Wednesday, February 12, 2025

HALI YA JOTO NCHINI


 Dar es Salaam, 12 Februari, 2025:

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inapenda kutoa taarifa ya hali la joto katika maeneo mbalimbali nchini.

Kumekuwepo na ongezeko la joto katika baadhi ya maeneo nchini hususan yapatayo misimu miwili ya mvua kwa mwaka kwa miezi ya hivi karibuni. Hali hii imesababishwa na kusogea kwa jua la utosi sambamba na upungufu wa mvua unaojitokeza katika maeneo hayo. Kwa kawaida vipindi vya jua la utosi nchini hufikia kilele mwishoni mwa mwezi Novemba wakati jua la utosi likiwa linaelekea kusini (Tropiki ya Kaprikoni) na hali hiyo hujirudia tena mwezi Februari wakati jua la utosi likiwa linaelekea kaskazini (Tropiki ya Kansa). Jua la utosi huambatana na hali ya ongezeko la joto kwa sababu uso wa dunia katika eneo tajwa huwa karibu zaidi na jua kuliko maeneo mengine.

Katika kipindi cha mwezi Februari, 2025 hali ya ongezeko la joto imeendelea kujitokeza katika baadhi ya maeneo nchini, ambapo hadi kufikia tarehe 11 Februari, 2025 kituo cha hali ya hewa cha Mlingano (Tanga) kiliripoti kiwango cha juu zaidi cha nyuzi joto 36.0°C mnamo tarehe 05 Februari ikiwa ni ongezeko la nyuzi joto 2.1°C ukilinganisha na wastani wa muda mrefu kwa mwezi Februari. Kituo cha hali ya hewa kilichopo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es salaam kiliripoti kiwango cha juu cha nyuzi joto 35.0°C mnamo tarehe 10 Februari, 2025 (ongezeko la nyuzi joto 2.2°C). Kituo cha Tanga kiliripoti nyuzi joto 35.1°C mnamo tarehe 10 Februari (ongezeko la nyuzi joto 2.3°C), Kibaha nyuzi joto 35.8 °C mnamo tarehe 10 Februari (ongezeko la nyuzi joto 3.0°C), na Kilimanjaro nyuzi joto 34.3°C mnamo tarehe 09 Februari, 2025 (ongezeko la nyuzi joto 0.6°C).

Aidha, ongezeko la unyevu angani (Relative humidity) katika kipindi hiki linalosababishwa na mvuke wa bahari hususan katika maeneo ya ukanda wa pwani na maeneo jirani limechangia pia mwili kuhisi joto zaidi ya viwango vinavyoripotiwa.

Vipindi vya ongezeko la joto vinatarajiwa kuendelea kujitokeza katika mwezi huu wa Februari, 2025 hususan katika maeneo ambayo msimu wa mvua za Vuli umeisha.

Hali ya joto kali inatarajiwa kupungua katika maeneo hayo mwezi Machi, 2025 hususan wakati ambapo mvua za msimu wa Masika zitakapoanza.

Kwa taarifa hii wananchi wanashauriwa kuendelea kuzingatia taarifa na tahadhari za hali mbaya ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania sambamba na kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazotokana na hali mbaya ya hewa.

Friday, February 7, 2025

Dkt.Chang'a atoa elimu ya Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi kwa wataalamu kutoka NGO



Dar es Salaam, 6 Februari 2025

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa  Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu wa Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC) Tarehe 6 Februari 2025 alipata fursa ya kuwahamasisha na kuwajengea uwezo zaidi kuhusu sayansi ya mabadiliko ya hali ya hewa na athari zake na namna ya kukabiliana nayo kwa wataalamu wa baadhi ya taasisi zisizo za kiserikali waliokuwa wanashiriki mafunzo ya siku moja yanayohusiana utekelezaji wa miradi ya kijamii kwa kuzingatia athari za mabadiliko ya tabia nchi "Partner's Capacity Building on Climate Action Integration into Development Programming".

Mafunzo hayo yamefadhiliwa na Ubalozi wa Ireland nchini. Taasisi zilizohudhuria mafunzo haya ni pamoja na Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation, AMREF International, UZIKWASA na Pangani fm.

Pamoja na kuelezea shughuli na taratibu za IPCC, Dkt.Chang'a amewahamasisha washiriki wa mafunzo kushiriki kwa wingi katika maandalizi ya ripoti za IPCC katika mzunguko wa saba ulioanza Julai 2023 na utakamilika kati ya 2029 au 2030 kwa kufanya tafiti na kutoa maoni kwenye ripoti mbalimbali za IPCC, "ushiriki wako unaweza kuwa walao kuweka maoni kwenye eneo moja la ripoti za IPCC na ukawa kwenye kumbukumbu miongoni wa wataalamu waliofanikisha ripoti hizi", alisema Dkt. Chang'a.

Wednesday, February 5, 2025

TMA NA EMEDO WAONGEZA NGUVU USAMBAZAJI WA TAAARIFA ZA HALI YA HEWA ZIWA VICTORIA


 




Tarehe: 04 Februari, 2025; Dodoma.

Katika kuendelea kuboresha usambazaji wa taarifa za hali ya hewa kwa jamii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetembelewa na Wataalamu wa Shirika lisilo la Kiserikali la Uhifadhi wa Mazingira na Maendeleo ya Kiuchumi la EMEDO ambalo linalojihusisha na uhifadhi wa mazingira  katika maeneo yanayozunguka Ziwa Viktoria.Ziara ya EMEDO ilikuwa na lengo la kujadiliana namna ya kuendelea kushirikiana katika usambazaji wa taarifa za hali ya hewa ili kuwafikia wananchi wengi zaidi wa maeneo yanayozunguka Ziwa Viktoria hususani wavuvi. Kikao kati ya TMA na EMEDO kimefanyika  Februari 4,2025 kwenye Ofisi za TMA Makao Makuu,Jijini Dodoma.

Wakati wa ziara hiyo yamefanyika majaribio ya matumizi ya kifaa maalumu cha usambazaji wa taarifa za hali ya hali ya hewa “Electronic Weather Board”, ambacho kitawasaidia wavuvi na watumiaji wa Ziwa Victoria kwenye kisiwa cha Goziba kuona utabiri wa hali ya hewa unaotarajiwa katika Ziwa kwa lengo la kufanya maamuzi sahihi ili kuokoa maisha na mali.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt.Ladislaus Chang'a aliushukuru uongozi  wa Shirika la EMEDO kwa ushirikiano unaoendelea kati ya Taasisi hizi wenye lengo la kusambaza taarifa na elimu ya matumizi sahihi ya taarifa zitolewazo na TMA katika maeneo ya ziwa Victoria.

"Haya ni mambo muhimu sana tunapaswa kufanya ili kuoanisha shughuli zetu na maono ya kimkakati na kuleta thamani kwa kile tunachofanya. Nimevutiwa sana na ushirikiano huu kwa sababu tunataka kila mmoja wetu kuchangia katika kufikia maono ya Taifa. Kwa mfano, kuimarisha hatua za kijamii kuhusu mabadiliko ya tabianchi na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa Duniani ".Alisema Dkt.Ladislaus Chang'a 

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa EMEDO, Bi. Editrudith Lukanga, alishukuru pia Mamlaka kwa ushirikiano huu  na kusema kuwa TMA imekuwa ikitoa wataalamu wake katika kutoa mafunzo kwa jamii na pia kutoa utabiri wa hali ya hewa, jambo ambalo limekuwa na manufaa kwa  jamii.

Kwa upande wake Meneja Mradi wa EMEDO,Bw.Arthur Mugema alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Taasisi hizi ndio umeleta matokeo ya kuandaa na kuweka kifaa cha  kielektroniki (Electronic Weather Board) kwenye kisiwa cha Goziba ambacho kinaenda kuboresha upatikanaji wa taarifa za hali ya  hewa.

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...