Friday, March 24, 2023

KAIMU MKURUGENZI MKUU WA TMA, DKT. LADISLAUS CHANG’A AONGOZA VIKAO VYA KAMATI YA JOPO LA KIMATAIFA LA SAYANSI YA MABADILIKO YA HALI YA HEWA NA TABIANCHI (INTERGOVERNMENTAL PANEL ON CLIMATE CHANGE) KUIDHINISHA TAARIFA YA SITA YA TATHMINI YA MABADILIKO YA HALI YA HEWA NA TABIANCHI.

Interlaken, Uswiss; Tarehe 17/03/2023. Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Ladislaus Chang’a, ambaye pia ni Afisa Kiungo wa Tanzania katika Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (Intergovernmental Panel on Climate Change - IPCC) ameongoza vikao vya kamati ya jopo hilo (Contact Group) katika mkutano wa 58 wa IPCC (Fifty-Eighth Session of the Intergovernmental Panel on Climate Change – IPCC 58) uliofanyika Interlaken, Uswiss kuanzia tarehe 13 hadi 18 Machi, 2023. Jopo la IPCC lilikutana kwa lengo kuu la kuidhinisha Taarifa ya Sita ya Tathmini ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi “IPCC Synthesis Report of the Sixth Assessment cycle (AR6) - Climate Change 2023". Utaratibu wa kuidhinisha taarifa za tathmini za IPCC huhusisha kamati ambazo huteuliwa kufanya mapitio ya maeneo maalumu katika rasimu ya taarifa na kutoa mapendekezo. Kwa upande wake, Dkt. Chang’a, aliteuliwa kuongoza kamati ya kuidhinisha “Sehemu A” ya taarifa hiyo (Section A and Figures, Summary for Policymakers of the Working Group III Contribution to the IPCC Sixth Assessment Report –SPM 1 and the associated Figure Caption) akishirikiana na Bi. Tina Christensen kutoka Denmark. Sambamba na kuongoza kamati hiyo, Dkt. Chang’a alitoa mchango wa kitaalamu wa sayansi ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi kwa Tanzania katika taarifa hiyo kwa manufaa ya nchi yetu. Dkt. Changa alifanikisha vizuri jukumu hilo na kuitangaza vyema Tanzania Kimataifa. Katika hatua nyingine, Dkt. Chang’a alikutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Taasisi ya Hali ya Hewa ya Korea (Korean Meteorological Adminstration – KMA) kuhusu ushirikiano na TMA katika masuala ya hali ya hewa ambapo kiongozi huyo alisema KMA iko tayari kupanua wigo wa ushirikiano na TMA. Miongoni mwa maeneo ambayo walikubaliana KMA na TMA kushirikiana ni matumizi ya mifumo ya kiditajitali katika uandaaji wa utabiri wa hali ya hewa,ufungashaji na usambazaji wa taarifa za hali ya hewa. Aidha, Dkt. Chang’a alikutana na kufanya mazungumzo na Bi. Shirley Matheson ambaye ni Mratibu wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi katika Shirika la Uhifadhi wa Mazingira (Worldwide Fund for Nature –WWF) ambapo walijadiliana kuhusu WWF kushirikiana na TMA katika masuala ya hali ya hewa na tabianchi. IPCC ni Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi liloanzishwa na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa (United Nations Environmental Programme – UNEP). Jopo hilo linaundwa na Nchi zote Wanachama wa WMO kupitia wataalamu ambao ni Maafisa Viungo (Focal Points) wanaowakilisha nchi zao katika Jopo hilo. Kwa Upande wa Tanzania, TMA imepewa dhamana ya kuiwakilisha Tanzania katika masuala hayo ambapo Afisa Kiungo wa Tanzania ni Dkt. Ladislaus Chang’a. Jukumu la Msingi la IPCC ni kutumia tafiti mbalimbali zinazohusu Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi na kuandaa taarifa za Tathmini (Synthesis Reports) ambazo ni muhimu katika kutoa maamuzi ya sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi. Tangu Jopo hilo lianzishwe mwaka 1988 limefanikiwa kutoa Taarifa tano (5) za tathmini ambapo taarifa ya 5 (The Fifth Synthesis Report (SYR) of the IPCC Assessment Report (AR5): Climate Change 2014) ilitolewa mwaka 2014. Mkutano wa 58 wa IPCC uliidhinisha Taarifa ya Sita ya Tathmini ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (The Sixth Synthesis Report (SYR) of the IPCC Assessment Report (AR6): Climate Change 2023).

KAMATI YA KUCHAKATA DATA ZA HALI YA HEWA DUNIANI YAKUTANA TANZANIA

Arusha, Tanzania; Tarehe 20/03/2023 Tanzania imekuwa mwenyeji wa mkutano wa Kamati ya Kuchakata Data za Hali ya Hewa Duniani, lengo ikiwa ni kuhakikisha data za hali ya hewa zinatumika ipasavyo na taasisi za hali ya hewa katika nchi wanachama wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na kwa manufaa ya sekta mbalimbali. Mkutano huo unaojumuisha wajumbe kutoka nchi kumi na mbili (12). Akizungumzia umuhimu wa mkutano huo kwa nchi, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo na Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Hamza Kabelwa, alisema “ kwanza ni kutangaza utalii wa nchi yetu ambapo wageni hawa watakuwa mabalozi wa vivutio vya Tanzania katika nchi zao, aidha, kutokana na changamoto kubwa za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, upatikanaji data sahihi za hali ya hewa ni muhmu kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania katika kusaidia kukabiliana na mabadiliko hayo ili kutoa taarifa sahihi za hali ya hewa kwa maendeleo endelevu”. Naye, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt. David Richardson, alisema Kamati anayoisimamia itajikita katika kusaidia kujenga uwezo na kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa watumiaji wote ili kulinda maisha ya watu na mali zao. Kwa upande wake, Dkt. Anthony Rea, Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu WMO alisema, majukumu ya kamati hiyo yanaenda sambamba na jitihada mbalimbali zinazoendelea kutekelezwa na WMO za kusaidia nchi katika kufanikisha upatikanaji wa data za uangazi za hali ya hewa ambazo zinazaa taarifa za hali ya hewa kwa matumizi ya nchi wanachama wa WMO. Nchi zinazoshiriki mkutano huo unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) kuanzia tarehe 20 hadi 24 Machi, 2023 ni Australia, Brazil, Canada, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Korea ya Kusini, Japan, Afrika Kusini, Hispania, Uingereza na Marekani.

TANZANIA YAADHIMIMISHA SIKU YA HALI YA HEWA DUNIANI 2023

Dodoma; Tarehe 23 Machi, 2023; Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeungana na nchi nyingine wanachama wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) kuadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani yenye Kauli Mbiu “Mustakabali wa Hali ya Hewa, Tabianchi na Maji kwa Vizazi vyote”. Akizungumza na wanahabari, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Mh Atupele Mwakibete (MB) alisema “Leo ni siku ya Hali ya Hewa Duniani. Kila mwaka ifikapo tarehe 23 Machi, Jumuiya ya Hali ya Hewa Ulimwenguni kote husherehekea siku hii, kukumbuka kuanzishwa kwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani ambapo Mkataba wa Uanzishwaji wa WMO ulisainiwa rasmi tarehe 23 Machi mwaka 1950.” Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inathamini mchango wa huduma za hali ya hewa katika maendeleo ya kijamii na uchumi wa nchi, hivyo serikali imefanya juhudi za dhati katika kuwekeza kwenye sekta ya hali ya hewa. “Katika kutatua changamoto kwenye sekta ya hali ya hewa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitunga sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ya mwaka 2019, ambayo ilihuisha utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini Tanzania na kuiongezea Mamlaka jukumu la udhibiti na uratibu wa shughuli za hali ya hewa nchini. Lengo likiwa ni kuongeza uwezo wa kitaasisi ili kusaidia uboreshwaji wa huduma za hali ya hewa.” Alisema, Mhe. Mwakibete. Aidha, Mh. Mwakibete alieleza kuwa katika kuhakikisha taarifa za hali ya hewa zinatolewa kwa usahihi na uhakika, Serikali ya Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya uwekezaji mkubwa katika huduma za hali ya hewa. Miongoni mwa uwekezaji ni ununuzi wa Miundombinu ya kisasa ya uchunguzi wa hali ya hewa ikiwa pamoja na rada za hali ya hewa, Katika kuadhimisha siku hii muhimu duniani, TMA imewakumbusha watanzania na wadau wote wa hali ya hewa kuhusu athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi duniani. Akifafanua Zaidi suala hilo kwa wanahabari, Dkt. Ladislaus Chang’a alisema “Maadhimisho ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani kwa mwaka 2023 yamekuja wakati muafaka ambapo mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi yanazidi kuongezeka na athari zake zinaonekana kila mahali na kuleta maafa ambayo yamesababishwa na ongezeko la idadi na ukubwa wa matukio ya hali mbaya ya hewa. Kwa mfano katika siku chache zilizopita, maeneo na nchi za kusini magharibi mwa Bahari ya Hindi yalikumbwa na kimbunga Freddy ambacho kilikuwa na nguvu kubwa na kilidumu kwa muda mrefu na kusababisha maafa makubwa na uharibifu wa mali, miundombinu na shughuli za kiuchumi katika nchi za Msumbiji, Malawi na Madagascar”. “Tanzania kama zilivyo nchi nyingine imeendelea kuathiriwa na kuongezeka kwa matukio ya hali mbaya ya hewa na maji yaliyosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa. Kwa wastani, joto la dunia limeongezeka kwa takribani nyuzi joto 1° na kwa upande wa Tanzania katika miaka michache iliyopita ongezeko la joto lilifikia takribani nyuzi joto 0.3 – 0.8 kwa kipimo cha sentigredi.” Alisisitiza Dkt. chang’a. Dkt. Chang’a aliwahakikishia watanzania na wadau wote wa hali ya hewa kwamba TMA itaendelea kutoa huduma bora za hali ya hewa zenye viwango vya kimataifa na watanzania watumie huduma hizi katika kufanya maamuzi ili kuongeza tija na ufanisi katika shughuli za kijamii na za kiuchumi. “Tunaposherehekea kumbukizi ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani (WMD) na miaka 150 ya Shirika la Kimataifa la Hali ya Hewa (IMO), tungependa kuihakikishia jamii na wateja wetu kuwa, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ni miongoni mwa Taasisi bora za hali ya hewa katika Bara la Afrika na katika nchi zinazoendelea na imedhamiria kutoa huduma bora za hali ya hewa zinazokidhi au kuzidi matarajio ya wateja wetu na zinazozingatia miongozo ya kitaifa na kimataifa, kwa kuendelea kuboresha taratibu zetu za kazi. Hivyo, napenda kutoa wito kwa wadau wote kuzitumia ipasavyo taaarifa na huduma za hali ya hewa zinazotolewa na TMA ili kuongeza tija na ufanisi katika kupanga, kufanya maamuzi na kutekeleza shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.” Dkt. Chang’a.

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...