Dar es Salaam; Tarehe 23 Disemba, 2021;
Wataalamu nchini wametakiwa kufanya tafiti zenye tija na kuelimisha jamii kupitia njia mbalimbali ikiwemo kuandika vitabu. Hayo yalizungumzwa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Mwita Waitara (MB) wakati akizindua rasmi kitabu cha Klimatolojia na Athari zitokanazo na Matukio ya Hali Mbaya ya Hewa Tanzania, katika Ukumbi wa Mikutano ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Ubungo Plaza,Tarehe 23/12/2021.
“Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuelimisha jamii na kuwaandaa na kuwataka wataalamu kutoa mchango chanya wa kusaidia kukabiliana na changamoto hizo, ikiwemo kufanya tafiti na kuelimisha jamii”. Alizungumza Mhe. Waitara.
Aidha, Mhe. Naibu Waziri alitoa wito kwa umma kukitumia vizuri kitabu hicho ili kujipatia elimu na uelewa zaidi kuhusiana na changamoto za hali ya hewa hapa Tanzania katika kupanga na kutekeleza mipango ya kijamii na kiuchumi kwa tija na ufanisi zaidi.
Katika hatua nyingine, Mhe. Waitara aliipongeza Bodi na Menejimenti ya TMA kwa usimamizi na kazi kubwa ya kuendelea kuboresha huduma za hali ya hewa ikiwemo utabiri mzuri uliotolewa wa kuhusiana na upungufu wa mvua katika maeneo mengi ya nchi kwa msimu huu wa mvua.
“Maeneo mengi yamekuwa na upungufu mkubwa wa mvua kama ambavyo mlisema katika taarifa yenu ya mwezi Septemba,2021. Utabiri na tahadhari mnazozitoa zinamchango mkubwa katika kuongeza ufanisi na tija katika shughuli zote za kiuchumi na kijamii na pia katika utekelezaji wa Miradi ya Kimkakati kama ya SGR na Ujenzi wa Bwawa la Nyerere”. Alifafanua Mhe. Waitara.
Awali wakati akimkaribisha Mgeni Rasmi, Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Dkt. Buruhani Nyenzi alisema Kitabu hicho ni cha sayansi ya hali ya hewa kinachoweza kutumika kwa ajili ya kuendeleza tafiti za hali ya hewa hasa kwa Tanzania na suala la kujivunia ni kuwa kitabu hicho kimeandikwa na mmoja wa wataalamu kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ambaye ni Dkt. Ladislaus Chang’a.
Akizungumzia mafanikio ya kitabu hicho, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi ambaye pia ni Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), alifafanua kuwa kitabu hiki kinatoa mchango mkubwa katika kuongeza uelewa wa changamoto za hali ya hewa kwa watu wote hususan wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu pamoja na Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa kilichopo Kigoma, watafiti, makandarasi na watunga sera.
“Baadhi ya maudhui ambayo yamewekwa katika kitabu hiki ni pamoja na tathmini ya hali ya klimatolojia na mwelekeo wa joto, mvua, unyenyevu na upepo, ambapo uelewa wake ni wa muhimu sana kwasasa na hata kwa wakati ujao ili kupanga na kutekeleza shughuli zote za kiuchumi na kijamii, ikiwemo kilimo, Nishati, Afya, Maji na Usafiri”. Alifafanua Dkt. Kijazi.
Naye, mwandishi wa kitabu hicho ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utafiti na Matumizi ya Huduma za Hali ya Hewa, Dkt. Ladislaus Chang’a alieleza chimbuko la kuhamasika kuandika kitabu hicho ni kutokuwepo kwa kitabu cha namna hiyo katika kufundisha kozi za klimatolojia na mabadiliko ya hali ya hewa UDSM na SUA, ushiriki mdogo wa wanasayansi wa Afrika katika masuala ya sayansi ya mabadiliko ya hali ya hewa katika Jopo la Kiserikali la Mabadiliko ya Hali ya Hewa Duniani – IPCC, hamasa na msukumo mdogo katika masuala ya sayansi na utafiti miongoni mwa vijana na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa Tanzania na Duniani.
No comments:
Post a Comment