Mgeni rasmi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya TMA Dkt. Buruhani Nyenzi akizungumza kwa kusisitiza wakati akifungua warsha ya wadau ya kujadili utabiri wa msimu wa mvua za Masika 2021 unaotarajiwa kutolewa rasmi Tarehe 18 februari, 2021 katika ukumbi wa mikutano wa TMA, Ghorofa ya tatu, Ubungo Plaza - Dar es Salaam, Tanzania
Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi akifafanua jambo kwa wadau katika warsha ya kujadili utabiri wa msimu wa mvua za Masika 2021 unaotarajiwa kutolewa rasmi Tarehe 18 februari 2021 katika ukumbi wa mikutano wa TMA, Ghorofa ya tatu, Ubungo Plaza - Dar es Salaam, Tanzania
Wadau kutoka sekta mbalimbali katika picha ya pamoja na mgeni rasmi kwenye warsha ya wadau ya kujadili utabiri wa msimu wa mvua za Masika 2021 unaotarajiwa kutolewa rasmi Tarehe 18 februari, 2021 katika ukumbi wa mikutano wa TMA, Ghorofa ya tatu, Ubungo Plaza - Dar es Salaam, Tanzania
Matukio katika picha wakati wadau wakifuatilia mada mbalimbali zilizowasilishwa katika warsha ya wadau ya kujadili utabiri wa msimu wa mvua za Masika 2021 unaotarajiwa kutolewa rasmi Tarehe 18 februari, 2021 katika ukumbi wa mikutano wa TMA, Ghorofa ya tatu, Ubungo Plaza - Dar es Salaam, Tanzania
Wadau kutoka sekta mbalimbali wakiwasilisha athari na ushauri katika sekta zao kwenye warsha ya wadau ya kujadili utabiri wa msimu wa mvua za Masika 2021 unaotarajiwa kutolewa rasmi Tarehe 18 februari, 2021 katika ukumbi wa mikutano wa TMA, Ghorofa ya tatu, Ubungo Plaza - Dar es Salaam, Tanzania
Dar es Salaam; Tarehe 15 - 16 Februari, 2021;
Wadau wa hali ya hewa kutoka sekta mbalimbali wametakiwa kutumia taarifa za hali ya hewa ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi. Hayo yalizungumzwa na Mgeni Rasmi na Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Buruhani Nyenzi, wakati akifungua Mkutano wa Wadau wa Utabiri wa Mvua za Msimu wa Masika (Machi -Mei 2021), uliofanyika katika Ukumbi wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (The Law School of Tanzania), Dar es Salaam.
“Nichuke fursa hii kuwasihi wadau wote wa hali ya hewa katika sekta mbalimbali kujihusisha zaidi katika kuelewa na kufuatilia masuala ya hali ya hewa na mabadiliko yake ili kuweza kuchukua hatua stahiki za kujikinga na kukabiliana na athari zitokanazo na mabadiliko ya hali ya hewa. Kwa kufanya hivyo tutasababisha mazingira tunayoishi yaendelee kubaki salama na kuwa katika asili yake na yenye kuvutia kwa shughuli za kiuchumi na kijamii kwa kizazi hiki na vizazi vijavyo”. Alizungumza Dkt. Nyenzi.
Aidha, Dkt. Nyenzi aliendelea kwa kusema kuwa ni jukumu letu kuendelea kuelimishana kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa na namna ya kukabiliana nayo na wakati huo huo tukiendelea kutekeleza sera na mikakati ambayo itatusaidia kutumia vyema huduma za hali ya hewa katika kuinua uchumi wa nchi yetu, kutoka uchumi wa kati tuliofikia sasa kwenda uchumi wa juu zaidi.
“Mabadiliko ya tabia nchi ni halisi ambapo tumeshuhudia athari mbalimbali zinazotokana na mabadiliko haya ikiwa ni pamoja na kuwa na vipindi vya mvua kubwa, kubadilika kwa misimu ya mvua hasa tarehe za kuanza na kuisha kwa mvua, wote tumeshuhudia mvua zilizo nje ya msimu kwa mwaka huu wa 2021 katika maeneo ambayo kwa kawaida huwa ni makavu kwa miezi ya Januari na Februari, hali hii inasababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa (climate change)”. Alifafanua Dkt. Nyenzi.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi alieleza kuwa mkutano huo unalenga kujadiliana na kupata maoni ya wadau jinsi utabiri wa mvua za Masika utakavyoweza kutumika kwa tija katika sekta mbalimbali hapa nchini na hivyo kuendeleza na kuimarisha utoaji wa huduma za hali ya hewa na matumizi yake kwa jamii.
“Ipo haja ya kutambua uwezo wa utabiri wa hali ya hewa na hususan utabiri wa msimu kama zana yenye nguvu katika kusaidia watoa maamuzi kukabiliana na changamoto zinazosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa. Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Tumia taarifa za utabiri kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa”. Alisema Dkt. Kijazi.
Dkt. Kijazi aliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa jitihada za kuboresha miundombinu na huduma za hali ya hewa hapa nchini na kufanya huduma zinazotolewa na TMA kuendelea kuwa bora na kukidhi viwango vya kimataifa.
Kwa upande wake, mdau kutoka Wizara ya Kilimo Bw. Robert Dimoso alisema katika kipindi cha msimu wa mvua za vuli ulioanza oktoba mpaka Disemba 2020, maeneo mengi yalipata mvua za chini ya wastani hivyo kupelekea kupata unyevunyevu mzuri kwenye udongo ambao ulisaidia kustawi vizuri kwa mazao, hata hivyo kuna maeneo machache yalipata mvua za juu ya wastani hasa mikoa ya kanda ya ziwa ambayo ilichangia kuharibika kwa zao la maharage, lakini kwa ujumla utabiri uliendana na uhalisia kama ulivyotabiriwa.
Naye, mdau kutoka sekta ya Makazi Mijini Bw. Tim Ndezi alitoa pongezi zilizotolewa na wakazi wanaoishi katika makazi holela akisema wakazi hao wamefurahishwa sana na utabiri uliotolewa katika msimu uliopita kwani umekuwa sahihi sana na hata idadi ya watu wanaoathirika na mafuriko katika msimu uliopita imekuwa ni kidogo sana kama rekodi zinavyoonesha kwasababu watu walipata taarifa mapema na kuchukuwa tahadhari.
Bw. Simon Kadogosa kutoka Redcross alisema utabiri uliwasaidia katika kuboresha akiba ya vifaa vya uokozi na vilevile ulichangia katika kufanikisha miradi mbalimbali ambayo inafanyika kwa ushirikiano na Ofisi ya Waziri Mkuu hususan kwenye mikoa ya Iringa, Songwe na Arusha.