Wednesday, December 18, 2024

TMA YAWAHAKIKISHIA HUDUMA BORA ZA HALI YA HEWA WADAU WA USAFIRI WA ANGA














 

18 Desemba, 2024, Dar es Salaam:

 

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imekutana na wadau wa usafiri wa anga wanaotumia huduma za hali ya hewa nchini na kuwahakikishia upatikanaji wa huduma bora za hali ya hewa katika sekta hiyo ya usafiri wa anga. 

Aidha katika mkutano huo wadau walijadiliana namna bora ya kuendelea kuboresha huduma hizo zinazotolewa na Mamlaka. Mkutano huo ulifanyika katika Ukumbi wa Mikutano uliopo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kufunguliwa rasmi na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TMA ambaye pia Mkurugenzi anayesimamia Ubora wa huduma za hali ya hewa Dkt. Geofrid Chikojo, tarehe 18 Desemba 2024.

 

“Huduma za hali ya hewa nchini hususan zinazotolewa kwenye shughuli za usafiri wa anga zimekidhi vigezo vya kimaitaifa, yaani zimethibitishwa na viwango vya ubora vya kimataifa (ISO certified). Kila mwaka Mamlaka imekuwa ikikaguliwa na wakaguzi kutoka nje ya nchi na hata Taasisi zenye dhamana hiyo nchi na matokeo yake yamendelea kubainisha ubora wa huduma zetu”. Alisema Dkt. Chikojo

 

Awali, Dkt. Chikojo alieza lengo la mkutano huo ni kujadiliana ana kwa ana, kupokea maoni ya wadau hao pamoja na kufafanua uboreshaji wa huduma zitolewazo na Mamlaka kutokana na uwekezaji mkubwa unaendelea kufanywa na Serikali kwenye miundombinu na wataalamu kwa ujumla.

 

”Kwa kipindi cha miaka hii mitatu Mamaka imefanikiwa kufunga rada mbili za hali ya hewa, hivyo kuongeza idadi ya mtandao wa rada nchini na kufikia 5 katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mtwara, Mbeya na Kigoma. Aidha, Mamlaka imefunga mitambo maalum katika viwanja zaidi ya 10 nchini, mitambo ambayo inasaidia kutoa taarifa muhimu za hali ya hewa kwa ajili ya kusaidia usafiri wa ndege wakati wa kutua na kuruka”. Alizungumza Dkt. Chikojo.

 

Naye Rubani Busee S. Busee, mdau kutoka Ndege za Serikali, aliipongeza TMA kwa kuendelea kuboresha huduma zake kwa kuwezesha usalama wa utendaji kazi wao. Aidha aliiomba Mamlaka kuhakikisha huduma zinaenda sambamba na teknolojia ya kisasa.







Sunday, December 15, 2024

MWENENDO WA KIMBUNGA “CHIDO”

 


Dar es Salaam, 15 Disemba, 2024:

Taarifa hii inahitimisha mfululizo wa taarifa za mwenendo wa Kimbunga “CHIDO” zilizokuwa zikitolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) tangu tarehe 12 Disemba 2024. Mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa unaonesha kuwa katika kipindi cha saa 6 zilizopita, Kimbunga “CHIDO” kimeingia nchi kavu katika eneo la kaskazini mwa Msumbiji na kimeanza kupoteza nguvu yake huku kikielekea kusini magharibi mbali zaidi ya nchi yetu.

Aidha, kutokana na ukaribu wa njia yake na maeneo ya hapa nchini, wakati Kimbunga ”CHIDO” kikiingia nchi kavu huko kaskazini mwa Msumbiji mnamo asubuhi ya leo tarehe 15 Disemba, 2024 kimeweza kusababisha vipindi vya mvua kwa mkoa wa Mtwara na maeneo jirani.

Hivyo, kwa sasa hakuna tena tishio la kimbunga “CHIDO” katika nchi yetu na hakuna madhara zaidi ya moja kwa moja yanayotarajiwa yakihusishwa na kimbunga hicho. Hata hivyo ikumbukwe kuwa, kwakuwa tupo ndani ya msimu wa mvua katika maeneo mengi hapa nchini, matukio ya mvua za kawaida za msimu yanatarajiwa kuendelea katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

USHAURI: Watumiaji wa taarifa za hali ya hewa na wananchi kwa ujumla wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam wa kisekta.

Saturday, December 14, 2024

MWENENDO WA KIMBUNGA “CHIDO” KATIKA BAHARI YA HINDI



Dar es Salaam, 14 Disemba, 2024:

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kutoa taarifa kuhusu mwenendo wa Kimbunga “CHIDO” katika Bahari ya Hindi.

Katika kipindi cha saa 24 zilizopita, Kimbunga “CHIDO kimeendelea kusalia katika eneo la Bahari kati ya Visiwa vya Comoro na kaskazini mwa Kisiwa cha Madagascar huku kikiendelea kuashiria kuelekea katika maeneo ya kaskazini mwa Msumbiji kikiwa katika kiwango cha Kimbunga Kikali (Intense Tropical cyclone) chenye kasi ya upepo unaofika kilomita 200 kwa saa. Kimbunga “CHIDO” kinatarajiwa kupita maeneo ya Visiwa vya Comoro siku ya leo na kuingia nchi kavu kaskazini mwa Msumbiji mnamo asubuhi ya kesho tarehe 15 Disemba 2024 kabla ya kuanza kupungua nguvu yake kuelekea tarehe 16 Disemba, 2024.

Kwa hapa nchini, kimbunga hicho bado hakiashirii uwezekano wa kusababisha athari za moja kwa moja. Hata hivyo, kutokana na ukaribu wa maeneo ambayo Kimbunga “CHIDO” kinatarajiwa kufika (kaskazini mwa Msumbiji) na maeneo ya kusini mwa nchi yetu, upo uwezekano mdogo wa matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa katika maeneo ya Mikoa ya Mtwara na Ruvuma na maeneo jirani hususan kwa siku ya kesho tarehe 15 Disemba 2024.

Vilevile, upo uwezekano wa kutokea matukio ya upepo mkali wa bahari unaofika kilomita 40 kwa saa na mawimbi makubwa yanayofika mita 2 katika maeneo ya mwambao wote wa pwani ya nchi yetu kwa siku ya kesho tarehe 15 Disemba, 2024.

USHAURI: Watumiaji wa bahari na wananchi kwa ujumla wanashauriwa kuendelea kufuatalia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam wa kisekta.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga “CHIDO” na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila inapobidi.

Friday, December 13, 2024

MWENENDO WA KIMBUNGA “CHIDO” KATIKA BAHARI YA HINDI


 

​Dar es Salaam, 13 Disemba, 2024: 

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kutoa taarifa kuhusu mwenendo wa kimbunga “CHIDO” katika Bahari ya Hindi. 

Kati ya siku ya jana Alhamisi tarehe 12 na leo Ijumaa tarehe 13 Disemba, 2024, Kimbunga “CHIDO” kimeendelea kusalia katika eneo la bahari kaskazini mwa kisiwa cha Madagascar huku kikiendelea kuashiria kuelekea katika maeneo ya kaskazini mwa Msumbiji katika kipindi cha siku tatu zijazo (tarehe 14 hadi 16 ya mwezi Disemba, 2024). 

Aidha, kimbunga hicho bado hakiashirii uwezekano wa kusababisha athari za moja kwa moja hapa nchini. Hata hivyo, kutokana na ukaribu wa maeneo ambayo kimbunga “CHIDO” kinatarajiwa kupita (kaskazini mwa Msumbiji) na maeneo ya kusini mwa nchi yetu, upo uwezekano mdogo wa matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa katika maeneo ya mkoa wa Mtwara na maeneo jirani hususan kwa siku ya tarehe 15 Disemba 2024. 

Vilevile, upo uwezekano wa kutokea matukio ya upepo mkali wa bahari unaofika kilomita 40 kwa saa na mawimbi makubwa yanayofika mita 2 katika maeneo ya mwambao wote wa pwani ya nchi yetu hasa kwa siku ya tarehe 15 Disemba, 2024. 

USHAURI: Watumiaji wa bahari na wananchi kwa ujumla wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam wa kisekta. 

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga “CHIDO” na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila inapobidi.

Thursday, December 12, 2024

UWEPO WA KIMBUNGA “CHIDO” KATIKA BAHARI YA HINDI KASKAZINI MWA MADAGASCAR


 

Dar es Salaam, 12 Disemba, 2024:

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatoa taarifa ya uwepo wa kimbunga “CHIDO” katika Bahari ya Hindi kaskazini mwa kisiwa cha Madagascar.

Mifumo ya hali ya hewa inaonesha kuwa kimbunga hicho kinatarajiwa kuelekea maeneo ya kaskazini mwa Msumbiji katika kipindi cha siku nne zijazo (tarehe 13 hadi 16 ya mwezi Disemba, 2024).

Aidha, kwa sasa, kimbunga hicho hakiashirii uwezekano wa kusababisha athari za moja kwa moja hapa nchini. Hata hivyo, kutokana na ukaribu wa maeneo ambayo kimbunga “CHIDO” kinatarajiwa kupita (kaskazini mwa Msumbiji) na maeneo ya kusini mwa nchi yetu, upo uwezekano mdogo wa matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa itakayoambatana na upepo mkali na mawimbi makubwa ya bahari kwa maeneo ya Mtwara na maeneo jirani hususan kati ya tarehe 14 na 16 ya Disemba 2024.

USHAURI: Watumiaji wa bahari na wananchi kwa ujumla wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam wa kisekta.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga hicho na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila inapobidi.

Friday, November 22, 2024

TMA YAELEZA ATHARI ZA MABADILIKO YA TABIANCHI KWENYE KILIMO CHA MWANI


Baku,Azerbaijan; Tarehe 22 Novemba, 2024; 

Kaimu Mkurugenzi wa TMA, Zanzibar, Masoud Faki ameeleza  namna kilimo cha mwani kinavyoweza kuathiriwa na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi. Alisema hayo wakati akiwasilisha mada katika Banda la Tanzania, lililopo kwenye Mkutano wa 29 wa Nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP29), unaofanyika Baku,Azerbaijan..

Alieleza kuwa kilimo cha mwani kinaathiriwa zaidi na mabadiliko ya hali ya hewa hususani mvua nyingi,joto kali na upepo mkali. Aidha, alifafanua, TMA inatoa huduma za utabiri ikiwemo Msimu na utabiri wa hali mbaya ya hewa wa siku tano ambao huwezesha wakulima kufanya maamuzi sahihi kama vile uchaguzi wa eneo linafaa ili kukabiliana na hali ya mvua nyingi ambayo husababisha upungufu wa kiwango cha chumvi na hivyo kusababisha magonjwa; maamuzi mengine ni uvunaji wa zao hilo ili kukabiliana na upepo mkali unaoweza kuleta madhara ya mwani kukatika na kupotelea baharini.

Thursday, October 31, 2024

UTABIRI WA MVUA ZA MSIMU NOVEMBA 2024 HADI APRILI 2025 WATOLEWA RASMI


Dar es Salaam, Tarehe 31 Oktoba, 2024

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi utabiri wa mvua za msimu kwa maeneo yanayopata mvua mara moja kwa mwaka. Maeneo hayo ni mikoa ya Kigoma, Katavi, Singida, Dodoma, Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe, Lindi, Mtwara, Ruvuma na Kusini mwa Morogoro katika kipindi cha miezi ya Novemba, 2024 hadi Aprili, 2025.

Akitoa utabiri huo kwa vyombo vya habari katika ukumbi wa Ubungo Plaza, Kaimu Mkurugenzi Mkuu, TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a alisema mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa katika maeneo ya mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Songwe, Singida na Dodoma; kaskazini na mashariki mwa mkoa wa Lindi, na kaskazini mwa mikoa ya Mbeya na Iringa. Aidha, mvua za Wastani hadi Juu ya wastani zinatarajiwa katika mikoa ya Njombe, Ruvuma, Mtwara, maeneo ya kusini na magharibi mwa mkoa wa Lindi, kusini mwa mikoa ya Mbeya, Iringa na Morogoro.

“Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Oktoba, 2024 katika mkoa wa Kigoma na kusambaa katika maeneo mengine yanayopata mvua za Msimu mwezi  Novemba, 2024 na mwisho katika mkoa wa Ruvuma Disemba, 2024. Kipindi cha nusu ya pili ya msimu (Februari – Aprili, 2025) kinatarajiwa kuwa na mvua nyingi ikilinganishwa na nusu ya kwanza (Novemba, 2024 – Januari, 2025)”. Alifafanua Dkt. Chang’a.

“Vipindi vifupi vya mvua kubwa vinatarajiwa kujitokeza hata katika meneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani”.Aliongeza Dkt. Chang’a

Aidha, Dkt. Chang’a alisema, Mamlaka imeendelea kuandaa utabiri wa maeneo madogo madogo, ambapo kwa msimu huu jumla ya wilaya  zote 63 zimeandliwa utabiri wake. Lengo la Mamlaka ni kuendelea kuboresha huduma zake kwa wadau ili kuchochea na kuimarisha mchango na matumizi ya taarifa za hali ya hewa katika kuongeza tija na  ufanisi kwenye shughuli za  kiuchumi na kijamii

Akieleza athari zinazoweza kujitokeza, Dkt. Chang’a alisema vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi pamoja na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao na miundombinu ya kilimo, hususan katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani, kina cha maji katika mito na mabwawa kinatarajiwa kuongezeka, hali inayoweza kusababisha mafuriko, hasa katika maeneo yanayoathiriwa na mafuriko.

Wednesday, October 30, 2024

NAIBU KATIBU MKUU UCHUKUZI ATEMBELEA OFISI ZA TMA.

 






Dar es Salaam, tarehe 30 Oktoba 2024.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi Ndg. Ludovick Nduhiye amefanya ziara ya kutembelea ofisi za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) zilizopo katika jengo la Ubungo Plaza, Dar es Salaam ikiwa ni moja ya malengo yake ya kuzitambua Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Uchukuzi, kufahamu majukumu ya kiutendaji na kuelewa changamoto zinazowakabili na Mikakati ya kuimarisha Taasisi na utoaji wa huduma.

Baada ya taarifa ya utendaji kutoka TMA, Naibu Katibu Mkuu, Uchukuzi aliipongeza TMA kwa kuendelea kuimarisha na kuboresha huduma za haki ya hewa nchini, ikiwemo kuongeza usahihi wa utabiri, akieleza kuwa yeye ni mmoja wa wadau wa Mamlaka na anafuatilia, kuzingatia na kutumia taarifa za hali ya hewa.

'Kiuekweli taarifa zenu ni nzuri, niwapongeze sana TMA, mimi ni mdau wa taarifa zenu na nimekuwa nikizifuatilia, kuzizingatia na pia kuzitumia, naweza kusema TMA ya sasa si kama ile za zamani." Alisisitiza Ndg. Nduhiye.

Aidha, akiwasilisha awali salamu za ukaribisho Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang'a alieleza Maono na Mikakati ya kuimarisha huduma na kuongeza ushawishi wa TMA na Tanzania katika masuala ya hali ya hewa kikanda na kimataifa. Aidha alisisitiza azma ya kuifanya Tanzania kuwa HUB ya mafunzo ya Rada za hali ya hewa katika Afrika. 

Katika hatua nyingine, Kaimu Mkurugenzi wa TMA, Ofisi za Zanzibar Ndg. Masoud Faki alihitimisha kwa kutoa salamu za shukrani kwa ndg. Nduhiye, kwa kuitembelea TMA ndani ya muda mfupi tokea ateuliwe kama Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi na kuahidi kufanyia kazi maelekezo yake.

Monday, October 28, 2024

WAANDISHI BORA WA HABARI ZA HALI YA HEWA WATUNIKIWA TUZO.

 













   
                   
                                                                                          
                                                                                                                                                                                                                     
                                                                       

                                                                                                                                                                    Dar es Salaam, Tarehe 28 Oktoba 2024;

Mwenyekiti wa Bodi Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Mhe. Jaji Mshibe Ali Bakari amewatunukia rasmi tuzo waandishi wa habari waliofanya vizuri kwa kipindi cha kuanzia mwezi Julai 2023 hadi Juni 2024 katika kuandika habari za hali ya hewa nchini. Hafla hiyo fupi ilifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Dar es Salaam, tarehe 28 Oktoba 2024.

Kabla ya kukadidhi tuzo hizo kwa washindi, Mhe. Mshibe ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi wa hafla hiyo aliipongeza TMA kwa kuendelea kuwashirikisha na kutoa motisha kwa wanahabari katika utoaji elimu na usambazaji wa huduma za hali ya hewa nchini.

Alieleza kuwa, TMA ni moja ya taasis chache nchini, zinazothamini mchango wa wanahabari kwa ujumla ikiwemo ubunifu wa kuanzisha TUZO ya wanahabari bora wa habari za hali ya hewa nchini kwa miaka mitano sasa, ambapo kwa mwaka huu nimeelezwa kuwa TMA imeongeza wigo wa washindi.

“Katika kuhakikisha tuzo hizi zinaendelea kuwa bora zaidi, mwaka huu Mamlaka imeboresha maeneo kadhaa ikiwemo kuongeza vipengele viwili vya waandishi kutoka nje ya Dar es Salaam na Zanzibar pamoja na kuboresha zawadi za washindi, hongereni sana TMA”. Alisistiza Mhe. Mshibe.

Lengo kuu la Tuzo hizi ni kuendelea kuleta hamasa na kujenga umahili katika uandaaji na usambazaji wa tarifa za hali ya hewa kwa jamii, na kuimarisha mchango wa wanahabari katika kuelimisha jamii kuhusu umuhimu na matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa”. Alieleza Dkt.Mshibe

Akimkaribisha mgeni rasmi kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu, TMA, Dkt. Hamza Kabelwa, Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri alisema Mamlaka kwa kutambua mchango huu mkubwa, imeendelea kuimarisha mahusiano haya kwa kuendelea kutoa motisha mbalimbali kwa wanahabari ikiwemo kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa takribani miaka 15 sasa hususani kipindi cha maandalizi ya utabiri wa mvua za misimu.

Mafunzo haya yamekuwa yakitolewa, vilevile, kutafuta fursa za ushiriki wa waandishi wa habari kwenye mafunzo au majukwaa ya kimataifa mfano; Mwaka jana waandishi wa habari 10 walipata mwaliko wa kushiriki mafunzo Nairobi, Kenya (wengi wao wapo katika kundi hili) na mwaka huu mmoja wao aliweza kushiriki katika Kongamano la kuaandaa utabiri wa msimu wa Vuli 2024 kwa nchi za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika nchini Kenya, na huko nyuma wapo walioshiriki katika makongamano hayo Adis Ababa, Ethiopia na Entebe, Uganda”. Aliendelea Dkt. Kabelwa.

Hafla hiyo ilifanyika wakati wa warsha ya wanahabari katika kujadili utabiri wa mvua za msimu kwa maeneo yanayopata mvua mara moja kwa mwaka (Novemba 2024 hadi Aprili 2025). Washindi wa tuzo hizo walikuwa; Mshindi wa TV na Redio ni John Mathias kutoka TBC 1, mshindi  wa Zanzibar ni Othman Ali Juma kutoka Alnoor FM,mshindi wa mikoani ni Adam Hando kutoka CG FM-Tabora, mshindi wa magazetini ni Superious Ernest kutoka gazeti la Uhuru na kwa mitandao ya kijamii ni Zaituni Mkwama kutoka Dailynews Digital TSN. TMA inatarajia kutoa rasmi utabiri wa mvua za Msimu siku ya Alhamis, tarehe 31 Oktoba 2024.                                          

Thursday, October 24, 2024

WADAU WA KISEKTA WATAKIWA KUKABILIANA NA ATHARI ZA MVUA ZA MSIMU 2024/25












 Dodoma; Tarehe 24 Oktoba, 2024

 

Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Mhe. Jaji Mshibe Ali Bakari amewataka wadau kutoka sekta mbalimbali kukabialiana na athari zitakazoweza kujitokeza pamoja na kuchukua hatua stahiki wakati wa mvua za msimu zinatotarijwa kuanza mwezi Novembea 2024 hadi Aprili 2025 kwa maeneo yanayopata mvua mara moja kwa mwaka hapa nchini. Alizungumza hayo wakati akifungua rasmi mkutano wa nane wa wadau wa utabiri wa mvua za Msimu uliofanyika katika ukumbi wa PSSSF, Dodoma, Tarehe 24/10/2024.

Mvua za Msimu, Novemba 2023 hadi Aprili 2024 zilitawaliwa na uwepo wa hali ya El NiƱo. Hali hii ilisababisha uwepo wa matukio ya mvua kubwa katika maeneo mengi nchini. Hivyo napenda kutoa msisitizo kuwa, katika majadiliano ya mvua za Msimu ya mwaka huu, Novemba 2024 hadi Aprili 2025, tujikite katika kujadili athari zinazoweza kujitokeza na kutoa ushauri stahiki”. Alisema Mh.Jaji Mshibe.

 

Jaji Mshibe aliongeza kuwa, Bodi itaendelea kuisimamia vizuri TMA katika utekelezaji wa mipango yake na kuiwezesha kutimiza ipasavyo Dira na mpango mkakati wake ili kuendelea kusaidia maendeleo ya nchi na Dunia kwa ujumla wake. Aidha, aliipongeza TMA kwa kuendelea kutoa utabiri wenye viwango vya juu vya usahihi unaokubalika kitaifa na kinmataifa.

 

Awali, Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu ambaye pia ni Mkurugenzi wa Udhibiti na Usimamizi wa Ubora TMA, Dkt. Geofrid Chikojo alisema Mamlaka imeendelea kuboresha taarifa za hali ya hewa kwa kutoa utabiri mahususi kwa sekta mbalimbali, katika kuboresha taarifa hizo kwa wadau, TMA imeendelea kutoa taarifa za utabiri wa maeneo madogo kwa wilaya zote za mikoa iliyopo katika ukanda unaopata mvua za Msimu.

“Utabiri wa Wilaya 63 umeandaliwa kwa maeneo husika, hivyo ni vyema kila wilaya na kila sekta ikatumia taarifa hizo katika kufanya maamuzi na kuweka mipango ili kuboresha huduma zao kwa lengo la kuongeza tija na pia kupunguza madhara ya hali mbaya ya hewa yanapojitokeza”. Alifafanua Dkt. Chikojo.

Naye mwakilishi wa wadau kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Cosmas Makomba alieleza namna taarifa za awali za mvua za msimu 2023/24 zilivyosaidia katika kuchukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kuandaa mkakati wa maafa, kutoa mafunzo pamoja na kuandaa mpango wa dharura kwa mikoa iliyotarajiwa kuathirika.

Mkutano huu ni muendelezo wa sehemu ya ushirikishwaji wadau wakati wa maandalizi ya utabiri wa msimu husika ambapo wataalamu kutoka sekta mbalimbali, wanapatiwa fursa za kuona rasimu ya utabiri husika na kutoa michango yao juu ya athari zinazotarajiwa katika sekta husika pamoja na ushauri ili kuwezesha kuandaa mbinu na mipango ya kukabiliana na athari hizo. Aidha, TMA hutumia fursa hiyo kupokea mrejesho wa namna bora ya kuendelea kuboresha huduma za hali ya hewa nchini.  

Mamlaka inatarajia kutoa rasmi utabiri wa mvua za msimu kwa kipindi cha mwezi Novemba 2024 hadi Aprili 2025 kwa maeneo ya Dodoma, Singida, Tabora, Mtwara, Lindi, Ruvuma, Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Rukwa, Morogoro Kusini na Kigoma tarehe 29 Oktoba 2024. Kauli mbiu ya msimu huu ni ‘Matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa kwa wote na kwa wakati’.

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...