Sunday, August 31, 2025

DKT. LADISLAUS CHANG’A ASHIRIKI KATIKA MKUTANO WA 6 WA MAWAZIRI NA MAMLAKA ZA MAZINGIRA WA ASIA NA PASIFIKI

 




Nadi, Fiji – 29 Agosti 2025

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a, kwa mwaliko wa Programu ya Umoja wa Mataifa uratibu wa Mazingira (UNEP) ameshiriki kikamilifu katika Mkutano wa 6 wa Mawaziri na Mamlaka za Mazingira wa Asia na Pasifiki (6th AP Forum) uliofanyika kuanzia tarehe 26–29 Agosti 2025 Jijini Nadi, Fiji. Mkutano huo uliandaliwa kwa pamoja na Serikali ya Fiji na UNEP ukiwa na kaulimbiu “Kutafuta Suluhisho Endelevu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi Duniani”.

Sambamba na mkutano huo, Dkt. Chang’a alikuwa na vikao mbalimbali na waheshimiwa na taasisi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kikao na Mhe. Rupa B. K., Waziri wa Serikali ya Nepal, Wizara ya Misitu na Mazingira, ambapo alimpatia taarifa kuhusu mpango kazi wa IPCC unaotekelezwa hadi mwaka 2029. Mazungumzo hayo yalijikita katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuboresha sera za mazingira. Mhe. Rupa alishukuru na kupongeza sana kazi kubwa inayofanywa na IPCC.

Aidha, Dkt. Chang’a alishiriki na kuratibu kikao cha ngazi ya Mawaziri kuhusu Mfumo wa tahadhari za majanga ikiwa ni pamoja na yale yanayosababishwa na hali ya hewa. Kikao hiki cha Waheshimiwa Mawaziri wa Asia na Pasifiki kilikuwa na wazungumzaji (panelists) wakiwemo: Mhe. Thoriq Ibrahim, Waziri wa Utalii na Mazingira wa Maldives; Mhe. Bi. Mona Ainu’u, Waziri wa Rasilimali Asili wa Niue; Mhe. Dkt. Maina Vakafua Talia, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira wa Tuvalu; Bi. Fleur Downard, Mkurugenzi wa Masuala ya Mazingira ya Kimataifa na Kitengo cha Umoja wa Mataifa, Wizara ya Mabadiliko ya Tabianchi, Nishati, Mazingira na Maji, wa Australia; na Bw. Sefanaia Nawadra, Mkurugenzi Mkuu, Sekretarieti ya Programu ya Mazingira kanda ya Pasifiki (Pacific Regional Environment Programme-SPREP).

Kikao hicho kiliangazia umuhimu wa mifumo ya tahadhari za majanga (multi-hazard early warning systems-MHEWS) kama mojawapo ya hatua bora zinazotekelezeka katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, kwa lengo la kulinda maisha na mazingira”.

Mkutano huu wa 6 wa Waheshimiwa Mawaziri wa Asia na Pasifiki wenye dhamana ya sekta ya mazingira ulikuwa pia jukwaa muhimu kwa makundi mbalimbali katika ukanda huo wawakilisha serikali zao, mashirika ya kikanda, vijana, sekta binafsi na wadau ambapo mchango na maoni yao vitasaidia katika maandalizi ya Mkutano wa 7 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (Seventh Session of the United Nations Environment Assembly (UNEA-7) unaotarajiwa kufanyika mwezi Desemba 2025 jijini Nairobi, Kenya.

Saturday, August 9, 2025

TMA YANYAKUA KOMBE MAONESHO YA NANE NANE 2025.

 






Morogoro, tarehe 08/08/2025

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imenyakua kombe kupitia maonesho ya Nane Nane 2025 yaliyofanyika katika Mkoa wa Morogoro. Ushindani wa TMA kupitia kundi la ushindani lililohusisha taasis za serikali upande wa Mawakala na Mamlaka za serikali nchini, umeifanya TMA kuibuka kidedea kwa kushika nafasi ya pili kwenye ambapo Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) ilishika nafasi ya kwanza na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ikishika nafasi ya tatu.

Aidha, TMA imelipokea kombe hilo kwa furaha kubwa na kutoa shukrani zao za dhati kwa waratibu wa maonesho hayo kwa kutambua mchango mkubwa wa TMA katika kuhudumia wadau mbalimbali kwenye maonesho hayo, ambapo wageni zaidi ya 2942 wameweza kuhudumiwa katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu ya sayansi ya hali ya hewa.

Thursday, August 7, 2025

VIONGOZI WAKUMBUSHWA KUHAMASISHA WANANCHI KUTUMIA TAARIFA ZA TMA


 









Morogoro, tarehe 07 Agosti 2025

Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Bi. Pili Mnyema amewakumbusha viongozi mbalimbali nchini kuendelea na jitihada za kuhamasisha wananchi kutumia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari katika Maonesho ya Nane Nane 2025 yanayoendelea kwenye viwanja vya Nane Nane, Morogoro.

“Kama viongozi tunajukumu la kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi wetu ikiwemo wakulima, wafugaji na wavuvi ili watumie utabiri wa hali ya hewa unaotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, itawasaidia wananchi kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa yaliyopo”. Alisisitiza Bi. Pili Mnyema

Kwa upande wa Meneja wa Kanda ya Mashariki-TMA, Bi. Hidaya Senga ameelezea njia mbalimbali zinazotumiwa na TMA katika usambazaji wa taarifa zake kama vile vyombo vya habari, tovuti, mitandao ya kijamii pamoja ushirikiano mkubwa na Taasis za kisekta ambao umesaidia kufikia wadau wengi wa sekta mbalimbali.

Bi. Hidaya ameongezea kwa kuwashauri wanafunzi kutembelea banda la TMA lililopo katika maonesho hayo ya Nane Nane ili kujifunza teknolojia mpya inayotumika TMA kwa kuona mtambo wa kisasa unaojiendesha wenyewe (Automatic Weather Station) kwa uhalisia zaidi.

Wednesday, August 6, 2025

ELIMU YA HUDUMA MAHUSUSI ZA HALI YA HEWA ZAWAVUTIA WENGI NANENANE MOROGORO

 










Morogoro, 06 Agosti 2025;

Elimu ya huduma mahususi za hali ya hewa inayotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeendelea kuwavutia wadau wengi waliotembelea katika banda la TMA kupitia maonesho ya NaneNane 2025 yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya NaneNane, Morogoro.

“ Sikuwahi kufikiria kama TMA inauwezo wa kuniandalia utabiri katika maeneo ya shamba langu, kwa kweli imenivutia sana” Alizungumza hayo mmoja wa wadau waliotembelea banda la TMA kupitia maonesho ya NaneNane, Morogoro Ndg. Seif Sempanga, Mkulima mwenye Ekari Zaidi ya 300, Kilindi Tanga.

Aidha, kupitia ujio wa wanafunzi kutoka shule mbalimbali mkoani Morogoro, wameshukuru sana kupata elimu ya mchakato mzima wa uandaaji utabiri wa hali ya hewa, namna taarifa za hali ya hewa zinavyosaidia huduma za usafirishaji ikiwemo usafiri wa anga na maji pamoja na sekta ya utalii.

“Namshukuru Mungu nimekuja kutembelea banda la TMA, nimejifunza mengi ambayo mengine sikuwahi kufikiria kuwa TMA wanafanya kazi kubwa namna hii, kumbe uwepo wa mvua inasaidia sekta ya utalii kuneemeka katika upatikanaji wa wanyama wengi kutokana na uwepo wa malisho na maji ya kutosha” alisema hayo mwanafunzi Nusiata Alexanda, kidato cha tatu kutoka shule ya sekondari ya sharte, Morogoro.

Monday, August 4, 2025

TMA YATUMIA FURSA YA MAONESHO YA NANENANE KUTOA ELIMU KWA JAMII









Dodoma, 03 Agosti 2025

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetumia fursa ya Maonesho NaneNane 2025 Kitaifa  yanayofanyika katika Viwanja vya Nzuguni, Dodoma kutoa elimu kwa jamii kuhusu huduma zitolewazo pamoja na jukumu kubwa la TMA la kudhibiti shughuli za hali ya hewa nchini.

Kupitia maonesho haya, wananchi na wadau mbalimbali wakiwemo wakulima, wavuvi na wafugaji wamepata elimu ya moja kwa moja kutoka kwa wataalamu wa TMA wakiwemo viongozi.

TMA imeeleza namna taarifa za hali ya hewa zinavyokusanywa, kuchakatwa na kuchambuliwa kupitia mifumo ya kisasa, na jinsi huduma hizo zinavyoweza kusaidia jamii.Aidha, TMA imeeleza umuhimu wa kuendesha shughuli za hali ya hewa zenye kukidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA ,Dkt.Ladislaus Chang'a na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), akiwahudumia wateja kwenye Banda la Mamlaka aliwahimiza wadau wote kufuatilia utabiri wa kila siku, utabiri wa msimu pamoja na tahadhari za hali mbaya ya hewa, huku akisisitiza matumizi sahihi ya taarifa hizo katika shughuli zote za kiuchumi na kijamii.

Aidha, aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya hali ya hewa na  rasilimali watu na hivyo kuleta maendeleo makubwa ya utendaji kazi wa Mamlaka.

Mamlaka ya Hali ya HewaTanzania inashiriki katika maonesho ya NaneNane Dodoma, Zanzibar, Mbeya na Morogoro.Kauli Mbiu ya mwaka huu ni  “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025”.

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...