|
Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani
(WMO) Kanda ya Afrika, Dkt. Daouda Konate (kushoto aliyevaa miwani) aliyekuwa
Mwenyekiti wa Kikao akimsikiliza Katibu Mkuu wa WMO, Prof. Petteri Taalas
(kushoto aliyekaa katikati ya wataalamu) akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa
shughuli za WMO katika Kanda ya Afrika (RA I) katika Mkutano wa viongozi wa WMO
Kanda ya Afrika (WMO Regional Association I Management Group) uliofanyika kwa
njia ya mtandao tarehe 10 hadi 12 Juni 2020.
|
|
Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika
la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi akichangia katika taarifa ya
utekelezaji wa shughuli za WMO katika Kanda ya Afrika (RA I) iliyowasilishwa na
Katibu Mkuu wa WMO, Prof. Petteri Taalas katika
Mkutano wa viongozi wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Kanda ya
Afrika (WMO Regional Association I Management Group) uliofanyika kwa njia ya
mtandao tarehe 10 hadi 12 Juni 2020. |
Dar es Salaam;
Mamlaka
ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema iko tayari kushirikiana na Taasisi za
Hali ya Hewa za Nchi Wanachama wa
Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO)
Kanda ya Afrika (WMO Regional Association
I (RA I), kusaidia kuboresha huduma za hali ya hewa katika maeneo ambayo
imekwisha kupiga hatua zaidi. Hayo yalisemwa
katika Mkutano wa Viongozi wa WMO Kanda ya Afrika (RA I Management Group), uliofanyika
kwa njia ya mtandao (videoconference) kuanzia tarehe 10 hadi 12 Juni, 2020.
Akizungumza
wakati akichangia taarifa ya utekelezaji wa shughuli za WMO katika Kanda ya
Afrika iliyowasilishwa na Katibu Mkuu wa WMO Prof. Petteri Taalas, Mkurugenzi
Mkuu wa TMA ambaye pia ni Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi alieleza kwamba
Tanzania imepiga hatua katika uandaaji wa majarida ya taarifa za klaimatolojia
(hali ya hewa ya muda mrefu) kwa nchi ya Tanzania, hivyo iko tayari kusaidia nchi
nyingine Wanachama wa WMO Kanda ya Afrika.
“Kuhusiana
na uandaaji wa taarifa za klaimatolojia (hali ya hewa ya muda mrefu), nafurahi
kusema kwamba Tanzania tumekwishaanza kutoa machapisho hayo tangu mwaka 2011 na
tuko tayari kusaidia katika ngazi ya Kanda”. Alisema Dkt. Kijazi.
Aidha,
aliendelea kusisitiza utayari wa Tanzania katika kusaidia nchi zingine wakati
akielezea faidi za kuwa na Mfumo wa Kitaifa wa Huduma za Hali ya Hewa (National
Framework for Climate Services) ambapo alisema kwa upande wa Tanzania, mfumo
huo umesaidia kuboresha sana huduma za hali ya hewa. Moja ya uboreshaji huo ni kutungwa kwa sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa
Na. 2 ya mwaka 2019 ambayo ina malengo ya kuiwezesha TMA kusimamia vyema huduma
zote za hali ya hewa zinazotolewa nchini Tanzania na hivyo kutekeleza vyema
program zote za WMO kwa ustawi wa wananchi wa Tanzania na dunia kwa ujumla hasa
ikizingatiwa kwamba hali ya hewa haina mipaka. Aliongeza Dr. Kijazi.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu wa WMO alimpongeza Dr. Kijazi kwa umahiri anaoonyesha
katika kushiriki kwenye program za WMO katika nafasi yake kama Mwakilishi wa
kudumu wa Tanzania katika Shrika la Hali ya Hewa Duniani na kama Makamu wa tatu
wa rais wa shirika hilo. Aidha, aliipongeza Tanzania kuwa imefanya kazi kubwa
katika kutekeleza program za WMO ikiwemo program ya Global Framework for
Climate services na akasema WMO inafurahishwa na utayari wa Tanzania kusaidia
nchi zingine barani Afrika.
Kwa
upande mwingine, Mkurugenzi wa WMO Ofisi ya Kanda ya Afrika, Dkt. Amos Makarau
alitoa taarifa ya wataalamu walioteuliwa kuongoza majopo na vikosi kazi mbalimbali
vya WMO, ambapo taarifa hiyo ilibainisha uteuzi wa Mkurugenzi wa Miundombinu na
Huduma za Ufundi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Dkt. Pascal Waniha kuwa
Makamu Mwenyekiti (Vice Chair) wa Kikosi Kazi cha Mtandao wa Dunia wa Upimaji wa
Hali ya Hewa (Study Group on Global Basic Observing Network (GBON), akiwa
miongoni mwa wataalamu watatu (3) walioteuliwa kutoka Afrika kuongoza majopo na
vikosi kazi vya WMO. Hii ni sifa na
heshima kwa Tanzania na TMA.
Awali
akifungua mkutano huo, Mwenyekiti ambaye ni Rais wa Shirika la Hali ya Hewa
Duniani (WMO) Kanda ya Afrika, Dkt. Daouda Konate kutoka Ivory Coast alisema lengo
la mkutano ni kujadili utekelezaji wa shughuli za huduma za hali ya hewa katika
Kanda ya Afrika. Mkutano ulijadili masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na
shughuli za WMO katika Kanda ya Afrika; utekelezaji wa maazimio ya Mkutano Mkuu
wa WMO (WMO Congress) wa mwezi Juni, 2019; Uteuzi wa wataalamu katika majopo na
vikosikazi vya WMO; Vipaumbele vya Kanda; Mpango Mkakati wa Kanda; na athari za
janga la ugonjwa wa “COVID-19” katika huduma za hali ya hewa.
Aidha,
baada ya majidiliano ya kina, mkutano ulikuja na mapendekezo ambayo ni pamoja na: kutoa nafasi kwa watunga sera
kushiriki katika mikutano ya Kanda ya Masuala ya hali ya hewa; na kuziomba Nchi
Wanachama kuridhia katiba ya Kamati ya Mawaziri wenye dhamana ya hali ya hewa
“African Ministerial Conference on Meteorology (AMCOMET).