Tuesday, October 31, 2023

TMA YATOA RASMI UTABIRI WA MVUA MAENEO YANAYOPATA MSIMU MMOJA KWA MWAKA.



Dar es Salaam; Tarehe 31 Oktoba, 2023;

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi mwelekeo wa mvua za Msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka ambayo ni mikoa ya  Tabora, Katavi, Kigoma, Singida, Dodoma, Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe, Lindi, Mtwara, Ruvuma na  na Kusini mwa Morogoro. Taarifa hiyo imesema  kipindi cha nusu ya msimu (Novemba 2023 hadi Januari, 2024) kinatarajiwa kuwa na mvua nyingi ukilinganisha na nusu ya pili (Februari hadi Aprili 2024), uwepo wa El-NiƱo unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika mvua za Msimu.

“Mvua za Juu ya Wastani hadi Wastani zinatarajiwa katika maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro, mikoa ya Iringa, Lindi, Mtwara, Singida, Dodoma, kaskazini mwa mkoa wa Katavi, Kigoma na Tabora. Aidha, mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani zinatarajiwa kusini mwa mkoa wa Katavi, mikoa ya Njombe, Rukwa, Songwe, Mbeya na Ruvuma”. Alisema Dkt. Ladislaus Chang’a, Kaimu Mkurugenzi Mkuu TMA na Makamu Mwenyekiti Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabia Nchi (IPCC) wakati wa mkutano na vyombo vya habari kuhusiana na mwelekeo wa mvua za Msimu, katika ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam,Tarehe 31 Oktoba, 2023. 

Dkt. Chang’a alibainisha athari zinazoweza kujitokeza ikiwa ni vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi pamoja na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao na miundombinu ya kilimo, vile vile, kina cha maji katika mito na mabwawa kinatarajiwa kuongezeka, aidha, Dkt. Chang’a alitoa ushauri kwa wadau mbalimbali kuzingatia matumizi endelevu ya uhifadhi wa rasimali maji.

Katika hatua nyingine, Dkt. Chang’a alifafanua kuwa Msimu wa Vuli kwa miezi ya Oktoba hadi Disemba, 2023 katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Dar es Salaam, kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, Pwani (ikijumuisha kisiwa cha Mafia) pamoja na Zanzibar (visiwa vya Unguja na Pemba) utabiri wake ulitolewa tarehe 24 Agosti, 2023. Mvua hizo zimeshaanza katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria, pwani ya kaskazini na baadhi ya maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki kama ilivyotabiriwa. Aidha, ongezeko la mvua linatarajiwa katika miezi ya Novemba na Disemba, 2023. Vilevile, mvua za nje ya msimu zinatarajiwa katika mwezi Januari na Februari, 2024.

Kwa taarifa zaidi tembelea: www.meteo.go.tz

Tuesday, October 3, 2023

UFAFANUZI WA TAARIFA YA TAHADHARI INAYOSAMBAA KUHUSU UWEPO WA PACIFIC EL NINO NA ATLANTIC EL NINO.


Dodoma; Tarehe 2 Oktoba, 2023;

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu taarifa ya tahadhari inayosambaa kuhusu uwepo wa Pacific Elnino na Atlantic El nino hatari sana na kuitaka jamii kununua jiki, water guard kwa ajili ya kuweka kwenye maji ya kunywa pamoja na masuala mengine yaliyoelezwa kwenye ujumbe huo, Aidha, ujumbe huo umekuwa ukisambaa kwenye mitandao ya kijamii na hivyo kuleta taharuki kwa wananchi.

Taarifa hiyo sio sahihi, taarifa sahihi ilitolewa tarehe 24 Agosti, 2023 kwa vyombo vya habari na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt. Ladislaus Chang’a na kutolewa maelekezo na viongozi mbalimbali wa nchi sambamba na kusambazwa kupitia vyanzo rasmi vya habari.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inaendelea kusisitiza umma kufuatilia na kuzingatia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na TMA pamoja na ushauri wa kisekta unaotolewa na Taasisi zenye Mamlaka kulingana na sheria na taratibu za nchi. Aidha, ikumbukwe kuwa ni kosa kwa mujibu wa sheria Na, 2 ya mwaka 2019 ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kwa mtu yeyote kutoa tahadhari ya hali mbaya ya hewa kinyume na taratibu na bila idhini ya Mamlaka. 

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...