Tuesday, March 17, 2026

MHE. KAKOSO ATOA WITO KWA WATANZANIA KUFUATILIA NA KUZINGATIA TAARIFA ZA HALI YA HEWA.

 






Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Selemani Kakoso (MB) ametoa wito kwa watanzania kufuatilia na kuzingatia taarifa za hali ya hewa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), kwa kuwa ni muhimu katika kupanga na kutekeleza mipango na shughuli katika sekta zote  za kiuchumi na kijamii hapa nchini, aliyasema hayo wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu katika ofisi ya TMA, Dar es Salaam.

 

“Natoa wito kwa Watanzania kufuatilia na kuzingatia  taarifa za utabiri zinazotolewa na TMA kabla ya kuanza kutekeleza majukumu yenu katika sekta zenu ikiwemo kilimo, maji au kibiashara kwa kuwa TMA imekuwa ikitoa taarifa za uhakika kila siku kupitia vyombo mbalimbali vya habari. Kutokana na ubora na ufanisi wa huduma zao,  na weledi na umahiri wa wataalamu wake, TMA  wameaminiwa kutoa misaada ya kitaalamu kwa  baadhi ya Taasisi za hali ya hewa katika nchi mbalimbali barani Afrika.” Alisisitiza Mhe. Kakoso

 

Kupitia ziara hiyo yenye lengo la kukagua miradi inayotekelezwa na TMA, kamati ilipata fursa ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Ofisi ya TMA Kanda ya Mashariki na Kituo cha Tahadhari ya Matukio ya Tsunami pamoja na Kituo cha Taifa cha Uhakiki wa vifaa vya hali ya hewa na baadaye Mamlaka ilielekezwa kuongeza jitihada za usimamizi katika kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa kwa kuzingatia matakwa ya mkataba.

 

Naye Waziri wa Uchukuzi mwenye dhamana ya kusimamia sekta ya hali ya hewa Prof. Makame Mbarawa (MB) alisema Serikali ya awamu ya sita itaendelea kuwekeza kwenye sekta ya hali ya hewa na kuisimamia kwa karibu. Mh. Mbarawa aliahidi kufuatiilia kwa karibu kuhakikisha kuwa fedha zinazohitajika kwa ajili yya ukamilishaji wa miradi hiyo muhimu ya ujenzi wa miundombinu ya huduma za  hali ya hewa zinapatikana kwa wakati.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu, TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chang’a aliishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kwa kuwa sababu mafanikio ya TMA yamechagizwa pia na mchango mkubwa wa kamati kutaka kuona changamoto za TMA zinatatuliwa, kupitia maelekezo mbalimbali waliyokuwa wanatoa kwa nyakati tofauti.

 

“Kupitia ziara ya mwaka 2022 Mwanza, kamati hii iliiongezea nguvu TMA katika kuhakikisha tunaimarisha miundombinu ya hali ya hewa ikiwemo ukamilishaji wa rada 5 za hali ya hewa, mitambo mbalimbali ya kiutendaji, ongezeko la rasilimali watu pamoja na kujengewa uwezo wa kiutendaji wataalam wa hali ya hewa” Alisema Dkt. Chang’a

 

Dkt. Chang’a aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuiwezesha Mamlaka katika utekelezaji wa miradi miwili ya ujenzi wa jengo la Ofisi ya TMA Kanda ya Mashariki na Kituo cha Tahadhari ya Matukio ya Tsunami, ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 65 pamoja na ujenzi wa Kituo cha Taifa cha Uhakiki wa vifaa vya hali ya hewa ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 40. Kukamilika kwa miradi hii miwili kutaifanya TMA kuwa katika nafasi nzuri ya kuwa kitovu cha kuhakiki vifaa vya hali ya hewa hadi Ukanda wa Afrika.

Sunday, March 8, 2026

IWD 2026: TMA na masuala ya jinsia katika utoaji wa tahadhari za hali ya hewa


 

WANAWAKE WA TMA WAADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI 2026, KWA KUFANYA SHUGHULI ZA KIJAMII.

 WANAWAKE WA TMA WAADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI 2026, KWA KUFANYA SHUGHULI ZA KIJAMII.







Wanawake wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) wameadhimisha Siku ya Wanawake Duniani katika mikoa mbalimbali nchini Tanzania kwa kufanya shughuli tofauti za kijamii zinazolenga kuimarisha mshikamano na kusaidia jamii.


Maadhimisho hayo yalifanyika kwa kuzingatia kaulimbiu ya mwaka huu isemayo: “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana; Msingi Jumuishi kufikia Dira ya Maendeleo 2050.”


Katika Mkoa wa Dodoma, watumishi wanawake wa TMA walipata fursa ya kutembelea Kituo cha Watoto Yatima cha Safina  kilichopo Ntyuka, ambapo walikutana na watoto wanaolelewa katika kituo hicho na kuwapa faraja pamoja na kuwasaidia kwa mahitaji mbalimbali.


Ziara hiyo ililenga kuonesha upendo, mshikamano na kuwapa matumaini watoto wasiokuwa na wazazi au wale wanaoishi katika mazingira magumu.

Sunday, March 1, 2026

DKT CHANG’A AFANYA MAZUNGUMZO NA KATIBU MKUU WA SHIRIKA LA HALI YA HEWA DUNIANI (WMO)

DKT CHANG’A AFANYA MAZUNGUMZO NA KATIBU MKUU WA SHIRIKA LA HALI YA HEWA DUNIANI (WMO)

 

 Geneva, 27 Februari 2026

Katibu Mkuu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (World Meteorological Organization - WMO) Prof. Celeste Saulo ameahidi kuendelea kushirikiana na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) katika kuboresha huduma za hali ya hewa kwa matumizi katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Ameyasema hayo wakati wa kikao cha pembezoni mwa kikao cha 70 cha Kamati Kuu Tendaji ya Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (Seventieth Session of the Intergovernmental Panel on Climate Change-IPCC (70th IPCC Bureau), alipokutana na  Dkt. Ladislaus Chang’a, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya hali ya Hewa Tanzania (TMA), ambaye pia ni Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika WMO na Makamu wa Mwenyekiti wa Jopo la IPCC kwa lengo la kujadiliana kuhusu maendeleo ya utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini Tanzania na mipango ya kuendeleza ushirikiano na WMO tarehe 27 Februari 2026 Jijini Geneva, Uswisi.

Prof. Celeste Saulo amempongeza Dkt. Chang’a na kufurahishwa na namna TMA wanavyoendelea kusimamia vyema utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini Tanzania. Aidha, Prof. Celeste Saulo ameahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuboresha huduma za hali ya hewa kupitia programu mbalimbali za WMO ikiwa ni pamoja na eneo la matumizi ya akili mnemba (AI) katika mnyororo mzima wa utoaji wa huduma za hali ya hewa. 

“Nimefurahishwa na maendeleo ya utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini kwenu. Sisi kama WMO tuko tayari kuendelea kushirikiana ili kuboresha zaidi huduma huduma za hali ya hewa nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na kuwaunganisha na taasisi nyingine zilizopiga hatua zaidi ili kubadilishana ujuzi zaidi” Alisema Prof. Celeste Saulo.

Katika Kikao hicho, Dkt. Ladislaus Chang’a amemshukuru Katibu Mkuu wa WMO kwa usaidizi kwa TMA kupitia programu zake mbalimbali za uboreshaji wa huduma za hali ya hewa kikanda na kitaifa zikiwemo za “Climate Risk and Early Warning Systems (CREWS-EA), “Systematic Observations Financing Facility (SOFF)” na “Weather and Climate Information Services for Africa (WISER)” ambazo zinatekelezwa kwa ushirikiano na Wadau wa Maendeleo na Nchi Wanachama wa WMO ambapo utekelezaji wake unaendelea vizuri. 

“Nashukuru sana kwa usaidizi wa WMO kupitia programu zake mbalimbali zikiwemo za CREWS, SOFF na WISER ambazo zinachangia pakubwa katika kuboresha utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini na kuongeza nguvu katika uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hususan katika uboreshaji wa miundombinu ya hali ya hewa nchini na kuwajengea uwezo wataalamu. Programu hizi sio tu zimechagiza katika uboreshaji wa huduma za hali ya hewa bali zinawajengea uwezo wataalamu wa TMA wa kusaidia nchi nyingine kuboresha huduma zao za hali ya hewa” Alisema Dkt. Chang’a.

Dkt. Chang’a alimjulisha Katibu Mkuu wa WMO kuwa, Taasisi za Hali ya Hewa za Nchi wanachama wa WMO ambazo wataalamu wa TMA wametoa msaada wa kiufundi Barani Afrika hivi karibuni ni pamoja na Burundi, Sudan Kusini na Zimbabwe ambapo nchi nyingine ikiwa ni pamoja na Zambia, Sierra Leone na Uganda wataalamu wanaendelea na majadiliano ya namna wanavyoweza kusaidiwa na TMA katika maeneo ambayo TMA tumepiga hatua zaidi. Maeneo ambayo TMA imezisaidia nchi nyingine katika tasnia hii ya hali ya hewa ni pamoja na uboreshaji wa “Mfumo wa Usimamizi wa Ubora wa huduma (Quality Management System-QMS and Competency Assessment )”, “Utabiri wa Hali Mbaya ya Hewa (Severe Weather Forecasting)”, “Utabiri wa Hali ya Hewa kwa Kutumia Modeli za Kompyuta (Numerical Weather Prediction-NWP)”, “Mchakato wa kisheria katika sekta ya hali ya hewa (Legal Matters)” na Usambazaji wa Huduma za Hali ya Hewa kwa Umma (Public Weather Services-PWS). 

Katika kuhitimisha mazungumzo yao, Dkt. Chang’a alimshukuru Katibu Mkuu wa WMO kwa fursa ya kuleta mikutano mikubwa ya kitaalamu nchini ikiwa ni pamoja na mkutano wa nne (4) wa Wataalamu bingwa wa utabiri wa hali ya hewa Duniani utakaojadili maendeleo ya utabiri wa hali ya hewa kwa kuzingatia ukuaji wa teknolojia na matumizi ya huduma hizi kwa sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi “The Fourth WMO Operational Climate Prediction (OCP-4)” unaotarajiwa kufanyika Arusha mwishoni mwa mwezi Juni hadi mwanzo wa Julai 2026 kwa mara ya kwanza barani Afrika na kwa Tanzania.

IMETOLEWA NA:
KITENGO CHA UHUSIANO
MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA (TMA)

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...