Monday, April 3, 2023

TMA YAKUMBUSHWA KUZINGATIA TARATIBU ZA SHERIA ZA MATUMIZI YA FEDHA.

Wafanyakazi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), wamekutana kupitia kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa TMA kilichofanyika katika ukumbi wa NSSF, Morogoro Tarehe 03 na 04 Aprili 2023, kwa dhumuni la kupokea, kujadili na kupitisha mapendekezo ya bajeti ya Mamlaka kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024. 

Mgeni rasmi katika ufunguzi wa kikao hicho alikuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Mhe. Atupele Mwakibete (MB) ambaye katika hotuba yake aliwakumbusha wajumbe kufanya kazi kwa bidii na weledi na kuzingatia uwajibikaji na taratibu za sheria za matumizi ya fedha. 

"Napenda kuwakumbusha kuzingatia Uzalendo, Uwajibikaji na Taratibu na sheria za matumizi ya fedha kwa kuhakikisha yale malengo ambayo mmejiwekea yanafikiwa na yanatekelezwa kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa". Alisisitiza Mhe. Mwakibete (MB).

Mhe. Mwakibete (MB), aliongezea kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inatambua umuhimu mkubwa katika kuimarisha miundombinu ya hali ya hewa ndiyo maana imefanya na inaendelea kufanya uwekezaji mkubwa wa kuimarisha mtandao wa Rada na miundombinu mingine ya hali ya hewa kama ilivyoainishwa katika Ilani ya uchaguzi wa CCM ya mwaka 2020-2025. 

"Aidha, kama alivyoagiza Mhe.Rais, TMA mnatakiwa kuwa wabunifu katika kuongeza vyanzo vya mapato na kusimamia ukusanyaji wa mapato ili kupunguza utegemezi kwa Serikali". Alisisitiza Mhe. Mwakibete. 

Vilevile, Mhe. Mwakibete aliipongeza TMA kwa usahihi wa utabiri Katika miaka ya hivi karibuni, wote tumeendelea kushuhudia jinsi ambavyo huduma za hali ya hewa zinavyondelea kuboreshwa. 

"Nawapongeza kwa viwango vya usahihi wa utabiri ambavyo vinaendelea kuongezeka. Nimeelezwa kuwa kwa msimu wa mvua za Vuli mwaka 2022, viwango vya usahihi vilikuwa asilimia 94.1%". Alisema Mhe. Mwakibete. 

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Dkt. Buruhani Nyenzi wakati akimkaribisha mgeni rasmi, alisema Mamlaka imeendelea kusimama imara na kufanya vizuri katika nyanja zote za Kitaifa na Kimataifa pamoja na mabadiliko ya uongozi, vilevile alieleza baadhi ya changamoto zinazoikabili TMA ni pamoja na maslahi duni. 

 “Pamoja na mafanikio hayo TMA inakabiliwa na changamoto ya maslahi duni kwa watumishi hali inayopelekea wataalam wengi kuhamia taasisi nyingine ndani na nje ya nchi.Naomba kuendelea kuiomba Wizara yako itusaidie ili watumishi wa Taasisi hii wapatiwe viwango vya mishahara vinavyolingana na majukumu yao ya kazi kama ilivyoainishwa kwenye tathmini.” 

Awali, Dkt. Ladislaus Changa, Mwenyekiti wa Baraza na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, aliishukuru Serikali ya Jamhuri wa Tanzania inayoongozwa na Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuitengea fedha Mamlaka na kwa juhudi kubwa ya kuwekeza katika kuimarisha miundombinu ya hali ya hewa. 

Dkt. Changa alisema kikao cha Baraza la wafanyakazi TMA ni utekelezaji wa mkataba mpya wa Baraza la wafanyakazi uliosainiwa tarehe 27 Februari 2023 baada ya majadiliano ya kina baina ya Menejimenti na Viongozi na wawakilishi wa TUGHE. Majadiliano ya kuandaa mkataba huu yalihusisha pia Viongozi wa TUGHE Taifa na Mkoa.

"Majadiliano yaliyofanyika na kusainiwa kwa mkataba ni uthibitisho wa ushirikishwaji mkubwa wa wafanyakazi katika maendeleo ya Taasisi na katika kushughulikia masuala mtambuka ikiwemo maslahi yao". Alisema Dkt. Changa.

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...