Dar es Salaam; Tarehe 21, Agosti 2024
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imekutana na wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini ili kujadili utabiri wa msimu wa mvua za Vuli (Oktoba – Disemba ) 2024, katika ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Dar es Salaam, Tarehe 21/8/2024.
“Warsha hii ni mwendelezo wa ushirikishwaji wa wanahabari katika kujadilli namna bora ya kufikisha taarifa sahihi kwa wananchi ili wajipange katika kuongeza tija na ufanisi wa utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii na pia kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na utabiri utakaotolewa” Alizungumza hayo Mgeni rasmi wakati akifungua warsha hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chang’a
Aidha, Dkt. Chang’a aliwashukuru wanahabari wote kwa mchango wao mkubwa katika kuhakikisha taarifa za hali ya hewa zinawafikia jamii kwa wakati na katika lugha inayoeleweka na kuongezea kuwa kupitia ushirikiano uliopo umepelekea mmoja wa wanahabari kutoka Channel Ten Bi. Dorcas Raymos kuambatana na Kaimu Meneja Masoko na Uhusiano Bi. Monica Mutoni kushiriki Mkutano wa Wadau wa Kikanda wa Maandalizi ya utabiri wa msimu Oktoba hadi Desemba 2024, Jijini Nairobi, Kenya na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo pale fursa zitakapojitokeza.
Kwa upande wake mwakilishi wa wanahabari Ndg. Bernard Lugongo kutoka gazeti la Dailynews, alitoa mrejesho wa namna usambazaji wa Utabiri wa mvua za Masika 2024 ulivyokuwa mkubwa na kupelekea Serikali na wadau kushauri wananchi katika sekta zao katika kupanga mikakati mapema ya kukabiliana na athari zilizotarajiwa kujitokeza.
“Vyombo vingi vya habari nchini vilisambaza taarifa za Utabiri wa Masika 2024 na kutoa tahadhari zilizokuwa zikitarajiwa kujitokeza, lakini pia kupitia elimu ya sayansi ya hali ya hewa tuliyoipata ilifanya usambazaji kwenda mbali zaidi katika kuwa tahadharisha wadau pamoja na serikali kwa ujumla ili wapange mikakati katika kushauri wananchi namna bora ya kukabiliana na hali tarajiwa katika maeneo yao” Alisema Ndg. Lugongo
Kupitia Warsha hii, wanahabari walipata elimu ya uelewa kuhusu sayansi ya hali ya hewa na kufanikiwa kupitia rasimu ya utabiri wa hali ya hewa katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba, 2024 unaotarajiwa kutolewa rasmi tarehe 22 Agosti 2024. Utabiri huo ni mahususi kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka ikihusisha mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Kaskazini mwa Morogoro, Visiwa vya Unguja na Pemba, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Simiyu, Mara, Geita, Mwanza, Shinyanga, Kagera na Kaskazini mwa Kigoma.
No comments:
Post a Comment