
Dodoma, Tarehe 21/01/2025, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa
(Mb) amezindua rasmi awamu
ya utekelezaji wa mradi wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuimarisha Uangazi wa
Hali ya Hewa (SOFF) kupitia hafla
iliyofanyika mjini Dodoma.
Mpango huu mkubwa
unaofanywa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kushirikiana na
Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Taasisi ya Hali ya Hewa ya
Denmark (DMI), unalenga kuimarisha uwezo wa Tanzania wa kufanya uangazi wa hali
ya hewa, ubadilishanaji wa data za hali ya hewa na katika kukabiliana na
changamoto zinazotokana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Katika
hotuba yake, Waziri Mkuu alisema “uzinduzi wa awamu ya utekelezaji wa mradi wa Mfuko
wa Umoja wa Mataifa wa Kuimarisha Uangalizi wa Hali ya Hewa (SOFF) ni hatua muhimu
kwa Tanzania na jumuiya za kimataifa.” Aliendelea kusema, “Utaongeza uwezo wa
Tanzania katika kukusanya na kusambaza data za hali ya hewa, mpango huu
utasaidia kujiandaa katika kukabiliana na maafa yatokanayo na mabadiliko ya
hali ya hewa, na kuzisaidia sekta muhimu kama vile kilimo, nishati na
usafirishaji katika kufanya maamuzi sahihi. Aliongeza kuwa mradi wa SOFF
unaendana na mikakati ya Serikali ya kuleta maendeleo kwa ustawi na uendelevu
wa Taifa.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile (MB), alisisitiza kuwa "SOFF sio tu inawekeza katika teknolojia
ya kisasa bali ni kichocheo cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi sababu data sahihi za hali ya hewa
huokoa na kulinda maisha na kuleta maendeleo endelevu." Naibu Waziri ameeleza kuwa Wizara ya
Uchukuzi ambayo inasimamia sekta ya hali ya hewa nchini Tanzania inatambua kuwa mafanikio ya
mpango wa SOFF yanategemewa kuwa endelevu na kuleta manufaa ya muda mrefu.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Mwakilishi wa Kudumu wa
Shirika la Hali ya Duniani (WMO) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko
ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dk.Ladislaus Chang'a alisisitiza namna mradi wa SOFF unavyosaidia
katika kukabiliana na mapungufu yaliyobainika katika miundombinu ya hali ya hewa nchini Tanzania ili
kukidhi viwango vya Kimataifa vya Mtandao wa Kimataifa wa Uangazi wa Msingi (GBON). Utafiti wa
mapungufu hayo ulifanyika mwaka 2023, "ulionyesha kuwa Tanzania inahitaji angalau vituo 27 vya
uangazi usawa wa ardhi kwa eneo la kilomita 200 kwa kilomita 200, na vituo vitano (5) vya uangazi
angani kwa eneo la kilomita 500 kwa kilomita 500."
Naye Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Shigeki Komatsubara, aliipongeza Serikali kwa hatua inayochukua
katika kufanya mipango ya kukabiliana na maafa, akisema kuwa “SOFF itakuwa ni nyenzo muhimu ya
kuwezesha mifumo ya utoaji wa tahadhali za mapema, kusaidia kufanya mifumo hii kuwa ya uhalisia
kwa jamii zilizo hatarini ulimwengu.” Alisema hayo akienda sawa na mpango wa Katibu Mkuu wa Umoja
wa Mataifa wa Tahadhali za Mapema kwa Wote, unaolenga kuhakikisha, ifikapo mwaka 2027, kila mtu
Duniani analindwa na mifumo madhubuti ya tahadhari za mapema.
Jumla ya bajeti iliyotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa awamu ya uwekezaji wa mradi wa SOFF nchini
Tanzania ni dola milioni 13.9, ambapo dola milioni 9 zinatolewa na Mfuko wa Mashirika ya Wadau wa
Hisani (Multi-Partner Trust Fund (MPTF)) huku sehemu iliyobaki ikifadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Mradi wa SOFF ni hatua kubwa katika kuboresha miundombinu ya data za
hali ya hewa kitaifa na kimataifa, kuwezesha maamuzi sahihi ya kusaidia ustahimilivu wa kiuchumi na
kimazingira. Kama sehemu ya mradi huo, Tanzania itanufaika kwa kuimarisha mifumo ya uangazi,
teknolojia ya kisasa, pamoja na ushirikiano wa kimataifa.