Monday, March 28, 2022

MWENENDO WA MVUA NCHINI.

 


Dar es Salaam, 28 Machi, 2022:

Mvua za Masika, 2022 katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka (Ukanda wa Ziwa Victoria, nyanda za juu kaskazini na pwani ya kaskazini) zilianza kunyesha wiki ya tatu(3) na ya nne(4)ya mwezi Februari 2022 katika maeneo mengikama zilivyotarajiwa. Hata hivyo, vimejitokeza vipindi virefu vya ukavu kati ya wiki ya kwanza na ya tatu yamwezi Machi, 2022 hususan kwa baadhi ya maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki na ukanda wa pwani ya kaskazini.Vipindi hivyo virefu vya ukavu vimesababishwa na matukio ya vimbunga hususan kimbunga Gombe kilichodumu kwa muda mrefu katika Bahari ya Hindi eneo laRasi ya Msumbiji pamoja na kujitokeza kwa joto la bahari la chini ya wastani katika eneo la pwani ya Afrika Mashariki.Hali hiyo imechangia pia Ukandamvua (ITCZ) kuendelea kusalia katika maeneo ya kusini mwa nchi ambapo kwa kawaida katika kipindi cha mwanzoni mwa mwezi Machi huanza kuelekea maeneo ya kaskazini mwa nchi.

Hata hivyo, unyeshajiwamvua unatarajiwa kuimarikakatikabaadhi ya maeneomwishoni mwa mwezi Machi, 2022na mwanzoni mwa mwezi Aprili,2022 na kufuatiwa na upungufu kati ya wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Aprili, 2022hususani kwa maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki na pwani ya kaskazini.

Kwa upande mwingine, kusalia kwa Ukandamvua katika maeneo ya kusini kumesababishamvua za Msimu kuendelea kunyesha kwa kiwango cha kuridhisha katika baadhi ya maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka (magharibi mwa nchi, kanda ya kati, nyanda za juu kusini magharibi, Ruvuma pamoja na maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro).

Wananchi wanashauriwa kuendelea kuzingatia taarifa na tahadhari za hali ya hewa zilizotolewa na zitakazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania sambamba na kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazotokana na hali mbaya ya hewa.

Friday, March 25, 2022

DKT. KIJAZI AELEZA MAFANIKIO YA UMOJA WA TAASISI ZA HALI YA HEWA ZA NCHI ZA SADC (MASA) YALIYOPATIKANA CHINI YA UENYEKITI WA TANZANIA


Picha Na 1: Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za  Umoja wa Taasisi za Hali ya Hewa za nchi za SADC “Meteorological Association of Southern Africa (MASA)” katika  kipindi cha Uenyekiti wa Tanzania ((Agosti 2019 hadi Machi 2022), kwenye mkutano Mkuu wa 14 wa MASA,  uliofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 17 Machi, 2022, ambapo Dkt. Kijazi aliongoza Mkutano huo akiwa Mwenyekiti anayemaliza muda wake.  Kulia kwake ni Meneja Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Wilbert Muruke akifuatilia majadiliano ya mkutano huo


Picha Na 2: Baadhi ya washiriki wa mkutano Mkuu wa 14 wa Umoja wa Taasisi za Hali ya Hewa za nchi za SADC “Meteorological Association of Southern Africa (MASA)” katika picha ya pamoja (kwa njia ya mtandao). 

 


 Mwanza: Tarehe 17/03/2022

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi, ameeleza mafanikio ambayo Umoja wa Taasisi za Hali ya Hewa za Nchi za SADC “Meteorological Association of Southern Africa (MASA)” umepata chini ya Uenyekiti wa Tanzania, katika kipindi cha Agosti 2019 hadi Machi 2022, licha ya changamoto ya ugonjwa wa UVIKO-19.

Dkt. Kijazi ambaye alikuwa Mwenyekiti wa MASA katika kipindi hicho cha miaka miwili na miezi 6, alieleza mafanikio hayo alipowasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za MASA katika kipindi cha uongozi wake, kwenye mkutano mkuu wa 14 wa Umoja huo “Fourteenth MASA Annual General Meeting (MASA AGM-14)” uliofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 17 Machi, 2022. Katika taarifa yake, Dkt. Kijazi alieleza kwamba licha ya changamoto ya ugonjwa wa UVIKO-19 iliyojitokeza katika kipindi hicho na kuathiri shughuli za MASA, mafanikio mbalimbali yalipatikana yaliyohusisha majukumu ya Bodi na Sekretarieti ya MASA.

“Tunafahamu kuwa changamojto ya ugonjwa wa UVIKO-19 iliathiri shughuli nyingi za MASA zilizokuwa zimepangwa kutekelezwa kutokana na masharti ya kusafiri na kufanya mikutano yaliyotolewa na Mamlaka za Afya. Hata hivyo, licha ya changamoto hiyo, napenda kuwajulisha kwamba Bodi ilijitahidi kutekeleza shughuli za MASA, ikiwa ni pamoja na maamuzi ya Waheshimiwa Mawaziri wa SADC, na kuna mafanikio kadha wa kadha ambayo ni muhimu Wanachama wa MASA kufahamishwa”. alisema Dkt. Kijazi na kuendelea kutaja mafanikio hayo.

Miongoni mwa mafanikio aliyoeleza Dkt. Kijazi ni pamoja na: Kukamilika kwa mpango wa kuhuisha kazi za MASA (MASA Rescue Plan); kuandaliwa kwa mpangokazi wa utekelezaji wa mpango huo (MASA Rescue Plan Programme of action); Tanzania kujitolea kuwa mwenyeji wa Sekretarieti ya MASA; na mikutano ya Bodi ya MASA kufanyika kwa njia ya mtandao. Aidha, Dkt. Kijazi alifafanua zaidi kwamba athari za ugonjwa wa UVIKO-19 kwa shughuli za MASA zililitokana pia na kutetereka kwa hali ya kifedha kutokana na Nchi Wanachama kushindwa kulipa ada za uanachama za kila mwaka.

Katika hatua nyingine, MASA ilifanya uchaguzi wa viongozi wapya wa umoja huo katika nafasi ya Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, na wajumbe wa Bodi kwa kipindi kingine cha miaka miwili. Katika uchanguzi huo, Nchi ya Msumbiji ilichanguliwa kuwa Mweyekiti mpya wa MASA na Lesotho kuwa Makamu Mwenyekiti. Kwa upande wa Wajumbe wapya wa Bodi ya MASA waliochanguliwa ni Afrika ya Kusini, Tanzania, na Zambia. 

Thursday, March 24, 2022

SIKU YA HALI YA HEWA DUNIANI 2022: SERIKALI YAITAKA JAMII KUFUATILIA TAARIFA ZA HALI YA HEWA NA KUCHUKUA HATUA ZA MAPEMA KUEPUKA MAAFA

 




Dar es Salaam; Tarehe 23 Machi, 2022;

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi kufuatilia taarifa za hali ya hewa na kuchukua hatua za mapema ili kuepuka majanga yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa. Aliyasema hayo alipokuwa akihutubia katika hafla ya uzinduzi wa nyumba 644 za wakazi wa Magomeni, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni – Dar es Salaam, Tarehe 23 Machi 2022.

Niwakumbushe leo ni Siku ya Hali ya Hewa Duniani, niwaombe wananchi wote kufuatilia taarifa za hali ya hewa. Huu ni mwezi wa tatu na mwezi wa nne tunategemea Masika na mvua zimeanza kuonesha makali yake, kwa hiyo niwaombe sana mfuatilie taarifa za hali ya hewa ili kujiepusha na majanga mapema, mtakapopata taarifa za hali ya hewa na tukazifuata, basi tutaepukana na majanga au maafa mapema Alisisitiza Mhe. Samia Suluhu Hassan.

 

Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (MB) ametoa wito kwa watumiaji na wadau wote wa taarifa za hali ya hewa hususani kwa jamii inayoathirika zaidi na maafa yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa, kufuatilia taarifa na kuchukua tahadhari pamoja na kuwataka kuunga mkono mipango ya Serikali katika uboreshaji wa huduma hizo. Aliyazungumza hayo alipozungumza na vyombo vya habari katika kuadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani-2022 yenye kauli mbiu “Tahadhari kwa Hatua za Mapema” katika Ukumbi wa Mikutano wa Mamlaka ya Bandari, Jijini Dar es Salaam.

 

Aidha, Mhe. Mbarawa aliongeza kuwa, katika kuboresha huduma za hali ya hewa, Serikali ilitunga sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) Na. 2 ya mwaka 2019 na inaendelea kuboresha miundombinu ya upimaji wa hali ya hewa kwa kununua RADA za hali ya hewa na vifaa vya kisasa na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa hali ya hewa. Uwekezaji huu umechangia kuongezeka kwa viwango vya usahihi wa utabiri wa hali ya hewa kufikia kati ya asilimia 93 na 96, viwango ambavyo ni vya juu ikilinganishwa na kiwango cha asilimia 70 kinachokubalika na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) kuwa kinafaa kwa matumizi. 

 

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi alipata wasaa wa kuzungumza na wanahabari kwa kuelezea sababu zilizopelekea kuchaguliwa kwa kaulimbiu hiyo kuwa ni kutokana na ongezeko la maafa yanayotokana na hali mbaya ya hewa kwa wingi na kwa ukubwa wake hasa kwa kusababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi duniani. Pia alisema endapo taarifa zikitolewa na tahadhari zikichukuliwa mapema zitapunguza maafa yatokanayo na hali mbaya ya hewa yanayoweza kujitokeza. Mwisho Dkt. Kijazi aliwatakia wadau wote wa hali ya hewa maadhimisho mema ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani.

 

Siku ya Hali ya Hewa Duniani huadhimishwa tarehe 23 Machi kila mwaka ikiwa ni kumbukizi ya kusainiwa kwa mkataba wa kuanzishwa kwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO).

 

 

Wednesday, March 16, 2022

KUMBUKUMBU YA MWAKA MMOJA WA HAYATI DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI


 

TMA YATAKIWA KUJIKITA KATIKA KUKUZA MAPATO YA NDANI

 




















TMA YATAKIWA KUJIKITA KATIKA KUKUZA MAPATO YA NDANI.


Mwanza; Tarehe 15 Machi, 2022;

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetakiwa kujikita katika kukuza mapato ya ndani ili kuweza kuboresha huduma zake za msingi. Hayo yalizungumzwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Moshi Seleman Kakoso (MB) katika semina ya kujenga uelewa wa majukumu na huduma zitolewazo na TMA, iliyofanyika katika Ukumbi wa TMDA, Mwanza, Tarehe 15/03/2022. 

Mhe. Kakoso aliitaka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kujikita katika kukuza mapato ya ndani ili kuweza kuboresha huduma za kimsingi za hali ya hewa na hivyo kufikia malengo.  

Aidha, Mhe. Kakoso aliendelea kwa kusisitiza kuwa ili kuwa na utabiri wa uhakika wa hali ya hewa, Mamlaka inahitaji vitendea kazi vya kutosha ambavyo upatikanaji wake unahitaji fedha za kutosha kutoka serikalini, na hivyo, kuitaka TMA kuendelea kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira kwa kuendelea kuboresha huduma za hali ya hewa katika sekta ya mazingira kwa lengo hilohilo la kuongeza mapato. Mhe. Kakoso alimalizia kwa kuipongeza TMA kwa kutoa huduma bora za hali ya hewa hapa nchini.

Naye, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Atupele Fredy Mwakibete (MB) alimpongeza Mkurugenzi Mkuu na watumishi wa TMA kwa kazi nzuri inayofanyika na kuwaasa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kutembelea Ofisi za TMA ili waweze kujionea kwa kina majukumu na huduma mbali mbali zitolewazo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na  Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt. Agnes Kijazi aliishukuru Kamati ya Bunge kwa fursa iliyopatikana ya kutoa elimu ya mchango wa huduma za hali ya hewa katika kukuza uchumi wa nchi. Vilevile alieleza kuwa majukumu ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania yamegawanyika katika sehemu kuu tatu ambayo ni kutoa huduma za hali ya hewa, kudhibiti shughuli za hali ya hewa hapa nchini kwa mujibu wa Kifungu cha kumi na nne (14) na kuratibu shughuli za hali ya hewa nchini kulingana na Kifungu cha tano (5) cha Sheria yaMamlaka ya Hali ya Hewa Na.2 ya Mwaka 2019. 

 

Katika hatua nyingine, wajumbe walipata fursa ya kutembelea rada ya hali ya hewa iliyopo Kiseke, Mwanza na kupitishwa katika mada mbalimbali za kuwajengea uelewa juu ya majukumu na mchango wa huduma za hali ya hewa zitolewazo na TMA kwa manufaa ya jamii na kuchangia katika kukuza uchumi kupitia matumizi ya huduma hizi katika sekta mbalimbali nchini. Wajumbe waliipongeza Mamlaka kwa kazi nzuri na kuelekeza TMA ihakikishe huduma za hali ya hewa  zinawafikia wakulima katika ngazi ya vijiji.

Thursday, March 3, 2022

TMA: MWAKA 2021 ULIKUWA NA WASTANI WA ONGEZEKO LA JOTO KWA NYUZIJOTO 0.5 NCHINI.

Tofauti kati ya halijoto la juu kwa miezi ya Novemba na Desemba mwaka 2021 
na wastani wa muda mrefu (1981-2010) 




 

Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi  akitoa taarifa ya klimatolojia ya hali ya hewa kwa mwaka 2021 kwa Tanzania. katika Ukumbi wa Makao Makuu ya TMA, Dar es Salaam Tarehe 03/03/2022.

 
 

Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi  katikati akiendelea kutoa taarifa ya klimatolojia ya hali ya hewa kwa mwaka 2021 kwa Tanzania. katika Ukumbi wa Makao Makuu ya TMA, Dar es Salaam Tarehe 03/03/2022.

Waandishi pamoja na washiriki mbalimbali wakisikiriza kwa makini  taarifa ya klimatolojia ya hali ya hewa kwa mwaka 2021 kwa Tanzania. katika Ukumbi wa Makao Makuu ya TMA, Dar es Salaam Tarehe 03/03/2022.

Dar es Salaam;Tarehe 03 Machi, 2022;

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania  (TMA) imetoa taarifa ya klimatolojia ya hali ya hewa kwa mwaka 2021 kwa Tanzania. Akizungumzia taarifa hiyo katika ukumbi wa mikutano, Makao Makuu ya TMA, Dar es Salaam, Tarehe 03 Machi 2022, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt. Agnes Kijazi, alisema kuwa mwaka 2021 ulikuwa na joto la juu ya wastani wa muda mrefu (1981-2010) kwa kiwango cha nyuzi joto 0.50C.

“Hali ya ongezeko la joto inaweza ikawa imeathiri afya za binadamu na wanyama, uzalishaji, usindikaji na uhifadhi wa vyakula, Mwezi Novemba 2021 ulivunja rekodi ya kuwa na joto kali zaidi ikilinganishwa na miezi ya Novemba ya miaka ya nyuma tangu 1970. Kwa upande mwingine, mwezi Disemba umekuwa wa tatu kwa kurekodi joto kali zaidi kwa mwezi huo tangu mwaka 1970”. alifafanua Dkt. Kijazi.

Aidha, ripoti hiyo ilieleza kuwa nchi ilikuwa na upungufu wa mvua katika maeneo mengi yanayopata mvua za misimu miwili (kanda ya ziwa, nyanda za juu kaskazini mashariki na pwani ya kaskazini), hasa wakati wa msimu wa mvua za Vuli, Oktoba-Disemba 2021. Kwa wastani, mwezi Novemba 2021 ulikuwa na mvua kidogo kuliko miezi yote inayopata mvua za vuli kwa mwaka na umeshika nafasi ya tatu miongoni mwa miezi mikavu ya Novemba iliyowahi kutokea tangu mwaka 1970.

“Kipindi cha ukavu cha muda mrefu kilitokea katika miezi ya Oktoba na Disemba 2021 na kusababisha athari kubwa kwa jamii na uchumi hasa jamii za wafugaji ambapo idadi kubwa ya mifugo ilikufa kwa kukosa malisho na maji katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Morogoro, Manyara na Pwani”. Alisema Dkt Kijazi.

Taarifa hiyo kwa ujumla imeeleza kuwa mwaka 2021 ulikuwa na matukio ya hali mbaya ya hewa, hususan mvua kubwa, mafuriko, vipindi virefu vya hali ya ukavu, upepo mkali na hali ya joto kali, ambavyo viliathiri maisha kwa kiasi kikubwa. Alifafanua kwamba kutokana na mabadiliko ya tabianchi, matukio ya hali mbaya ya hewa yamekuwa yakiongezeka idadi (frequency) na nguvu (strength).

Katika hatua nyingine, Dkt. Kijazi alitoa taarifa ya tathimini ya athari za mabadiliko ya hali ya hewa (IPCC WGII report) iliyotolewa na Jopo la Kiserikali la Tathmni ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC) ikieleza kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yanayojumuisha kuongezeka kwa idadi na ukubwa wa matukio ya hali mbaya ya hewa ikiwemo ukame na mvua kubwa pamoja na ongezeko la joto ambalo linatarajiwa kufikia nyuzi joto 1.50C ifikapo mwaka 2040 endapo hatua za kupunguza uzalishaji wa gesi ukaa hazitachukuliwa hasa kwa nchi zinazozalisha gesi hiyo kwa wingi duniani na yameendelea kusababisha athari na madhara makubwa zaidi kwa jamii, viumbe hai na mfumo mzima  wa ikolojia.

“Uwezo wa kuhimili changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa utakuwa mashakani zaidi endapo ongezeko la joto litazidi nyuzi joto 1.50C”. Alieleza Dkt. Kijazi wakati akiwasilisha masuala yaliyoainishwa katika taarifa ya Jopo hilo la Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi. Taarifa hiyo ya jopo la kisayansi inapatikana katika tovuti ya IPCC.

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...