Monday, January 18, 2021

TMA YAENDELEA KUMILIKI CHETI CHA UBORA WA HUDUMA KWA VIWANGO VYA KIMATAIFA KWA KIPINDI CHA MIAKA KUMI (10) SASA.

 

Dar es salaam,Tarehe 16 Januari, 2021

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeendelea kumiliki cheti cha kimataifa cha uthibitisho wa utoaji huduma bora za hali ya hewa katika sekta ya usafiri wa anga kwa mara nyingine. Mamlaka ambayo imekuwa na cheti hiki kwa miaka kumi sasa, ni miongoni mwa Taasisi chache za hali ya hewa barani Afrika kufanikiwa kushikilia cheti hicho kwa kipindi kirefu.

Mafanikio hayo yamepatikanabaada ya kukamilika kwa ukaguzi uliofanyika kwa njia ya mtandao na Kampuni ya Kimataifa ya Certech kutoka Canada, kuanzia Tarehe 11 hadi 15 Januari 2021 katika vitengo na ofisi mbalimbali ndani ya Mamlaka, Makao Makuu na Mikoani. Ukaguzi huu ulifanyika kwa mujibu wa viwango vya ubora vilivyowekwa na Shirika la Viwango la Kimataifa (ISO 9001:2015) na ulimalizika kwa taarifa nzuri ya kwamba TMA imeboresha sana mifumo yake ya utoaji huduma na hivyo inastahili kuendelea kumiliki cheti hicho cha ubora cha kimataifa.

Akizungumzia mafanikio hayo, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi ambaye pia ni Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), alisema kuwa Mamlaka imeanza kumiliki cheti hicho cha ubora tangu mwaka 2011, ambapo Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza kwa Taasisi za Hali ya Hewa Kusini mwa Jangwa la Sahara kupata cheti hicho kwa vigezo vya ubora vilivyoainishwa katika mwongozo wa “ISO 9001:2008”, na ilipofika mwaka 2017 Tanzania kupitia TMA ilifanya kazi ya ziada kuhakikisha inafanikiwa kupata cheti kipya kwa mujibu wa vigezo vipya vya “ISO 9001:2015,” ambacho kiliifanya Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa kuwa nchi ya tatu barani Afrika ambayo taasisi yake ya hali ya hewa imepata cheti hicho kabla ya Septemba 2018 iliyokuwa ni mwisho wa matumizi ya cheti cha zamani.

“Mamlaka imekuwa ikikaguliwa kimataifa kila mwaka na mkaguzi kutoka nje ya nchi ili kuangalia ubora wa huduma zitolewazo, ni furaha kubwa kuona bado TMA inaendelea kuwa taasisi ya mfano kwa taasisi zingine za hali ya hewa barani Afrika na nje ya Afrika kwa kuendelea kukidhi viwango vya Kimataifa. Mpaka sasa TMA imefanikiwa kutoa mafunzo kwa baadhi ya taasisi za hali ya hewa katika nchi za SADC, EAC na zingine zikiwemo Saudi Arabia, Libya, Nigeria, Maldives, n.k kuhusu jinsi ya kufanikisha upatikanaji wa cheti hiki pamoja na kuboresha weledi wa wataalamu katika Taasisi zao za Hali ya Hewa. Mafanikio haya ni kutokana na ‘team work’ iliyopo baina ya menejimenti na watumishi wa Mamlaka, weledi, bidii na miongozo mizuri tuliyojiwekea ya kuhakikisha tunafanikiwa ikiwa ni pamoja na kufanyika kwa ukaguzi wa ndani mara kwa mara”. Alisema Dkt. Kijazi.

Aliongeza kwa kusema kwamba upatikanaji wa cheti hicho unaihakikishia dunia kwamba anga la Tanzania katika masuala ya hali ya hewa liko salama kwa ndege zote za kimataifa kuruka kwani ilishakubalika kimataifa kwamba kwa nchi ambazo taasisi zao za hali ya hewa hazijapata cheti hicho cha ubora ndege hazitaruka katika anga la nchi hizo. Dkt. Kijazi alisema TMA inajivunia kutoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi yetu kupitia sekta ya usafiri wa anga kwani katika viwanja vyote vya ndege nchini huduma za hali ya hewa zinatolewa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa. Hata katika viwanja ambavyo ndege hazitui kwa saa 24, TMA inaendelea kupima hali ya hewa katika viwanja hivyo kwa saa 24 ili kukidhi matakwa ya kimataifa katika utoaji wa huduma za hali ya hewa. Aliwapongeza watumishi wa TMA kwa kazi kubwa wanayoifanya kuhakikisha TMA inatimiza majukumu yake.

Awali wakati akikamilisha ukaguzi huo, mkaguzi wa nje kutoka Certech - Canada Bwana Frank Strohmeier, alisema TMA imekuwa ikiboresha kila mara mifumo yake ya utoaji huduma na hivyo kwa mwaka huu, hapakuwa na hoja (nonconformity) yoyote ambayo ingehitaji kutolewa maelezo na kupelekea kuhitajika kwa marekebisho katika mfumo wa utoaji huduma. Hivyo maeneo yote ambayo TMA imekaguliwa yamekuwa na ubora wa hali ya juu pasipo kuwa na mapungufu yoyote. Alifurahishwa na jinsi ambavyo ukaguzi umefanyika kwa njia ya mtandao ukiwa na mafanikio makubwa pasipo changamoto yoyote ya teknolojia hivyo akawapongeza sana wataalam wa ICT wa TMA kwa kufanya kazi zao kwa weledi. Alimalizia kwa kuipongeza menejiment nzima ya TMA kwa kazi nzuri inayofanyika.

“Nawapongeza sana kati ya taasisi za hali ya hewa ambazo kampuni yangu imekagua katika nchi mbali mbali duniani sijawahi kuona taasisi ambayo huduma zake zinaendelea kuwa bora mwaka hadi mwaka kama ilivyo kwa TMA. Mwaka huu sina hoja yoyote mifumo yote imeboreshwa, wafanyakazi wana weledi wa hali ya juu na wanafahamu wanachokifanya, taratibu zote mlizojiwekea mnazitekeleza ikiwemo jinsi ya kutoa utabiri na kuufikisha kwa watumiaji katika sekta ya usafiri wa anga kwa wakati, utoaji wa tahadhari za hali mbaya ya hewa katika anga, uhakiki wa usahihi wa utabiri unaotolewa katika sekta ya usafiri wa anga, upimaji wa weledi wa watumishi wanaofanyakazi katika viwanja vya ndege, hali ilivyokuwa 2018 sivyo ilivyo 2019 uboreshaji ni wa hali ya juu, nawapongeza sana”. Alisema Bwana Frank kutoka kampuni ya Certech iliyoko nchini Canada.

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...