Wednesday, February 22, 2023

TMA YATOA UTABIRI WA MSIMU WA MVUA ZA MASIKA 2023 KWA MAENEO YANAYOPATA MVUA MARA MBILI KWA MWAKA.


Dar es Salaam, Tarehe 22/02/2023;

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi utabiri wa msimu wa mvua za Masika 2023 kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka. Akizungumza wakati wa mkutano na vyombo vya habari katika Ofisi za TMA-Dar es Salaam, Ubungo Plaza, tarehe 22/02/2023, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a alisema maeneo mengi ya nchi yanayopata misimu miwili ya mvua yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani.

 

“Mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi yayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka isipokuwa maeneo machache ya mikoa ya Dar es Salaam, pwani (ikijumuisha mafia),kaskazini mwa Morogoro pamoja na Kisiwa cha Unguja ambapo mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa”. Alisema Dkt. Chang’a.

 

Aidha, aliongezea kuwa “Ongezeko la mvua linatarajiwa katika kipindi cha mwezi Mei 2023, hususan katika maeneo ya pwani ya kaskazini”.Alisema Dkt. Chang’a.

 

Mvua za Masika zinatarajiwa kuanza mwezi Machi 2023 katika maeneo mengi na zinatarajiwa kuisha katika wiki ya nne ya Mwezi Mei 2023, katika maeneo mengi ingawa mwendelezo wa mvua za nje ya msimu unatarajiwa mwezi Juni 2023 katika maeneo machache ya mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Morogoro kaskazini, Pwani, Kisiwa cha Mafia, kisiwa cha unguja na Pemba.

 

Akizungumzia athari zinazoweza kujitokeza, Dkt. Chang’a alisema vipindi vifupi vya mvua kubwa vinaweza kujitokeza hivyo kuweza kusababisha mafuriko, uharibifu wa miundombinu, upotevu wa mali na maisha, milipuko ya magonjwa pamoja na athari nyingine zitokanazo na mvua nyingi.

 

Kwa taarifa zaidi tembelea; www.meteo.go.tz https://www.meteo.go.tz/weather_forecasts/seasonal-weather-forecast

 

Tuesday, February 21, 2023

TMA YASITITIZA UMUHIMU WA KUFIKISHA TAARIFA ZA UTABIRI WA HALI YA HEWA KWA UHAKIKA, USAHIHI NA KWA WAKATI

 













 










Kibaha; Tarehe 21 Februari, 2023;

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imesisitiza umuhimu wa taarifa za utabiri wa hali ya hewa kutolewa kwa uhakika, usahihi na kwa wakati kwa ajili ya maendeleo ya jamii na uchumi wa nchi. Haya yalizingumzwa na Kaimu Mkurugunzi mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Dkt. Ladislaus Chang’a wakati akifungua Warsha ya ya wanahabari inayohusu mwelekeo wa msimu wa mvua za Masika kwa kipindi cha mwezi machi hadi mei 2023 yenye kauli mbiu Matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa kwa maendeleo endelevu”.

“Kama mnavyofahamu warsha hii ni muendelezo wa juhudi za kuhakikisha taarifa za utabiri wa hali ya hewa zinawafikia walengwa kwa uhakika, usahihi na kwa wakati. Napenda kuendelea kuwashukuru wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya habari ikiwa ni pamoja na mitandao ya kijamii (Online Media) kwa kuendelea kuwa nguzo muhimu katika kusambaza na kufikisha taarifa za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na tahadhari za hali mbaya ya hewa kwa watumiaji yaani jamii kwa ujumla Hii imesaidia katika kuongeza uelewa na mwamko wa jamii katika kufuatilia na kutumia taarifa za hali ya hewa” Alisema Dkt Chang’a.

Kwa kusisitiza, Dr Chang’a Alisema ” Kuongezeka kwa mwamko na uelewa kuhusu taarifa za hali ya hewa ni muhimu kwa taarifa hizi zikiifikia jamii kwa wakati, uhakika na usahihi itaisaidia jamii kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa. Vilevile, taarifa mahsusi za hali ya hewa kwaajili ya matumizi ya sekta mbalimbali zinasaidia katika ukuaji wa kiuchumi. Pia itazisaidia mamlaka zinazohusika kupanga mipango ya kukabiliana na majanga yatokanayo na hali mbaya ya hewa, mikakati ya kimaendeleo, upatikanaji wa chakula na lishe bora pamoja na afya kwa ustawi wa jamii kwa ujumla.”

Wanahabari nao walitoa pongezi na shukurani kwa Mamlaka ya hali ya hewa kwa ushirikiano wanaoendelea kupata katika uwasilishwaji wa taarifa za hali ya hewa kwa Jamii. Ushirikiano huu unatolewa kwa njia za Mafunzo ya wanahabari hapa nchini na nje ya nchi. Haya yalisemwa na Ndg Dorcas Raymos wa Channel 10, Akiwasilisha Taarifa la Jopo la wanahabari walioenda nchini kenya kwa mafunzo ya Utolewaji wa taarifa za hali ya hewa.

”Tunaishukuru Mamlaka ya hali ya hewa kwa kutupa fursa ya kushiriki mafunzo yaliyotolewa na ICPAC nchini Kenya. Pamoja na mambo mengine tulinufaika kwa kujifunza mifumo ya ufuatiliaji athari ziletwazo na hali ya mbaya ya hewa (Hazards Watch/ Drought Watch). Mfumo huu utatusaidia kupata taarifa mapema na kuwahabarisha jamiii ili iweze kuchukua tahadhari dhidi ya athari zitokanazo na hali mbaya ya hewa” Alisema Ndg Dorcas Raymos 

Kwenye Warsha Hii iliyofanyika Kibaha,Pwani, Wanahabari walipata fursa ya kujua vitu mbalimbali kama Tathmini ya Mvua za ksimu wa vuli (Oktoba hadi disemba 2022), Mwenendo wa Mvua za msiumu wa (Novemba 2022 hadi Aprili 2023). Wanahabari pia walijifunza Lugha na Maneno yanayotumiwa katika uwasilishwaji wa taarifa za utabiri wa Hali ya hewa. Mafunzo haya yalitolewa na wataalam kutoka TMA.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inatarajia kutoa Rasmi taarifa ya msimu wa mvua za Masika Tarehe 23 Februabri 2023

Monday, February 20, 2023

TMA YAKUTANA NA SEKTA MBALAMBALI NCHINI ILI KUJIPANGA NA MSIMU WA MASIKA 2023























Dar es salaam; Tarehe 20 Februari, 2023;

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imekutana na sekta mbalimbali nchini ili kujipanga na msimu wa masika, katika Ukumbi wa NIT, jijini Dar es salaam, tarehe 20 Februari, 2023.

 

Akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Dkt. Buruhani Nyenzi, alisema lengo la mkutano huo ni kujadili mwenendo wa mvua za msimu wa Masika 2023 na kuandaa taarifa zinazolenga kuchochea matumizi sahihi za huduma za hali ya hewa kulingana na utabiri utakaotolewa. Aidha, alisisitiza kuwa ushirikiano na ushirikishwaji wa wadau ni muhimu katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa.

 

“Tunapoelekea kutoa utabiri wa mvua za Masika (Machi hadi Mei), 2023 ninapenda kuipongeza Mamlaka ya Hali ya Hewa kwa kuendelea kushirikisha wadau mbalimbali kutoa michango yao katika shughuli za utoaji wa huduma za hali ya hewa ambazo ni pamoja na mchakato wa utabiri wa misimu ya mvua. Ushirikiano na ushirikishwaji huu ni muhimu sana hasa katika kipindi hiki ambapo dunia pamoja na nchi yetu tunakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa”. Alisema Dkt. Nyenzi.

 

“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuchukua hatua thabiti za kukabiliana na hali hii kwa kuimarisha miundo mbinu ya Hali ya Hewa ikiwemo ununuzi wa vifaa kama vile vifaa vya kisasa vinavyojiendesha vyenyewe na Rada”. Alisisitiza Dkt. Nyenzi.

 

Awali wakati akimkaribisha mgeni rasmi, Kaimu Mkurugenzi Mkuu, TMA, Dkt.Ladislaus Chang’a aliishukuru Serikali na wadau wa maendeleo kwa kuendelea na uwekezaji katika miundombinu ya hali ya hewa hapa nchini, kupitia jitihada hizo, Mamlaka imeendelea kutoa taarifa za utabiri wa maeneo madogo madogo kwa wilaya zote za mikoa iliyopo katika ukanda unaopata mvua za Masika na hivyo kusaidia  katika kufanya maamuzi stahiki kwa lengo la kuongeza tija na ufanisi, na pia kupunguza madhara ya hali mbaya ya hewa inapojitokeza.

 

“Kama mnavyotambua, mvua za Masika ni mahsusi kwa maeneo ya pwani ya kaskazini, nyanda za juu kaskazini mashariki, na Ziwa Viktoria ambayo hupata misimu miwili ya mvua kwa mwaka (Masika na Vuli). Mvua hizi zina mchango mkubwa katika sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, nishati, maji n.k. Hivyo, taarifa sahihi za hali ya hewa pamoja na athari zake ni muhimu kupatikana kwa wakati ili kuwezesha jamii na wadau kujipanga na kuandaa shughuli za kiuchumi na kijamii katika maeneo yao ”.Alisema Dkt. Chang’a.

 

Kwa upande wake Bi,Wilfrida Ngowi Mratibu Kitengo cha Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu alisema ‘’Serikali imeweka na imeendele kuimarisha mifumo na taratibu ya kukabiliana na maafa yatokanayo na matukio ya Hali mbaya ya Hewa ikiwemo mafuriko.

 

Naye,James Kirahuka Mhandisi Rasilimali Maji, akiwasilisha mrejesho wa msimu wa mvua uliopita, alisema baada ya kupokea utabiri wa hali ya hewa kwa msimu wa mvua za Vuli 2022 ukionesha upungufu wa mvua, TANESCO ilijipanga kwa kuongeza njia zingine za uzalishaji wa umeme ili kupunguza makali ya changamoto ya upatikanaji wa umeme.

 

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, inatarajia kutoa rasmi taarifa  ya msimu wa mvua za Masika tarehe 22 Februari 2023. 

Thursday, February 9, 2023

WATUMISHI TMA WATAKIWA KUISHI KAULI MBIU YA MHE. RAIS KWA VITENDO










 

Kibaha, Pwani 06 - 07/02/2023

 

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Ladislaus Chang’a amewataka watumishi wa TMA kutumia kauli mbiu ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa vitendo.

 

Dkt. Chang’a aliyasema hayo wakati akifungua rasmi mafunzo ya kuongeza uwezo kwa wataalam wa TMA katika utabiri wa mvua za msimu. 

 

“Watumishi wote mnatakiwa kuangalia namna gani tunaweza kuishi kwa vitendo kauli mbiu ya Kazi Iendelee kwa kuzingatia weledi na umahiri mkubwa, kauli ambayo Mhe. Rais amekuwa akiisisitiza kila wakati”. Alisema Dkt. Chang’a.

 

“Sisi, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) jukumu letu la msingi ni kutoa utabiri wa hali ya hewa hivyo mafunzo haya yatasaidia kuendeleza kazi yetu ya msingi na kutoka viwango tulivyopo kwenda viwango vya juu zaidi ikiwa ni maana halisi ya kazi iendelee”. Alisisitiza Dkt. Chang’a.

 

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri, Dkt. Hamza Kabelwa alisema mafunzo hayo ni kwaajili ya kuwajengea uwezo wataalam wa TMA na kusaidia kuboresha huduma za hali ya hewa zinazotolewa kwa wadau mbalimbali.

 

Warsha hiyo muhimu ya mafunzo juu ya utabiri wa mvua za msimu ilifanyika katika ukumbi wa mikutano wa TARI, Kibaha, Pwani, Tarehe 06 – 07 Februari, 2023 kwa ufadhili wa Taasisi ya Utafiti ya Norway ya Michelsen ambayo ni mtekelezaji wa mradi wa wa Huduma za Hali ya Hewa zinazozingatia jinsia kwa usalama wa chakula na lishe (COGENT). Lengo la mradi ni kuboresha huduma za hali ya hewa zinazotolewa na TMA kwa sekta mbalimbali katika kulinda maisha na mali za watu.

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...