Monday, May 15, 2023

TANZANIA YAPEWA KIPAUMBELE UBORESHAJI WA MIUNDO MBINU YA HALI YA HEWA

Mwakilishi Mkazi Tanzania, Mpango wa Umoja wa Mataifa Kusaidia Maendeleo Duniani (UNDP), Bi. Christiane Musisi, akizungumza wakati wa warsha maalumu ya kuangalia mapungufu ya miundo mbinu ya hali ya hewa, Ukumbi wa PSSSF, Dodoma, Tarehe 15/05/2023.


Mwakilishi kutoka Taasisi ya Hali ya Hewa Denmark (DMI), Bw. Christian Johansen akizungumza wakati wa warsha maalumu ya kuangalia mapungufu ya miundombinu ya hali ya hewa, Ukumbi wa PSSSF, Dodoma, Tarehe 15/05/2023.


Baadhi ya washiriki wa warsha maalumu ya kuangalia mapungufu ya miundombinu ya hali ya hewa nchini.






Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Ladislaus Chang’a akizungumza wakati wa warsha maalumu ya kuangalia mapungufu ya nchi katika miundo mbinu ya hali ya hewa, Ukumbi wa PSSSF, Dodoma, Tarehe 15/05/2023.




Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Hali ya Hewa ya Denmark, zimekutana na wadau katika warsha maalumu ya kuangalia mapungufu ya nchi katika miundo mbinu ya hali ya hewa ili kuweza kufanya maboresho ambayo yatasaidia kuleta tija katika utoaji huduma za hali ya hewa kwa maendeleo ya Taifa.

 

Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Ladislaus Chang’a alieleza kuwa Tanzania imepata fursa ya kuchaguliwa kuwa miongoni mwa nchi 26 duniani ambazo zimepewa kipaumbele katika kuimarisha huduma za hali ya hewa kupitia miundo mbinu ya uangazi wa hali ya hewa chini ya mwamvuli wa Mfuko wa Kuimarisha Uangazi wa hali ya hewa (Systematic Observations Financing facility-SOFF). Mfuko huu umekuwa ukichangiwa nan chi mbalimbali duniani, na wadau mbalimbali wa Maendeleo ikiwemo Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na Mpango wa Umoja wa Matatifa wa Kusaidia Maendeleo Duniani (UNDP).

 

Dkt. Chang’a alisema, ‘fursa hii ni muhimu kwa Tanzania hususani kipindi hiki ambacho dunia ikiwemo nchi yetu inakabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi, changamoto hizi zinahitaji msukumo wa kipekee katika kuimarisha miundombinu ya hali ya hewa lakini vilevile, utoaji wa huduma hususan huduma za utabiri na tahadhari za hali mbaya ya hewa ”. Alisema Dkt. Chang’a. 

 

“Hii ni mojawapo ya jitihada ambazo zinaenda kuchangia katika jitihada kubwa zinazofanywa na serikali yetu ya kuimarisha huduma za hali ya hewa  na kuongeza uwezo wetu wa kuhimili changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa. Tunaishukuru sana Serikali”. Aliongeza Dkt. Chang’a.

 

Kwa upande wake Bw. Christian Johansen, mwakilishi wa Taasisi ya Hali ya Hewa ya Denmark (DMI),alisema ushirikiano baina ya Tanzania na Denmark ni wa muda mrefu na unaendelea kukua. Ushirikiano wa sasa baina ya TMA, DMI na UNDP unalenga kuboresha huduma za hali ya hewa kwa kuimarisha miundombinu ya uangazi pamoja na kuendeleza  mahusiano mazuri yaliyoweka baina ya nchi hizi mbili. Alisema kupitia program ya SOFF waliweza kutembelea katika maeneo ya Singida, Dodoma, Shinyanga, Mwanza na Tabora, na kufanya tathmini ya uwezo na mahitaji katika kuimarisha uangazi, na kupitia warsha hii wanatarajia kupata taarifa zaidi za maeneo mengine ya nchi yanayohitaji maboresho na uimarishaji wa mfumo wa uangazi.

 

Naye mwakalishi Mkazi wa UNDP Tanzania, Bi. Christine Musisi alishukuru kwa mahusiano mazuri baina ya UNDP na TMA, ikiwemo misaada mbalimbali ambayo UNDP imekuwa ikitoa kusaidia uimarishwaji wa huduma za hali ya hewa. Alieleza kuwa takwimu zinaonesha ongezeko la matukio ya hali mbaya ya hewa ikiwemo matukio ya mafuriko, na hivyo programu hii itasaidia upatikanaji wa taarifa sahihi za hali ya hewa na za uhakika na hivyo kuchangia katika kuongeza kasi ya maendeleo katika sekta muhimu kama vile kilimo, mifugo, nishati, uchukuzi, afya na maji. Aidha, aliongeza kusema kuwa uboreshaji wa miundombinu ya hali ya hewa ni kwa manufaa ya nchi na dunia kwa ujumla.


 

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...