Thursday, July 17, 2025

TANZANIA YACHANGIA UIMARISHWAJI WA HUDUMA ZA HALI YA HEWA


  Dar es Salaam, Tanzania – 16 Julai 2025

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kujizatiti katika kuimarisha huduma za hali ya hewa katika ukanda wa Afrika Mashariki, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maazimio ya kikao cha Wakuu wa taasisi za Hali ya Hewa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kilichofanyika tarehe 23 hadi 24 Mei, 2024 Entebbe, Uganda.

Kama sehemu ya utekelezaji wa maazimio,  Dkt. Mafuru Kantamla, Meneja wa Ofisi ya Utabiri Hali ya Hewa, alitoa  mafunzo ya utoaji wa utabiri wa hali mbaya ya hewa sambamba na utoaji wa tahadhari ya hali mbaya ya hewa kwa wataalamu wa  hali ya hewa wa Sudan Kusini (SSMS). Mafunzo hayo yalifanyika mjini Juba kuanzia tarehe 16 hadi 19 Juni 2025.

Wakati huo huo, wataalamu wa Mfumo wa Usimamizi wa Ubora (QMS) kutoka TMA, Dkt. Geofrid Chikojo na Bw. Danford Nyenyema walitekeleza awamu mbili za mafunzo kwa Taasisi ya Hali ya Hewa ya Burundi (IGEBU) katika mchakato wa kuanzisha utekelezaji wa QMS. Mafunzo haya yalifanyika kuanzia tarehe 27 hadi 31 Januari 2025 na kuendelea tena tarehe 9 hadi 13 Juni 2025. Aidha, mafunzo haya yalilenga kuweka misingi ya maandalizi ya taratibu za kazi, kuandaa nyaraka za QMS na kufanya ukaguzi wa ndani.

Mafunzo haya yote yamefanyika kwa kushirikiana na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na yamefadhiliwa kupitia Mradi wa CREWS Afrika Mashariki.

Akizungumza kuhusu mafanikio haya, Dkt. Ladislaus Chang’a, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa IPCC alisema:

“TMA imejipanga kikamilifu kuchangia katika kuimarisha utoaji wa huduma za hali ya hewa, ikiwa ni pamoja na mifumo ya tahadhari za hali ya hewa barani Afrika, kwa kuzingatia dhana ya kutomwacha yeyote nyuma, kutumia uwezo wetu wa kipekee na nguvu zetu binafsi na za pamoja. Ziara hizi za kitaalamu nchini Sudan Kusini na Burundi ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya TMA na ni mfano wa dhamira yetu ya pamoja ya kuimarisha utekelezaji wa Ajenda 2063 ya Afrika Tunayoitaka, pamoja na Mpango Mkakati wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (2024–2027).”

 

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...