Wafanyakazi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
wametakiwa kuachana na mfumo wa zamani wa kutumia makaratasi katika kuhifadhi
taarifa zao muhimu na badala yake kuanza
kutumia mfumo wa kisasa wa kieletroniki.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
Pof. Makame Mbarawa jana jijini Dar es
Salaam wakati wa mkutano na wafanyakazi hao na kueleza kuwa kwa kufanya hivyo
kutasaidia kupunguza matumizi ya fedha za kununulia karatasi.
“Katika ofisi zenu nimeona kila mtu anakomputa ni jambo zuri
hivyo zitumieni katika kuhifadhi taarifa muhimu za taasisi yenu kwa mfumo wa
kieletroniki,” alisema Prof.Mbarawa.
Aliongeza kwa kusema
kuwa serikali imetumia fedha nyingi katika kujenga mkongo wa taifa wa kuhifadhi
taarifa muhimu hususani za serikali
pamoja na taasisi zake hivyo ni budi
waanze kuutumia mkongo huo kwa kuhifadhia taarifa zao.
Pia amewataka watumishi kuwa waadilifu,wachapaka kazi,
wabunifu na kuwa na uwazi baina ya watendaji wa juu na watumishi wa ngazi ya
chini kwa kushirikiana na wafanyakazi wa
mikoani.
“Watanzania wanamatarajio mengi kutoka kwetu katika kukuza uchumi wa nchi hivyo ni wajibu
wetu kutimiza matarajio yao kwa kuwapatia mahitaji muhimu ikiwemo miundo mbinu
imara ya barabara, bandari ,shirika la ndege la kisasa na utabiri wa hali ya hewa wenye uhakika,” alisema Prof.
Mbarawa.
Prof. Mbarawa alitoa
wito kwa kuwataka watumishi hao kufanya
kazi kwa ushirikiano kila mmmoja
kujituma katika eneo lake la kazi ili kuleta matokeo yaliyobora na hivyo kukuza
uchumi wa nchi kwa kufikia uchumi wa kati.
Na Lorietha Laurence – Maelezo