Sunday, December 28, 2025

HALI YA MVUA KUBWA NCHINI

 HALI YA MVUA KUBWA NCHINI


Dar es Salaam, 28 Desemba, 2025:
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inapenda kutoa taarifa ya mwenendo wa Mvua Kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali hapa nchini. 

Mnamo tarehe 26 hadi 27 Desemba, 2025 Mamlaka iliendelea kutoa Tahadhari ya vipindi vya Mvua Kubwa katika maeneo mengi nchini kuanzia tarehe 26 hadi 29 Desemba, 2025. Kwa mujibu wa Tahadhari hiyo maeneo yaliyotarajiwa kuathirika na vipindi hivi vya mvua kubwa ni pamoja na Mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe, Dodoma, Singida, Songea, Morogoro, Lindi, Mtwara, Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga, Dar es Salaam, Pwani (ikijumisha Kisiwa cha Mafia) pamoja na Visiwa vya Unguja na Pemba. 

Kuanzia usiku wa kuamkia leo hadi hivi sasa maeneo mengi nchini yameendelea kupata vipindi vya Mvua Kubwa zikiambatana na upepo mkali na hivyo kusababisha uharibifu wa mali na miundombinu katika baadhi ya maeneo hapa nchini. Hadi kufikia saa 3:00 kamili asubuhi ya leo viwango vya mvua kubwa vinavyozidi milimita 50 ndani ya saa 24 vilipimwa katika vituo vya Same (milimita 94.5), Morogoro (milimita 58.6) na Tabora (milimita 55.4). Aidha, viwango vya mvua vilivyopimwa katika vituo vingine ni pamoja na Hombolo (milimita 49.5), Kibaha (milimita 43.6), Dodoma (milimita 36.6) na Iringa (milimita 35.6). 

Hadi muda huu tumepokea taarifa kuwa mvua hizo zimesababisha athari katika miundombinu ya reli ya zamani ya MGR kwa kuathiri madajara katika eneo la Kidete, Wilaya ya Kilosa Mkoa wa Morogoro na Gulwe Wilaya   Dodoma; kusababisha hitilafu za umeme wa TANESCO pamoja na umeme wa SGR; na pia Barabara kuu ya Morogoro - Iringa eneo la Mama Marashi - Mikumi kumetokea maporomoko ya mawe na tope kurundikana barabarani.

Mvua hizo zimesababisha miundombinu na shughuli za usafiri wa abiria na shehena kwa ujumla kuathirika, hususan kupitia Reli ya SGR.

Kwa ujumla Serikali inaendelea na juhudi za kurejesha hali hiyo katika hali yake ya kawaida. 

Mifumo ya hali ya hewa iliyopo kwa sasa inaonesha kuendelea kuimarika kwa Ukanda Mvua na hivyo kuendelea kusababisha vipindi vya Mvua Kubwa katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Mara, Simiyu, Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe, Morogoro, Ruvuma, Lindi na Mtwara kwa siku ya kesho tarehe 29 Desemba, 2025. 

USHAURI: Wananchi wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa mara kwa mara kila inapobidi.
 


Saturday, December 20, 2025

TMA YASISITIZA UMUHIMU WA KUFUATILIA NA KUZINGATIA TAARIFA ZA HALI YA HEWA

 Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ( TMA) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa Duniani ( IPCC) Dkt. Ladislaus Chang'a akieleza umuhimu wa kufuatilia na kuzingatia taarifa za hali ya hewa pamoja na tahadhari za hali mbaya ya hewa wakati wa kikao cha kamati ya Wataalam ya Kitaifa ya Usimamizi wa Maafa tarehe 19 Disemba, 2025 Jijini Dodoma


Kikao hicho kiliongozwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Dkt. Jim Yonazi






Tuesday, December 16, 2025

MAFUNZO YA USIMAMIZI WA MIRADI YA MAENDELEO KWA MENEJIMENTI YA MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA

 MAFUNZO YA USIMAMIZI WA MIRADI YA MAENDELEO KWA MENEJIMENTI YA MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA 











Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya hewa Tanzania (TMA) na Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani(WMO), Dkt. Ladislaus Chang'a  alifungua  mafunzo ya usimamizi wa miradi ya  maendeleo kwa menejimenti ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) yanayoendeshwa na Chuo Cha Uhasibu Arusha (IAA),  ambapo mafunzo hayo yamejikita zaidi  katika usimamizi wa miradi ya uwekezaji wa miundombinu kama “Capital Expenditure (CapEx)”.


 Dkt. Chang'a katika ufunguzi alisema kuwa TMA ikiwa ni Taasisi ya Serikali  iliyopewa majukumu ya kutoa huduma za hali ya hewa, kuratibu na kudhibiti shughuli zote zinazohusiana na masuala ya hali ya hewa nchini. Mamlaka inashiriki pia kutekeleza miradi mbalimbali yenye malengo yanayochangia kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya TMA ya kitaifa, kikanda na kimataifa.


Aidha, alieleza kuwa miongoni mwa miradi ambayo inatekelezwa na TMA ni ikiwemo miradi ya uwekezaji wa miundombinu mbalimbali “Capital Expenditure (CapEx)”, Ujenzi wa Kituo cha Ufuatiliaji wa matukio ya Tsunami (Tsunami Centre), TMA inapata ufadhili wa kujenga vituo vipya vitatu (3) vya kupima hali ya hewa katika anga za juu kupitia mradi wa (SOFF) na nyinginezo nyingi. 


Kwa upande wake Mtiva wa Kitivo cha Mafunzo ya Insia na Sayansi za Jamii, Dkt. Leticia Rwabishungi wa chuo Cha Uhasibu Arusha aliwashukuru sana  TMA kwa kufika  IAA kwa mafunzo  ya usimamizi wa miradi na kusema chuo kina kozi nyingi sio tu Uhasibu bali kozi mbalimbali na kwa ngazi zote hivyo aliwakaribisha kuendelea kupata mafunzo katika chuo cha IAA.


Mojawapo ya walioshiriki katika ufunguzi wa mafunzo hayo ni  Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Mkurugenzi wa Huduma za Ushauri wa Chuo cha IAA,  Menejimenti ya Mamlaka ya Hali ya Hewa, Wakufunzi kutoka Chuo cha IAA, Wataalamu mbalimbali kutoka TMA, IAA na UNDP.


Mafunzo haya yameanza Disemba 15 mpka 19, mwaka 2025.

TMA YAPONGEZWA KWA KUIMARISHA IMANI YA WATANZANIA KUPITIA TAARIFA SAHIHI ZA HALI YA HEWA





Arusha 15 Disemba 2025,

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilipata fursa adhimu ya kutembelewa na Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa David Kihenzile(MB), katika Mkutano Mkuu wa 18 wa Tathmini ya Utendaji wa Sekta ya Uchukuzi. Mkutano huo ulifanyika katika Ukumbi wa AICC, Jijini Arusha.

Katika mkutano huo, Mheshimiwa Naibu Waziri aliipongeza Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kwa mchango wake mkubwa katika utoaji wa taarifa sahihi na za kuaminika za hali ya hewa, ambazo zimeendelea kusaidia kuboresha usalama na ufanisi katika sekta ya uchukuzi na kuwa taasisi yenye kuaminiwa na Watanzania.

Mkutano huo unafanyika kwa muda wa siku tatu, kuanzia tarehe 15 - 17 Desemba 2025 na kuwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya uchukuzi.

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...