Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Bi. Theo
Ntara ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kyela (watatu
kutoka kushoto), Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu TMA Dkt. Hamza Kabelwa (wa nne
kutoka kushoto) katika picha ya pamoja na washiriki wa warsha inayohusu uboreshaji
wa huduma za hali ya hewa katika maeneo ya Ziwa Nyasa kwa sekta ya wakulima na
wafugaji, wavuvi na wasafirishaji, tarehe 14 Mei 2015 katika hotel ya Kyela Resort-Mbeya
Mamlaka
ya Hali ya Hewa kwa kushirikiana na Shirika la Hali ya Hewa Duniani kupitia mpango
wa utoaji wa huduma za hali ya hewa wa GFCS yaani “Global Framework for Climate Services” imezindua rasmi huduma ya kutoa taarifa za hali ya hewa
hususan tahadhari na utabiri mahususi kwa watumiaji wa ziwa nyasa. Taarifa hizo
zitasamabazwa kupitia vyombo mali mbali vya habari ikiwemo redio za kijamii.
Huduma hiyo ilizinduliwa rasmi tarehe 11 Mei 2015 huko Kyela mkoani Mbeya na Mheshimiwa
Mkuu wa Wilaya ya Kyela Dkt. Thea Ntara aliyemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.
Katika
kuhakikisha huduma hiyo inakuwa endelevu TMA wameandaa warsha ya “UBORESHAJI NA UAINISHAJI WA MAHITAJI YA
HUDUMA ZA HALI YA HEWA KATIKA MAENEO YA ZIWA NYASA KWA WAKULIMA NA WAFUGAJI,
WAVUVI NA WASAFIRISHAJI’’ iliyofanyika
katika hotel ya Kyela Resort jijini Mbeya. Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa
Mkoa wa Mbeya Bi. Thea Ntara alisema ‘Hivi karibuni tumeshuhudia matukio ya
mvua ya mawe, mafuriko na radi katika baadhi ya maeneo ya mkoa wa Mbeya, hali
hii imesababisha madhara makubwa ya kijamii na kiuchumi. Nimatumaini yangu kuwa
taarifa zinazopatikana kutoka kwa wananchi na wataalam mbalimbali kupitia
semina hii zitaiwezesha Mamlaka ya Hali ya Hewa kuboresha taarifa zake kwa umma
na kuwawezesha watalaam kutoa ushauri stahiki unaozingatia taarifa za hali ya
hewa’. Alizungumza hayo wakati akifungua rasmi warsha ya wadau wa hali ya hewa wanaotumia
ziwa nyasa iliyowajumuisha wasafirishaji, wakulima, wavuvi, wafugaji, Ofisi ya
Bandari, SUMATRA,usalama, Maafa, maliasili na vyombo vya habari.
Nae
Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt Agnes Kijazi katika hotuba yake iliyowasilishwa na
Mkurugenzi wa Utabiri TMA Dkt. Hamza Kabelwa alisema ‘Katika kuhakikisha TMA
inazidi kuziboresha huduma zake, wataalam wa TMA wameweza kutembelea maeneo mbalimbali
ya Wilaya ya Kyela ili kupata uelewa zaidi wa majanga yanayoikumbuka wilaya
hiyo na namna gani ya kuweza kufanyia kazi’.
‘TMA kwa kushirikiana na wadau mbalimbali vikiwemo vyombo vya habari
imejikita katika kuhakikisha jamii inapata taarifa za hali ya hewa kwa wakati
hususan kunapokuwa na vipindi vya matukio
ya hali mbaya ya hewa kama vile mvua kubwa, ukame, upepo mkali, mawimbi
makubwa n.k kwa lengo la kuisaidia jamii
kuchukua tahadhari mapema ili kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na
matukio hayo hivyo kuchangia katika
kuokoa maisha ya watu na mali zao’ alisema Dkt. Kijazi.
IMETOLEWA NA MONICA MUTONI AFISA HABARI MAMLAKA YA
HALI YA HEWA TANZANIA.