya jinsia yakajumuishwa na kupewa kipaumbele katika huduma za hali ya hewa ili kuhakikisha kwamba wanawake  wanakuwa na sauti katika kutoa maamuzi ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa” ilieleza hotuba hiyo ya mheshimiwa Rais.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Shirika la hali ya Hewa Duniani (WMO), Bwana Michael Jarraud alisema kwa kiasi kikubwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani limepata mafanikio kwa kuongeza utoaji wa huduma zenye mtazamo wa kijinsia kwa wakati na kwa ufanisi. “Hilo limewezekana kwa kupitia dhamira ya WMO ya kuzingatia mahitaji maalum ya wanawake na wanaume, pia ushirikishwaji wa wanawake na wanaume katika kuandaa na kubuni huduma mbalimbali kwa  kuzingatia usawa wa kijinsia”. Aliongeza Bwana Jarraud. Katika hotuba yake ya kufunga mkutano huo, Katibu Mkuu huyo wa WMO alitoa pongezi maalum kwa Bara la Afrika kwa kuongoza Duniani katika kuteua wanawake kuwa wakuu wa Taasisi za Hali ya Hewa. Mpaka sasa  kuna takribani jumla ya nchi sita za Afrika ikiwemo Tanzania ambazo wakuu wa Taasisi za Hali ya Hewa ni wanawakwe.
“ Athari za mabadiliko ya hali ya hewa zinawapata wanawake na wanaume kwa wakati mmoja ingawa wanaoathirika zaidi ni wanawake kutokana na kukosa elimu ya namna ya kujikinga”, alisema  Dkt. Elena Manaenkova, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Shirika la hali ya Hewa Duniani (WMO). Bi. Elena Manaekova aliongeza kuwa, wanawake na wanaume wanahitaji kuwa na haki sawa katika kupata ujuzi wa namna ya kutumia taarifa za hali ya hewa, hivyo kuwawezesha wanawake ni muhimu ili kuwajengea uwezo katika kukabiliana na na athari zinazotokana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt. Agnes Kijazi alisema kuna haja ya kuwatia moyo wasichana wenye ndoto za kuwa wanasayansi mahiri wa baadae ili waweze  kutimiza ndoto zao na kufikia malengo waliyojiwekea.  “Vijana wa kike wanahitaji kukataa kukatishwa tamaa bali waangalie wanawake ambao wamepata mafanikio katika sayansi na kufuata mifano yao” aliongeza Bi. Agnes Kijazi akizungumza katika mkutano huo.
“Sekta ya Afya inatakiwa kuwa mstari wa mbele katika kueleza huduma wanazohitaji kutoka Taasisi za hali ya hewa ili kuziwezesha Taasisi hizo kutoa huduma zinazokidhi mahitaji ya watumiaji. Aidha, Taasisi  za hali ya hewa zinapaswa kuanzisha mfumo mahususi wa usambazaji wa taarifa za hali ya hewa ili ziwafikie walengwa kwa wakati” alisema Bi. Hellen Msemo mwanasayansi  kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa  wakati akitoa mada katika Mkutano huo.
Mkutano huo  ulitoa mapendekezo mbalimbali ikiwa pamoja na kuwaongezea uwezo wanawake ili waweze kupata na kuzitumia taarifa za hali ya hewa, kuhamasisha Taasisi za Hali ya Hewa Duniani kuandaa mikakati ya mafunzo na kampeni zinazolenga kuhamasisha wanawake kusoma masomo ya sayansi ili kujiunga katika fani ya hali ya hewa na kuboresha njia za usambazaji wa taarifa za hali ya hewa ili taarifa hizo ziwafikie wanawake wengi. Aidha Taasis za Hali ya Hewa zimetakiwa kuhakikisha taarifa zinatolewa katika lugha nyepesi ya kueleweka kwa wanawake na wanaume.

Imetolewa na : Monica Mutoni Afisa Mahusiano wa TMA.

No comments:

Post a Comment