Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatoa taarifa juu ya uwepo wa ongezeko la joto katika maeneo mbalimbali nchini.
Kumekuwepo na ongezeko la joto katika baadhi ya maeneo nchini. Hali hii imesababishwa na kusogea kwa jua la utosi sambamba na upungufu wa mvua katika maeneo mengi hapa nchini kama ilivyotabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania. Kwa kawaida vipindi vya jua la utosi nchini hufikia kilele mwishoni mwa mwezi Novemba wakati jua la utosi likiwa linaelekea kusini (Tropiki ya Kaprikoni) na hali hiyo hujirudia tena mwezi Februari wakati jua la utosi likiwa linaelekea kaskazini (Tropiki ya Kansa). Jua la utosi huambatana na hali ya ongezeko la joto kwa sababu uso wa dunia katika eneo tajwa huwa karibu zaidi na jua kuliko maeneo mengine.
Katika kipindi cha mwezi Oktoba, 2022, hali ya joto iliongezeka katika maeneo mbali mbali nchini. Kiwango cha juu zaidi cha joto cha nyuzi joto 36.9 0C kiliripotiwa katika kituo cha Mpanda, Katavi mnamo tarehe 26 Oktoba, 2022. Kiwango hiki ni sawa na ongezeko la nyuzi joto 4.0 0C ukilinganisha na wastani wa muda mrefu kwa mwezi Oktoba. Aidha, baadhi ya maeneo mengine yaliyokuwa na ongezeko la joto kwa mwezi Oktoba, 2022 ni pamoja na mkoa wa Tabora nyuzi joto 35.7 (ongezeko la nyuzi joto 3.0), Moshi nyuzi joto 34.1 (ongezeko la nyuzi joto 3.2) na Dar es Salaam nyuzi joto 32.8 (ongezeko la nyuzi joto 1.4).
Aidha, katika wiki mbili za mwanzo za mwezi Novemba, 2022; hali ya ongezeko la joto iliendelea kujitokeza katika baadhi ya maeneo ambapo kituo cha Mpanda kiliripoti nyuzi joto 35.4 0C mnamo tarehe 2 Novemba, 2022 ikiwa ni ongezeko la nyuzi joto 4.7 ukilinganisha na wastani wa muda mrefu kwa mwezi Novemba. Kituo cha Tabora kiliripoti nyuzi joto 34.8 (ongezeko la nyuzi joto 3.7), Dar es Salaam nyuzi joto 33.7 (ongezeko la nyuzi joto 2.1) pamoja na Kilimanjaro nyuzi joto 34.3 (ongezeko la nyuzi joto 2.4).
Vipindi vya ongezeko la joto vinatarajiwa kuendelea kujitokeza katika mwezi Novemba, 2022 hususan katika maeneo yanayotarajiwa kuendelea kuwa na upungufu wa mvua na kupungua kidogo ifikapo mwezi Disemba, 2022 ambapo ongezeko la mtawanyiko wa mvua unatarajiwa.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inaendelea kutoa wito kwa wananchi kufuatilia taarifa za mwenendo wa hali ya hewa zinazotolewa pamoja na kutafuta, kupata na kutumia ushauri wa wataalamu wa kisekta ili kuepuka au kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na hali mbaya ya hewa ikiwemo ongezeko la joto.