Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inapenda kutoa taarifa ya vipindi vya mvua kubwa vilivyojitokeza katika baadhi ya maeneo nchini.
Mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali hapa nchini zimepelekea uwepo wa athari katika baadhi ya maeneo. Mnamo usiku wa tarehe 19 kuamkia tarehe 20 Januari, 2024 vimejitokeza vipindi vya mvua kubwa zilizoambata na upepo mkali katika baadhi ya maeneo nchini na kusababisha athari ikiwemo mafuriko, uharibifu wa mali na miundombinu. Maeneo yaliyokumbwa na mvua hizo ni pamoja na Mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara, Arusha, Kilimanjaro na Manyara pamoja na Visiwa vya Unguja na Pemba. Hadi kufikia saa 3 asubuhi ya leo (20 Januari, 2024) kituo cha Zanzibar kiliripoti kiasi cha milimita 85.2 za mvua kwa saa 24 ikifuatiwa na kituo cha Kibaha milimita 84.8 na Dar es Salaam milimita 54.6.
Uwepo wa mvua hizo unasababishwa na kuimarika kwa mifumo ya hali ya hewa inayosababisha mvua nchini ikiwemo hali ya El-NiƱo kama ilivyoelezwa hapo awali. Aidha, Ukanda Mvua pamoja na kuimarika kwa migandamizo midogo ya hewa iliyopo mashariki mwa kisiwa cha Madagascar imepelekea pia kuwepo na vipindi vya mvua kubwa. Migandamizo hiyo midogo ya hewa inapelekea kuvuta upepo wenye unyevunyevu kutoka magharibi (Misitu ya Kongo) kuelekea baadhi ya maeneo ya nchini. Aidha, katika taarifa za mwelekeo wa mvua za Vuli, 2023 iliyotolewa tarehe 24 Augusti, 2023 na Mvua za Msimu 2023/2024 iliyotolewa tarehe 31 Oktoba, 2023 zilionesha uwepo wa vipindi vya mvua za nje ya msimu katika kipindi cha miezi ya Januari na Februari, 2024 hususan katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.
Uchambuzi wa mifumo ya hali ya hewa bado unaendelea kuonesha uwepo wa hali hiyo ya vipindi vya mvua vya nje ya msimu. Mamlaka inaendelea kufuatilia mienendo ya hali ya hewa nchini na kutoa mrejeo pale itakapobidi. Kwa taarifa hii wananchi wanashauriwa kuendelea kuzingatia taarifa na tahadhari za hali mbaya ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania sambamba na kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazotokana na hali mbaya ya hewa.