Washiriki mbalimbali wa Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwenye picha ya pamoja na Mgeni rasmi katika Ukumbi wa Magadu, Morogoro. |
Washiriki mbalimbali wa Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)wakati wa ufunguzi wa Baraza la Wafanyakazi wa TMA katika Ukumbi wa Magadu, Morogoro. |
Morogoro, Tarehe: 29/11/2021;
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Buruhani Nyenzi ameiagiza TMA kusimamia sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya Mwaka 2019 kikamilifu. Alizungumza hayo wakati akifungua rasmi Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), lililofanyika katika Ukumbi wa Magadu, Morogoro, tarehe 29/11/2021.
“Nawaagiza mkasimamie Sheria hii kikamilifu ikiwa ni pamoja na ukusanyaji wa mapato katika maeneo yaliyoainishwa. Hii itasaidia kuwezesha utekelezaji wa majukumu yenu kwa ufanisi mkubwa pamoja na kutatua changamoto mbali mbali zilizo katika uwezo wenu”.Alisema Dkt. Nyenzi
“Nimejulishwa pia kuwa ili kutekeleza sheria iliyoanzisha taasisi hii mmefanikiwa kuandaa kanuni zitakazowezesha utekelezaji wa sheria hiyo. Katika eneo hili, niwapongeze kwa kukamilika kwa Kanuni saba za Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya mwaka 2019 ikiwemo Kanuni ya Tozo, natambua kuwa kanuni hizi zimeshasainiwa, kilichobaki ni utekelezaji wake”.Alizungumza Dkt. Nyenzi.
Aidha, Dkt. Nyenzi aliipongeza TMA kwa kazi nzuri inayofanyika na kuwataka kuchapa kazi kwa bidii na kuendelea kutoa taarifa kwa watoa maamuzi ili kusaidia ufanyaji wa maamuzi na kuwezesha Serikali kukabiliana na changamoto zinazosababishwa na matukio ya hali mbaya ya hewa ambayo yanazidi kuongezeka kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumzia ushiriki wa TMA katika Mkutano mkubwa wa COP26 ambao Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alishiriki na kuhutubia mkutano huo. Alisema, anatambua katika maazimio ya mkutano huo TMA inajukumu la kufanya ili kufanikisha jitihada za kuhimili athari za mabadiliko ya tabia nchi, hivyo, jukumu hilo litatimizwa vyema kwani TMA ina wataalamu wanaokubalika kimataifa wakiwemo wajumbe katika kamati mbali mbali za Shirika la Hali ya Hewa Duniani na Mwenyekiti wa Baraza hili ambaye ni Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani.Aliongeza Dkt. Nyenzi.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt. Agnes Kijazi aliishukuru Serikali na kueleza madhumuni maalum ya Baraza hilo ni kufanya tathmini ya utendaji wa Mamlaka, tathmini ambayo itasaidia kuongeza ubora na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa umma kwa lengo la kupunguza athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi.
“Hivi karibuni tumeshuhudia athari mbalimbali zitokanazo na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi ikiwa ni pamoja na kuwa na vipindi vya ongezeko la joto hadi kufikia nyuzi joto 35.6 kwa maeneo ya ukanda wa Pwani. Aidha, nichukuwe fursa hii kuendelea kutoa wito kwa watanzania wenzangu kuendelea kufuatilia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kila mara ili kupunguza madhara yatokanayo na hali mbaya ya hewa”.Alifafanua Dkt. Kijazi.
Vile vile, Dkt. Kijazi alieleza baadhi ya changamoto ni mishahara midogo hali inayopelekea wataalamu kuhamia katika Taasisi zingine, hata hivyo ‘Job Evaluation’ ilishafanyika ambayo TMA inaendelea kusubiri idhini ya kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa.