Katika jitihada za kuhakikisha Mamlaka ya Hali ya Hewa
Tanzania (TMA) inafikia viwango vya kimataifa kulingana na matakwa ya Shirika
la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Chuo cha Hali ya Hewa Kigoma kimefanikiwa
kufanya awamu ya tatu ya kozi ya huduma
za hali ya hewa kwa usafiri wa anga kwa baadhi ya wafanyakazi wa TMA.
Akifunga rasmi kozi hiyo na kuwatunuku vyeti wahitimu,
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TMA, Dkt. Buruhani Nyenzi aliwataka wahitimu
wote pamoja na wafanyakazi wengine wa Mamlaka kuwa vielelezo katika
vituo vyao vya kazi katika kuzingatia maadili, kanuni na taratibu za kazi na
kufanya kazi kwa weledi mkubwa hususani kwenye sekta ya usafiri wa anga. Aidha
aliahidi kwamba Bodi itashirikiana na menejimenti ya TMA kuhakikisha kwamba
miundo mbinu ya Chuo cha Hali ya Hewa Kigoma inaboreshwa.
Akimkaribisha mgeni rasmi Dkt. Agnes
Kijazi, Mkuruggenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa alisema mafunzo hayo ni
sehemu ya kutekeleza mpango mkakati wa Mamlaka wa kuendeleza watumishi ili
kukidhi viwango vya Shirika la Hali ya Hewa Duniani.
Naye Mkuu wa Chuo cha Hali ya Hewa Kigoma, Bw. Joseph
Aliba alitoa shukrani za dhati kwa serikali kwa kuwezesha uboreshaji wa huduma
kama vile usajili wa chuo, maktaba, ujenzi wa uzio wa chuo, mafunzo kwa
waalimu, kuunganishwa katika mkongo wa Taifa huku akitaja baadhi ya changamoto
zilizopo.
Akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wote, Bi.
Beatrice Kitero, alishukuru Mamlaka kwa mafunzo na kuahidi kuyafanyia kazi
katika uboreshaji wa huduma za hali ya hewa kwaajili ya usafiri wa anga nchini.
Kozi ya huduma za hali ya hewa kwaajili ya usafiri wa
anga, imeandaliwa na Chuo cha Hali ya Hewa Kigoma kwa muda wa mwezi mmoja na ilifanyika Makao Makuu ya TMA, Ubungo Plaza, Dar es Salaam. Wahitimu
ni wafanyakazi wa Mamlaka waliohitimu degree ya Hali ya Hewa kutoka
vituo vya Mbeya, Dodoma, Kigoma, Makao Makuu (DSM) na Zanzibar.
No comments:
Post a Comment