Saturday, November 25, 2023

DKT. CHANG’A APEWA JUKUMU LA KUSIMAMIA BODI YA SAYANSI KATIKA JOPO LA KIMATAIFA LA SAYANSI YA MABADILIKO YA HALI YA HEWA NA TABIANCHI (IPCC)

 




Geneva, Uswisi: Tarehe 22/11/2023

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi “Intergovernmental Panel on Climate Change (IPCC)”, Dkt. Ladislaus Chang’a, amepewa jukumu la kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Sayansi katika Jopo la IPCC. 

Dkt. Chang’a alipewa jukumu hilo katika mkutano wa 66 wa viongozi wa Jopo la IPCC (Sixty-sixth IPCC Bureau) uliofanyika Geneva, Uswiss tarehe 15 na 16 Novemba, 2023. Lengo kuu la mkutano huo lilikuwa ni kujadili maandalizi ya utekelezaji wa shughuli za IPCC katika Tathmini ya Saba ya IPCC ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC Seventh Assessment Cycle - AR7). Mkutano huo ni wa kwanza tangu uongozi mpya wa IPCC uchaguliwe katika uchaguzi uliofanyika mwezi Julai 2023. Uongozi wa IPCC una jumla ya viongozi thelathini na nne (34), Dkt. Chang’a ni miongoni mwa viongozi hao ambapo alichaguliwa katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti akiwa miongoni mwa Makamu Wenyeviti watatu wa IPCC.

Bodi ya Sayansi ya IPCC atakayoisimamia Dkt. Chang’a inaundwa na Makamu Wenyeviti wote watatu wa IPCC ambao ni Dkt. Ladislaus Chang’a (Tanzania), Prof. Ramón Pichs-Madruga (Cuba), na Prof. Diana Ürge-Vorsatz (Hungary). Miongoni mwa shughuli zitakazoambatana na jukumu hilo jipya alilopewa Dkt. Chang’a ni: kusimamia programu ya IPCC ya ufadhili wa mafunzo (IPCC Scholarship Programme); kuratibu ushiriki wa wanasayansi chipukizi (Young Scientists) katika masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi; na kuwakilisha jopo la IPCC katika programu ya WMO ya utafiti “(World Weather Research Programme (WWRP) ”. 

Jukumu jipya alilopewa Dkt. Chang’a la kusimamia Bodi ya Sayansi ya Jopo la IPCC pamoja na fursa za mpya za mashirikiano na WMO ni mwendelezo wa kuaminika kwa TMA na Tanzania kimataifa. Hii inatokana na mchango mzuri unaotolewa na wataalamu wa TMA katika nafasi mbalimbali wanazohudumu, ikiwa ni pamoja na vikosikazi vya WMO. Mafanikio haya yanaendelea kuitangaza Tanzania kimataifa na kuimarisha zaidi mahusiano mazuri ya kidiplomasia kati ya Tanzania na nyingine katika utoaji wa huduma za hali ya hewa.

Katika hatua nyingine, Dkt. Chang’a alishiriki katika mkutano wa kuwajengea uwezo Wawakilishi wapya wa Kudumu wa Nchi katika WMO (Permanent Representatives of Members with WMO) uliofanyika Geneva, Uswis kuanzia tarehe 20 hadi 22 Novemba, 2023. Kupitia mkutano huo, alipata pia fursa ya kukutana na baadhi ya viongozi katika vitengo vya WMO ambapo walijadili maeneo mapya ya ushirikiano na TMA kupitia programu za WMO, ikiwa ni pamoja na WMO kutambua mifumo iliyobuniwa na wataalamu wa TMA ili itumike katika huduma za hali ya hewa. 

IPCC ni Chombo cha Umoja wa Mataifa kinachosimamiwa na WMO na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (United Nations Environmental Programme- UNEP). Chombo hicho kilianzishwa mwaka 1988 kwa jikumu la kusimamia sayansi ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi ambapo Jopo hilo hufanya tathmini za mwenendo wa Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi na kuandaa taarifa za tathmini (Climate Change Assessment Reports) ambazo zina mchango muhimu katika kufanya maamuzi ya kukabiliana na madhara yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi. Tangu kuanzishwa kwake, IPCC imeandaa taarifa sita za tathmini, ambapo tathmini ya sita (IPCC Sixth Assessment cycle) ilianza mwaka 2015 na kukamilika mwaka 2022. Uongozi mpya wa IPCC utasimamia Tathmini ya Saba ya IPCC ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi inayotarajiwa kuanza mapema mwaka 2024 na kukamilika mwaka 2030.

Thursday, November 23, 2023

WADAU WA MAZINGIRA WAPATA ELIMU YA HUDUMA MAHSUSI ZITOLEWAZO NA TMA

 




Matukio mbalimbali kwa picha kupitia jukwaa la mkutano mkuu wa tano wa mwaka wa Chama cha Wataalam wa Mazingira Tanzania (TEEA) pamoja na maonesho ya bidhaa na teknolojia za "Eco - Friendly" uliofanyika katika ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), tarehe 22 Novemba 2023.


Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...