Dar es
Salaam, Tarehe 08/04/2020:
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa
ripoti ya tathimini ya hali ya hewa ya Tanzania kwa mwaka 2019. Uzinduzi wa
ripoti hiyo ulifanyika wakati wa kikao cha Bodi ya TMA kilichofanyika katika
ofisi za Makao Makuu ya TMA.
Akizungumzia ripoti hiyo Mkurugenzi Mkuu wa TMA,
Dkt. Agnes Kijazi alisema mwaka 2019 umechukua nafasi ya nne kwa kurekodi kiasi
cha mvua nyingi tangu mwaka 1970.
“Kiwango cha mvua nchini kwa mwaka 2019 kilikuwa ni
wastani wa milimita
1283.5 sawa na asilimia 125 ya wastani wa mvua ya muda mrefu
(1981-2010), kiwango hiki ni zaidi ya wastani wa mvua ya muda mrefu kwa milimita 256.5.
Katika historia, mvua hii imechukua nafasi ya nne kwa wingi kati ya miaka iliyopata
mvua nyingi zaidi tangu mwaka 1970 ambapo miaka iliyokua na mvua nyingi zaidi tangu mwaka 1970 ni 1982, 1997 na 2006”. Alisema Dkt. Kijazi
Aidha, ripoti hiyo ilieleza kuwa takwimu
zinaonesha kuwa joto la nchi limeendelea kuongezeka kwa kiwango cha juu kuanzia
mwaka 1995, ambapo joto la usiku limeongezeka zaidi ilikilinganishwa na joto la
mchana. Pamoja na hayo taarifa za ripoti zitolewazo zimekuwa zikichangia ripoti
za tathimini ya hali ya hewa ya dunia zinazoandaliwa na Shirika la Hali ya Hewa
Duniani (WMO).
Vilevile Dkt. Kijazi alitoa wito kwa wadau wa
sekta mbalimbali kutumia taarifa zilizopo kwenye ripoti hiyo kwaajili ya
mipango ya maendeleo ya kiuchumi na jamii kama vile kilimo, ujenzi, maendeleo ya
viwanda n.k
Awali wakati akitoa maelezo ya jumla, Mkurugenzi wa
Utafiti na Matumizi ya Hali ya Hewa, Dkt. Ladislaus Chang’a alisema kuwa,
ripoti hizi zimekuwa zikitolewa tokea mwaka 2011 hadi 2019 na lengo ni kukuza
ufahamu na uelewa kwa jamii, wadau na watoa maamuzi juu ya mabadiliko ya hali
ya hewa na tabia nchi. “Tathmini za ripoti hizi huonesha taarifa za kina za
uchambuzi wa hali ya hewa na athari zake na kuziweka katika mtazamo wa
kihistoria”. Alisema Dkt. Chang’a
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya
Hali ya Hewa Dkt. Buruhani Nyenzi aliipongeza Menejimenti ya TMA kwa kutoa
taarifa hiyo kwani ilielezwa kwamba ni nchi mbili tu Afrika ambazo zinatoa
taarifa hizo ikiwemo Tanzania na Ivory Coast
No comments:
Post a Comment