Wednesday, April 24, 2019

MWENDELEZO WA TAARIFA YA KIMBUNGA KENNETH

Kaimu Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania(TMA) dkt. Paschal Waniha, mbele ya waandishi wa habari  akichambua  mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa kuelezea mrejeo wa mwenendo wa mgandamizo mdogo wa hewa uliopewa jina la "Kenneth" katika bahari ya Hindi

Taarifa hii inatoa mrejeo wa mwenendo wa mgandamizo mdogo wa hewa uliopewa jina la “Kenneth” katika bahari ya Hindi na athari zake kwa maeneo mbalimbali hapa nchini.
 
Katika kipindi cha saa 24 zilizopita, mgandamizo mdogo wa hewa (Kenneth) umeendelea kuimarika kwa kasi hadi kufikia kiwango cha kimbunga kamili. Kimbunga Kenneth kwa sasa kipo umbali wa takribani kilometa 700 mashariki mwa Mtwara. Mifumo ya hali ya hewa inaonesha kimbunga Kenneth kilichopo eneo la kaskazini magharibi mwa kisiwa cha Madagascar kinaambatana na mvua kubwa na upepo mkali katika eneo hilo. Aidha, vipindi vya upepo mkali unaofikia na kuzidi kasi ya kilometa 80 kwa saa vinatarajiwa kujitokeza katika ukanda wa pwani ya kusini (Lindi na Mtwara). Kimbunga hicho kinaendelea kutawala mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini, hivyo kusababisha ongezeko la mvua zinazoambatana na ngurumo za radi pamoja na upepo mkali kadri kinavyokaribia maeneo ya ukanda wa pwani.
Kimbunga hiki kitakapoingia nchi kavu kikiwa na nguvu inayotarajiwa kitakuwa na madhara makubwa kwa maisha ya watu na mali zao. Madhara yanayotarajiwa ni pamoja na mtawanyiko mkubwa wa mafuriko, uharibifu wa mali na makazi, kuezuliwa mapaa kutokana na upepo mkali, uharibifu wa mazao mashambani, miundombinu kutokana na mafuriko na upepo mkali, kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari katika kipindi kifupi (storm surge), kuathirika kwa shughuli za usafirishaji kwa njia ya anga, kwenye maji na nchi kavu inaweza kuathirika hasa katika mkoa wa Mtwara na maeneo jirani (umbali wa kilometa 500).
Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania inaendelea kufuatilia mwenendo wa kujengeka kwa kimbunga hicho kusini magharibi mwa bahari ya Hindi pamoja na mwenendo wa mifumo mingine ya hali ya hewa kwa ujumla na itaendelea kutoa taarifa za mrejeo kila itakapobidi.

USHAURI: Wananchi wanashauriwa kuendelea kufuatilia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania na kuzingatia tahadhari zilizotolewa na mirejeo yake pamoja na kupata na kuzingatia ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

Imetolewa tarehe 24 Aprili 2019 na:
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania

KIMBUNGA KENNETH23/04/2019

Taarifa hii inatoa mrejeo wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa katika bahari ya Hindi na athari zake kwa maeoneo mbalimbali hapa nchini.

Mifumo ya hali ya hewa inaonesha kuendelea kuimarika kwa mgandamizo mdogo wa hewa uliopewa jina la “Kenneth” katika eneo la kaskazini magharibi mwa kisiwa cha Madagasca ambao unambatana na mvua kubwa na upepo mkali katika eneo hilo. Mgandamizo huo unaendelea kusababisha mawingu mazito na ongezeko la mvua katika maeneo mengi hapa nchini hususan katika maeneo ya kanda ya ziwa Victoria, nyanda za juu kaskazini mashariki na ukanda wa pwani. Aidha, vipindi vya upepo mkali unaofikia kasi ya kilometa 40 kwa saa vimeendelea kujitokeza katika ukanda wa pwani kama ilivyotabiriwa na vinatarajiwa kuendelea. Hata hivyo, pamoja na kuendelea kuimarika kwa mgandamizo huo bado haujafika kiwango cha kimbunga kamili na upo umbali wa takribani kilometa 1000 mashariki mwa Mtwara. Inatarajiwa kuwa Mgandamizo huo utaendelea kuimarika kwa kasi na kufikia kiwango cha kimbunga kamili “Kenneth” kati ya tarehe 25 na 26 April 2019 na kuendelea kutawala mwenendo wa Mifumo ya hali ya hewa hapa nchini.

Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania inaendelea kufuatilia mwenendo wa kujengeka kwa mfumo huo uliopo kusini magharibi bahari ya Hindi pamoja na mwenendo wa mifumo mingine ya hali ya hewa kwa ujumla na itatoa taarifa za mrejeo kila itakapobidi.

USHAURI: Wananchi wanashauriwa kuendelea kufuatilia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania na kuzingatia tahadhari zilizotolewa na mirejeo yake pamoja na kupata na kuzingatia ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

Imetolewa na:
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania

Wednesday, April 17, 2019

TMA - JARIDA LA HABARI TOLEO LA 2


Kwa taarifa zaidi tembelea: http://www.meteo.go.tz/news/189

TMA YAPATA MAFUNZO YA KUTUMIA MFUMO WA SERIKALI WA KIELEKRONIKI KATIKA UKUSANYAJI WA MAPATO YA SERIKALI (GePG)).


Washiriki wa mafunzo ya kutumia mfumo wa serikali wa kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato katika picha ya pamoja na mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya hali ya hewa dkt. Agnes Kijazi (katika ya waliokaa)
Matukio mbalimbali katika picha wakati wafanyakazi wa TMA wakipata mafunzo ya kutumia mfumo wa serikali wa kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato ya serikali (GePG).

12/04/2019; DAR ES SALAAM

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imepata mafunzo ya kutumia mfumo wa serikali wa kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato ya serikali (GePG) ikiwa niutelezaji wa sheria ya fedha za umma, sura 348 iliyopitishwa na bunge kifungu cha 44 cha mwaka 2017.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Agnes Kijazi alieleza kuwa mafunzo hayo ni mwendelezo wa juhudi za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) katika kutekeleza maelekezo yote yanayotolewa na Serikali inayoongozwa na mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa lengo la kuongeza tija na ufanisi katika utoaji huduma bora kwa umma. Alisisitiza kwamba mafunzo hayo yataiwezesha Mamlaka kuboresha njia za ukusanyaji wa mapato na hivyo kutoa huduma bora kwa wananchi.

Kwa upande wa washiriki wa mafunzo hayo, meneja wa fedha na uhasibu Bw. Michael Ntagazwa alieleza faida za mfumo huo kuwa ni kuboresha utendaji kazi ikiwa pamoja na urahisi katika kuandaa na kupata taarifa za mapato kwa vituo vyote na kwa wakati wowote.

Naye mtaalam kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Jane Kazoba alieleza kuwa mfumo huo umeunganishwa na ofisi mbalimbali zinazokusanya mapato ya serikali zikiwemo wizara na taasisi zake na taasis zinazotoa huduma za fedha nchini.

Imetolewa:
Ofisi ya Uhusiano
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)

Monday, April 1, 2019

MHE. NDITIYE ASHUHUDIA SERIKALI IKISAINI MKATABA WA KUFUNGA RADA NYINGINE MBILI ZA HALI YA HEWA MKOA WA MBEYA NA KIGOMA

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akizingumza na waandishi wakati wa kusaini mikataba ya upatikanaji wa Rada mbili za hali ya hewa kwa mikoa ya Mbeya na Kigoma, kulia ni mwakilishi wa ECC kutoka Marekani Bw. Edwin Kasanga na kushoto ni mkurugenzi mkuu wa TMA Dkt. Agnes Kijazi
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akizingumza na waandishi wakati wa kusaini mikataba ya upatikanaji wa Rada mbili za hali ya hewa kwa mikoa ya Mbeya na Kigoma, kulia ni mwenyekiti wa bodi ya ushauri ya TMA Dkt. Buruhani Nyenzi na kushoto ni mkurugenzi mkuu wa TMA Dkt. Agnes Kijazi
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akishuhudia tukio la kusainiana mikataba ya upatikanaji wa Rada mbili za hali ya hewa kwa mikoa ya Mbeya na Kigoma, pamoja na mwenyekiti wa bodi ya ushauri ya TMA Dkt. Buruhani Nyenzi na wanasheria wa TMA na ECC
Mwenyekiti wa bodi ya ushauri ya TMA Dkt. Buruhani Nyenzi akizungumza wakati wa kusaini mikataba ya upatikanaji wa Rada mbili za hali ya hewa kwa mikoa ya Mbeya na Kigoma 

Baadhi ya wafanyakazi wa TMA na wanahabari wakishuhudia tukio la kusainiana kwa mikataba ya upatikanaji wa Rada mbili za hali ya hewa kwa mikoa ya Mbeya na Kigoma 

Serikali ya awamu ya tano imejizatiti katika kuhakikisha huduma za hali ya hewa nchini zinakuwa za viwango vya kimataifa na za usahihi wa hali ya juu. Katika kufanikisha hili Serikali ya awamu ya tano iliahidi kuendelea kuongeza mtandao wa Rada za hali ya hewa ili kufikia Rada saba (7) zinazohitajika kwa nchi nzima.
Serikali kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, imesaini mkataba wa ununuzi wa Rada mbili za hali ya hewa zitakazofungwa eneo la Kawetere katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya na eneo la Nyamoli katika barabara ya kuelekea Bulombora, Kigoma na hivyo kuifanya Tanzania kuwa na jumla ya mtandao wa rada tano (5). Ikumbukwe kuwa tayari Mamlaka imeishafunga rada mbili za hali ya hewa huko Kiseke Mwanza na Bangulo Dar es Salaam pia imeanza utaratibu wa ufungaji wa Rada Mtwara. Hii inaifanya Tanzania kuwa Taasisi bora kwa uangazi wa wa hali ya hewa kwa njia ya Rada katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Ununuzi wa Rada hizi mbili (ya nne na ya tano) kwa ajili ya Mbeya na Kigoma umegharimu kiasi cha Tshs. 5,715,971,148.45 (USD 2,497,125) kwa kila moja na pia utengenezaji na ufungaji wa rada zote mbili utachukua muda wa miezi kumi na nne hadi kukamilika kwake.  Mtengenezaji wa Rada hizo ni Enterprise Electronics Corporation (ECC)
Rada hizi zina uwezo wa kuona hadi kilometa za mkato 450 (Aerial distance) huku zikizunguka (radius distance) na uwezo halisia wa kuona mpaka matone madogo sana ya mvua ni kilometa za mkato 250.
Rada za hali ya hewa ni moja ya mitambo inayotumika kufanya uangazi wa hali ya hewa wa masafa marefu. Mitambo hii husaidia katika kukusanya data za hali ya hewa zinazoonesha uhalisia wa anga kipindi Radar inapozunguka. Rada inasaidia;
·        Kujua kwa wakati maeneo yenye mvua, aina ya mawingu yaliyopo na wakati mwingine hata kujua ni kiasi gani cha mvua kinachotarajiwa.
·        Kufuatilia maeneo yenye mvua kubwa na za mawe zinazoambatana na radi na upepo mkali hivyo kuweza kutoa tahadhari kwa muda muafaka.

·        Kufuatilia muelekeo wa mifumo inayosababisha hali mbaya ya hewa (mvua za mawe, upepo mkali na dhoruba).

·        kufuatilia vimbunga baharini kadri ya upeo wake na hivyo kuweza kutoa tahadhari kutokana na mwenendo wa vimbunga hivyo.

·        Kufuatilia upepo unaoweza kuleta madhara kwa usalama wa usafiri wa anga (wind shear) na


·        Kutoa ushauri kwa watumiaji wa huduma za hali ya hewa ili wachukue tahadhari wakati wa shughuli zao kiuchumi na kijamii.

·        Kusaidia kutoa utabiri wa muda mfupi na wakati wa hali mbaya ya hewa.

Wito unatolewa kwa wananchi wote kutoa ushirikiano katika kulinda na kutunza mitambo hii ya Rada pamoja na vifaa vyote vya hali ya hewa kwa manufaa ya Taifa letu.


MATUKIO MBALIMBALI WAKATI WA BARAZA LA WAFANYAKAZI WA TMA