Monday, May 3, 2021

BARAZA 2021: BODI YA TMA YAZUNGUMZIA UFUATILIAJI WA KIMBUNGA JOBO.















 Pwani, Tarehe: 28/04/2021;

Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Mgeni Rasmi, Dkt. Buruhani Nyenzi amezungumzia jitahada zilizofanywa na TMA katika kuutaarifu umma kuhusu kimbunga Jobo kilichotokea hivi karibuni. Dkt. Nyenzi alizungumza hayo wakati akifungua rasmi Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), lililofanyika katika Ukumbi wa Baraza la Wakunga na Manesi, Kibaha, Pwani, tarehe 28/04/2021. 

 

“Tumeshuhudia jinsi mlivyoweza kufuatilia taarifa za kimbunga Jobo na jinsi mlivyotoa taarifa za kimbunga hicho kwa weledi mkubwa. Katika zama hizi za mabadiliko ya tabia nchi mifumo ya hali ya hewa inabadilika badilika na tunashuhudia ongezeko la majanga yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa hivyo kutoa taarifa ya mwenendo wa mifumo hiyo ni jambo la muhimu”. Alisema Dkt. Nyenzi

 

“Pale ambapo mifumo inaonesha hali hatarishi watu wanachukua tahadhari na pale ambapo mifumo imerejea katika hali ya kawaida watu wanaendelea na shughuli zao na hilo ndilo mlilolifanya wakati mnakifuatilia kimbunga Jobo ‘Nawapongeza sana’ “. Aliendelea Dkt. Nyenzi

 

Aidha, Dkt. Nyenzi alizipongeza Mamlaka mbalimbali katika Serikali ambazo zilitafsiri tahadhari zilizotolewa katika mazingira yao kwa kengo la kulinda maisha ya wananchi na mali zao. 

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt. Agnes Kijazi aliishukuru Serikali hususani Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa heshima waliyowapa wana TMA ya kusimamia utendaji wa Taasisi ya Hali ya Hewa hapa nchini kwa ustawi wa maendeleo ya nchi yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Vile vile aliishukuru Serikali kwa uwezeshaji wa masuala mbalimbali ikiwemo kusimamia upatikanaji wa sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa na uboreshaji wa miundo mbinu zikiwemo rada za hali ya hewa

“Kwa ujumla maboresho na uwekezaji uliofanywa na Serikali katika sekta ya hali ya hewa umesababisha kuongezeka kwa usahihi wa utabiri na hivyo kuchangia katika azma ya Serikali ya kujenga na kukuza uchumi shindani kama ilivyoainishwa katika Ilani ya Chama Tawala”. Alisema Dkt. Kijazi.

Akifunga rasmi Baraza hilo, Mgeni Rasmi na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Dkt. Makame Omar Makame aliipongeza TMA kwa kufanya kazi kubwa kwa saa 24 wakati wa tishio la Kimbunga Jobo na kusaidia kupunguza taharuki kwa jamii. Aidha, alitoa wito kwa wajumbe wa Baraza kuboresha utendaji kazi wao kwa kupitia mijadala iliyofanyika ikiwemo suala la maslahi bora.

“Ni vyema niwakumbushe wajumbe na kupitia kwenu wafanyakazi wote wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kuwa, siku zote maslahi huendana na wajibu. Hivyo pamoja na kuomba uboreshaji wa maslahi, mnao wajibu wa kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha sekta ya hali ya hewa inachangia katika maendeleo ya uchumi wa Taifa letu”. Alizungumza Dkt. Makame.

Baraza hilo lilihudhuriwa na wajumbe tisini na nane kutoka vituo vya hali ya hewa Tanzania bara na Tanzania Zanzibar pamoja na wageni waalikwa kutoka wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (sekta ya uchukuzi) na wawakilishi kutoka TUGHE taifa. Wajumbe walipata fursa ya kujadili Bajeti ya Mamlaka kwa Mwaka 2021/2022 na kumaliza kwa kuweka maazimio ya kimkakati yenye lengo la kuongeza ufanisi katika sekta ya hali ya hewa hapa nchini.

 

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...