Saturday, December 15, 2018

COP24: TANZANIA YATUMIA FURSA KUHAMASISHA ONGEZEKO LA WATAALAM KUTOKA AFRIKA KATIKA SEKRETARIET YA SHIRIKA LA HALI YA HEWA DUNIANI (WMO)


Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inashiriki Mkutano wa 24 wa Mabadiliko ya Hali ya Hewa (Climate Change Conference 24) unaoendelea huko Katowice, Poland kuanzia tarehe 3 hadi 14 Desemba 2018.

Mkutano huo umewakutanisha wadau mbalimbali kutoka duniani kote wakiwemo viongozi wa nchi, mashirika ya kimataifa, taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali n.k. Ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhe. Mussa Sima

Prof. Petteri Taalas (wa pili kutoka kulia) Katibu Mkuu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (World Meteorological Organization) katika picha ya pamoja na Mhe. Mboni Mhita (MB) (wa pili kutoka kushoto) na mjumbe wa bunge la  Pan-Africa, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania  Dkt. Agnes Kijazi na  Bw. Marcellin Kokou Nakpon(wa kwanza kushoto),  Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Hali ya Hewa ya Benin 

Kupitia mkutano huo, Mbunge wa Handeni Vijijini Mhe. Mboni Mhita na Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi walipata fursa ya kuongea na Katibu Mkuu wa WMO na kujadili masuala mbali mbali yanayohusu ushiriki wa Taasisi za Hali ya Hewa za Afrika katika kutekeleza programu za WMO na misaada WMO inayoweza kutoa kuziwezesha taasisi hizo ikiwa pamoja na kuongeza wataalam kutoka Afrika katika Secretariat ya WMO.

Aidha mhe. Mboni aliiomba WMO kuendelea kuzisaidia nchi za Afrika kupata vifaa vya kisasa kulingana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa ili kufanikisha utoaji wa taarifa sahihi za hali ya hewa kwa maendeleo endelevu.

Aliongezea kwa kutoa mfano wa umuhimu wa taarifa za hali ya hewa kwa jimbo lake, ambapo alielezea namna walivyo nufaika na kilimo cha mhogo (mazao yanayostahimili ukame) baada ya kupata utabiri wa msimu mvua kutoka TMA.

Kwa upande wa Dkt. Kijazi aliwashukuru WMO kwa ushirikiano wanaoendelea kuutoa kwa TMA ikiwemo kufadhili baadhi ya miradi ya huduma za hali ya hewa nchini.

No comments:

Post a Comment