Wednesday, January 22, 2025

UZINDUZI WA MRADI WA MFUKO WA UMOJA WA MATAIFA WA KUIMARISHA UANGAZI WA HALI YA HEWA


 














Dodoma, Tarehe 21/01/2025, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) amezindua rasmi awamu ya utekelezaji wa mradi wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuimarisha Uangazi wa Hali ya Hewa (SOFF) kupitia hafla iliyofanyika mjini Dodoma.

Mpango huu mkubwa unaofanywa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Taasisi ya Hali ya Hewa ya Denmark (DMI), unalenga kuimarisha uwezo wa Tanzania wa kufanya uangazi wa hali ya hewa, ubadilishanaji wa data za hali ya hewa na katika kukabiliana na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

 

Katika hotuba yake, Waziri Mkuu alisema “uzinduzi wa awamu ya utekelezaji wa mradi wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuimarisha Uangalizi wa Hali ya Hewa (SOFF) ni hatua muhimu kwa Tanzania na jumuiya za kimataifa.” Aliendelea kusema, “Utaongeza uwezo wa Tanzania katika kukusanya na kusambaza data za hali ya hewa, mpango huu utasaidia kujiandaa katika kukabiliana na maafa yatokanayo na mabadiliko ya hali ya hewa, na kuzisaidia sekta muhimu kama vile kilimo, nishati na usafirishaji katika kufanya maamuzi sahihi. Aliongeza kuwa mradi wa SOFF unaendana na mikakati ya Serikali ya kuleta maendeleo kwa ustawi na uendelevu wa Taifa.

Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile (MB), alisisitiza kuwa "SOFF sio tu inawekeza katika teknolojia 
ya kisasa bali ni kichocheo cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi sababu data sahihi za hali ya hewa 
huokoa na kulinda maisha na kuleta maendeleo endelevu." Naibu Waziri ameeleza kuwa Wizara ya 
Uchukuzi ambayo inasimamia sekta ya hali ya hewa nchini Tanzania inatambua kuwa mafanikio ya 
mpango wa SOFF yanategemewa kuwa endelevu na kuleta manufaa ya muda mrefu.

 

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Mwakilishi wa Kudumu wa 
Shirika la Hali ya Duniani (WMO) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko 
ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dk.Ladislaus Chang'a alisisitiza namna mradi wa SOFF unavyosaidia 
katika kukabiliana na mapungufu yaliyobainika katika miundombinu ya hali ya hewa nchini Tanzania ili 
kukidhi viwango vya Kimataifa vya Mtandao wa Kimataifa wa Uangazi wa Msingi (GBON). Utafiti wa 
mapungufu hayo ulifanyika  mwaka 2023, "ulionyesha kuwa Tanzania inahitaji angalau vituo 27 vya 
uangazi usawa wa ardhi kwa eneo la kilomita 200 kwa kilomita 200, na vituo vitano (5) vya uangazi 
angani kwa eneo la  kilomita 500 kwa kilomita 500."

 

Naye Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Shigeki Komatsubara, aliipongeza Serikali kwa hatua inayochukua 
katika kufanya mipango ya kukabiliana na maafa, akisema kuwa “SOFF itakuwa ni nyenzo muhimu ya 
kuwezesha mifumo ya utoaji wa tahadhali za mapema, kusaidia kufanya mifumo hii kuwa ya uhalisia 
kwa jamii zilizo hatarini ulimwengu.” Alisema hayo akienda sawa na mpango wa Katibu Mkuu wa Umoja 
wa Mataifa wa Tahadhali za Mapema kwa Wote, unaolenga kuhakikisha, ifikapo mwaka 2027, kila mtu 
Duniani analindwa na mifumo madhubuti ya tahadhari za mapema.

 

Jumla ya bajeti iliyotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa awamu ya uwekezaji wa mradi wa SOFF nchini 
Tanzania ni dola milioni 13.9, ambapo dola milioni 9 zinatolewa na Mfuko wa Mashirika ya Wadau wa 
Hisani (Multi-Partner Trust Fund (MPTF)) huku sehemu iliyobaki ikifadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya 
Muungano wa Tanzania. Mradi wa SOFF ni hatua kubwa katika kuboresha miundombinu ya data za 
hali ya hewa kitaifa na kimataifa, kuwezesha maamuzi sahihi ya kusaidia ustahimilivu wa kiuchumi na 
kimazingira. Kama sehemu ya mradi huo, Tanzania itanufaika kwa kuimarisha mifumo ya uangazi, 
teknolojia ya kisasa, pamoja na ushirikiano wa kimataifa.

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...