10 Septemba 2024, Arusha:
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa elimu kwa wadau mbalilmbali wa Ununuzi kuhusu matumizi sahihi ya huduma za hali ya hewa pamoja na kuchangia gharama za upatikanaji wa huduma hizo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi nchini.
Hayo yalizungumzwa na Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Hamza Kabelwa katika mada aliyoiwasilisha katika Jukwaa la 16 la Ununuzi la Afrika Mashiriki katika Ukumbi wa AICC, Arusha, linalofanyika tarehe 09 hadi 12 Sepetemba, 2024.
Dkt. Kabelwa alieleza kuwa, kiasi kikubwa cha matumizi ya fedha kinahusisha ununuzi, ni vyema huduma za hali ya hewa zikapewa kipaumbele katika utekelezaji wa Mipango ya Ununuzi na miradi mbalimbali ya maendeleo nchini ili kuongeza thamani ya fedha katika mradi. “Kwa kipindi cha hivi karibuni tumeshuhudia miradi mingi ikisimama kutokana na madhara yatokanayo na hali mbaya ya hewa, ni muda muafaka sasa wadau wanaohusika kuhakikisha wanatumia huduma hizo wakati wa ubunifu na kabla ya kuanza utekelezaji wa miradi yao”. Alisisitiza Dkt. Kabelwa.
Aidha, washiriki walijulishwa kwamba, huduma hizo mahsusi zinahitaji kuchangiwa gharama kidogo ambazo ziliwasilishwa rasmi katika hotuba ya Waziri wa Fedha ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2024/25, kifungu cha 158 ilikieleza mapendekezo ya mabadiliko ya kufanya marekebisho ya Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, sura 157 kuhusu Ada za Hali ya hewa kwa usalama wa uendeshaji wa Miradi ya Ujenzi. Lengo likiwa ni kuongeza tija na ufanisi wa utendaji kazi na kuimarisha usalama wa watu na mali.
Katika hatua nyingine, wataalaam kutoka TMA kupitia maonesho yanayoendelea katika viwanja vya AICC, walieleza pia huduma za hali ya hewa zinahitaji uwekezaji wa miundombinu ya kisasa na gharama kubwa za uendeshaji ili kuwezesha utoaji wa huduma bora, hivyo ni vyema kwa wadau mbalimbali kujitokeza kutumia huduma hizo sambamba na kuchangia gharama kidogo ya huduma mahsusi.