Dar es Salaam, 17 Aprili 2020:
Kumekuwa na
hali ya taharuki na maswali kutoka kwa umma terehe 16 Aprili, 2020 jioni kuhusu
mwonekano wa anga kuwa na rangi nyekundu au chungwa katika baadhi ya maeneo
nchini. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
(TMA) inatoa ufafanuzi kuhusu hali hiyo ya anga kama ifuatavyo;
Mwonekano
huo wa rangi ya anga ni hali ya kawaida ambayo hutokea wakati jua linapozama au
kuchomoza katika mazingira yenye kuwa na hali ya hewa kama vile mawingu, matone
madogo madogo ya maji na barafu katika anga mara mvua inapokatika na jua
linapokuwa katika upande tofauti na eneo mvua inaponyesha. Hali ambayo husababisha
kutawanywa kwa miale ya mwanga wa jua. Hivyo kutokana na ukubwa wa matone ya
maji katika wingu na chembechembe za vumbi katika anga, sehemu ya miale ya jua
inayotawanywa zaidi katika mazingira hayo ni mawimbi ya miale ya jua
inayohusiana na rangi nyekundu au chungwa hivyo kufanya anga kuonekana katika
rangi hizo (Mawimbi madogo sana
huwakilisha rangi ya blue na makubwa rangi nyekundu au rangi ya chungwa). Hali
hii haina tofauti sana na namna Upinde Mvua unavyojitokeza angani, isipokuwa
upinde mvua unakuwa na rangi zote saba za spectrum ya mwanga. Mabadiliko hayo ya hali ya anga hayana madhara
yeyote.
Katika hali
iliyozoeleka mara nyingi, anga huonekana kuwa rangi ya bluu kutokana na
kutawanywa kwa mawimbi ya miale ya jua kunakofanywa na gesi ya Nitrojeni na
Oksijeni ambazo ndizo hufanya sehemu kubwa ya gesi katika hewa. Hali hiyo
inatokana na molekuli za gesi hizo kuwa ni ndogo sana hivyo hutawanya sehemu ya
mawimbi madogo zaidi ya miale ya jua iliyo katika rangi ya blue katika spectrum
ya mwanga. Rangi hiyo huonekana katika macho ya binadamu kwa kipindi hicho.