Thursday, March 3, 2022

TMA: MWAKA 2021 ULIKUWA NA WASTANI WA ONGEZEKO LA JOTO KWA NYUZIJOTO 0.5 NCHINI.

Tofauti kati ya halijoto la juu kwa miezi ya Novemba na Desemba mwaka 2021 
na wastani wa muda mrefu (1981-2010) 




 

Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi  akitoa taarifa ya klimatolojia ya hali ya hewa kwa mwaka 2021 kwa Tanzania. katika Ukumbi wa Makao Makuu ya TMA, Dar es Salaam Tarehe 03/03/2022.

 
 

Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi  katikati akiendelea kutoa taarifa ya klimatolojia ya hali ya hewa kwa mwaka 2021 kwa Tanzania. katika Ukumbi wa Makao Makuu ya TMA, Dar es Salaam Tarehe 03/03/2022.

Waandishi pamoja na washiriki mbalimbali wakisikiriza kwa makini  taarifa ya klimatolojia ya hali ya hewa kwa mwaka 2021 kwa Tanzania. katika Ukumbi wa Makao Makuu ya TMA, Dar es Salaam Tarehe 03/03/2022.

Dar es Salaam;Tarehe 03 Machi, 2022;

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania  (TMA) imetoa taarifa ya klimatolojia ya hali ya hewa kwa mwaka 2021 kwa Tanzania. Akizungumzia taarifa hiyo katika ukumbi wa mikutano, Makao Makuu ya TMA, Dar es Salaam, Tarehe 03 Machi 2022, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt. Agnes Kijazi, alisema kuwa mwaka 2021 ulikuwa na joto la juu ya wastani wa muda mrefu (1981-2010) kwa kiwango cha nyuzi joto 0.50C.

“Hali ya ongezeko la joto inaweza ikawa imeathiri afya za binadamu na wanyama, uzalishaji, usindikaji na uhifadhi wa vyakula, Mwezi Novemba 2021 ulivunja rekodi ya kuwa na joto kali zaidi ikilinganishwa na miezi ya Novemba ya miaka ya nyuma tangu 1970. Kwa upande mwingine, mwezi Disemba umekuwa wa tatu kwa kurekodi joto kali zaidi kwa mwezi huo tangu mwaka 1970”. alifafanua Dkt. Kijazi.

Aidha, ripoti hiyo ilieleza kuwa nchi ilikuwa na upungufu wa mvua katika maeneo mengi yanayopata mvua za misimu miwili (kanda ya ziwa, nyanda za juu kaskazini mashariki na pwani ya kaskazini), hasa wakati wa msimu wa mvua za Vuli, Oktoba-Disemba 2021. Kwa wastani, mwezi Novemba 2021 ulikuwa na mvua kidogo kuliko miezi yote inayopata mvua za vuli kwa mwaka na umeshika nafasi ya tatu miongoni mwa miezi mikavu ya Novemba iliyowahi kutokea tangu mwaka 1970.

“Kipindi cha ukavu cha muda mrefu kilitokea katika miezi ya Oktoba na Disemba 2021 na kusababisha athari kubwa kwa jamii na uchumi hasa jamii za wafugaji ambapo idadi kubwa ya mifugo ilikufa kwa kukosa malisho na maji katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Morogoro, Manyara na Pwani”. Alisema Dkt Kijazi.

Taarifa hiyo kwa ujumla imeeleza kuwa mwaka 2021 ulikuwa na matukio ya hali mbaya ya hewa, hususan mvua kubwa, mafuriko, vipindi virefu vya hali ya ukavu, upepo mkali na hali ya joto kali, ambavyo viliathiri maisha kwa kiasi kikubwa. Alifafanua kwamba kutokana na mabadiliko ya tabianchi, matukio ya hali mbaya ya hewa yamekuwa yakiongezeka idadi (frequency) na nguvu (strength).

Katika hatua nyingine, Dkt. Kijazi alitoa taarifa ya tathimini ya athari za mabadiliko ya hali ya hewa (IPCC WGII report) iliyotolewa na Jopo la Kiserikali la Tathmni ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC) ikieleza kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yanayojumuisha kuongezeka kwa idadi na ukubwa wa matukio ya hali mbaya ya hewa ikiwemo ukame na mvua kubwa pamoja na ongezeko la joto ambalo linatarajiwa kufikia nyuzi joto 1.50C ifikapo mwaka 2040 endapo hatua za kupunguza uzalishaji wa gesi ukaa hazitachukuliwa hasa kwa nchi zinazozalisha gesi hiyo kwa wingi duniani na yameendelea kusababisha athari na madhara makubwa zaidi kwa jamii, viumbe hai na mfumo mzima  wa ikolojia.

“Uwezo wa kuhimili changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa utakuwa mashakani zaidi endapo ongezeko la joto litazidi nyuzi joto 1.50C”. Alieleza Dkt. Kijazi wakati akiwasilisha masuala yaliyoainishwa katika taarifa ya Jopo hilo la Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi. Taarifa hiyo ya jopo la kisayansi inapatikana katika tovuti ya IPCC.

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...