TMA YAKAA KIKAO KAZI CHA KUANDAA MPANGO MKAKATI WA UJUMUISHAJI WA MASUALA YA JINSIA NA MAKUNDI MAALUM KATIKA UTOAJI WA TAHADHARI ZA HALI MBAYA YA HEWA
Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Hali ya Hewa na Mabadiliko ya Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a, alifungua kikao kazi cha kuandaa mpango mkakati wa ujumuishaji wa masuala ya jinsia na makundi maalum katika utoaji wa tahadhari za hali mbaya ya hewa, kilichofanyika kuanzia tarehe 12 hadi 15 Januari 2026 jijini Dodoma katika ukumbi wa Morena Hotel.
Kikao kazi hicho kililenga kujumuisha masuala ya jinsia na makundi maalum katika utoaji wa taarifa za tahadhari za hali mbaya ya hewa hapa nchini Tanzania, kwa lengo la kuimarisha mifumo ya utoaji wa tahadhari ili jamii zilizo katika mazingira hatarishi ziweze kupata taarifa sahihi, zilizoimarishwa na kwa wakati, hivyo kupunguza athari za majanga yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Dkt. Chang’a alisema kuwa TMA imekuwa taasisi ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki miongoni mwa nchi zinazotekeleza mradi wa CREWS – Climate Risk and Early Warnings System (East Africa Project) kuchukua hatua ya kihistoria ya kuandaa mpango mkakati wa kuingiza masuala ya jinsia na makundi maalum katika utoaji wa tahadhari za hali mbaya ya hewa. Alisisitiza kuwa mpango huo, ambao ni wa kwanza kuandaliwa na TMA na Afrika kwa ujumla, umeiweka Tanzania katika historia ya kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuandaa mpango mkakati wa aina hiyo, hatua itakayoongeza ufanisi katika huduma za hali ya hewa.
Aliongeza kuwa mpango huo unatarajiwa kuwa mfano bora kwa nchi nyingine za Afrika.
Kwa upande wake, Joan Kimaku, Afisa wa Kikanda wa UN Women, aliipongeza TMA kwa kuwa taasisi ya kwanza kukubali na kuchukua hatua za haraka katika utekelezaji wa mpango mkakati huu muhimu wa ujumuishaji wa masuala ya kijinsia katika mifumo ya tahadhari za hali mbaya ya hewa.
Washiriki wa kikao kazi hicho walitoka katika taasisi mbalimbali zikiwemo Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Watoto, Norges Vel, UNDP na UN Women.





No comments:
Post a Comment