Wednesday, March 23, 2016

TMA-MAKAO MAKUU YAADHIMISHA KILELE CHA SIKU YA HALI YA HEWA DUNIANI KWA KUPANDA MITI

Mkurugenzi Mkuu-TMA, Dkt. Agness Kijazi akiongoza zoezi la kupanda miti katika kiwanja cha TMA kilichopo maeneo ya Sinza (Simu 2000) kama ishara ya ushiriki wa zoezi la upandaji miti nchini, tukio hilo limeenda sambamba na kilele cha maadhimisho ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani kwa kushirikiana na Wakala wa Misitu Tanzania.

Tuesday, March 8, 2016

DKT. KIJAZI ATOA MWELEKEO WA MVUA KWA KIPINDI CHA MACHI - MEI 2016 NCHINI KWA VYOMBO VYA HABARI, MWANZA




MWELEKEO WA MVUA ZA MACHI - MEI 2016
Kutokana na mwelekeo wa mifumo ya hali ya hewa inayotarajiwa, mvua za Machi hadi Mei, 2016 zinatarajiwa kuwa kama ifuatavyo:-
(i)     Mvua za Masika (kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua)
Msimu wa mvua za Masika katika kipindi cha  miezi ya Machi hadi Mei, 2016 ni mahususi katika maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara), pwani ya kaskazini, (Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Morogoro-kaskazini pamoja na Visiwa vya Unguja na Pemba), kanda ya Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga) na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma. Mvua hizo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani kwa maeneo mengi ya ukanda huo isipokuwa maeneo ya kusini mwa ukanda huo yanatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi chini ya wastani.
Mwelekeo wa msimu wa mvua za Masika, 2016 ni kama ifuatavyo:-

Kanda ya Ziwa Victoria: (Mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga): Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza ya  mwezi  Machi, 2016 katika mikoa ya Kagera na Mara na kusambaa katika mikoa ya Geita, Mwanza, Shinyanga na Simiyu katika wiki ya pili ya mwezi Machi 2016. Mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo ya mikoa ya Kagera, Mwanza, Mara na kaskazini mwa mkoa wa Geita. Kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, kusini mwa Geita na Simiyu, pamoja na  mkoa wa Shinyanga mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani.

Ukanda wa Pwani ya Kaskazini: (Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Morogoro-kaskazini pamoja na Visiwa vya Unguja na Pemba):
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya pili hadi ya tatu  ya mwezi Machi, 2016 na zinatarajiwa kuwa za wastani  hadi juu ya wastani katika maeneo ya  kaskazini  na mashariki mwa mkoa wa Tanga ; na Visiwa vya Unguja na Pemba. Mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro pamoja na maeneo ya  kusini magharibi mwa mkoa wa Tanga.

Nyanda za juu Kaskazini Mashariki: (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara):
Mvua katika maeneo haya zinatarajiwa kuanza katika wiki ya pili hadi tatu ya  mwezi Machi, 2016. Mvua hizo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika  maeneo mengi ya mikoa ya Arusha na Kilimanjaro pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Manyara; na zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani katika maeneo mengi ya mkoa wa Manyara na kusini mwa mkoa wa Arusha.


(ii) Mvua za Msimu (Novemba – Aprili) kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua.
Mvua za msimu (Novemba hadi Aprili) ni mahususi kwa maeneo ya  Magharibi mwa nchi (Mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi na Rukwa), kanda ya  kati (Mikoa ya Singida na Dodoma), nyanda za juu kusini-Magharibi (Mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe na kusini mwa Morogoro), kusini mwa nchi na pwani ya kusini (mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara).  Mvua hizo zilianza mwezi Novemba 2015 na zinatarajiwa kuendelea hadi  mwezi Aprili, 2016. Katika maeneo hayo mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani katika maeneo mengi.

Kanda ya Magharibi (Mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi na Rukwa):
Katika kipindi kilichobaki cha msimu, mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani na zinatarajiwa kuisha mnamo wiki ya nne ya mwezi Aprili, 2016.

Kanda ya kati (Mikoa ya Singida na Dodoma):
Katika kipindi kilichobaki cha msimu, mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani na zinatarajiwa kuisha mnamo wiki ya kwanza ya mwezi Aprili, 2016.

Nyanda za juu Kusini Magharibi: (Mikoa ya Mbeya, Songwe Iringa, Njombe na kusini mwa Morogoro):
Katika kipindi kilichobaki cha msimu, mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani na zinatarajiwa kuisha mnamo wiki ya tatu ya mwezi Aprili, 2016 katika maeneo ya mikoa ya Mbeya , Songwe na Njombe na zinatarajiwa kuisha katika wiki ya kwanza ya mwezi Mei, 2016 katika maeneo ya mkoa wa Iringa.

Maeneo ya kusini na pwani ya kusini (Mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara)
Katika kipindi kilichobaki cha msimu, mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani na zinatarajiwa kuisha mnamo wiki ya pili ya mwezi Aprili, 2016.




KATIBU TAWALA WA WILAYA YA NYAMAGANA MKOANI MWANZA AWATAKA WANAHABARI KUTUMIA FURSA YA MAFUNZO YA EL-NINO NA ATHARI ZAKE KWA KIPINDI CHA UTABIRI WA MSIMU WA MVUA ZA VULI 2015 KAMA CHACHU YA UBORESHAJI WA ELIMU KWA JAMII.



Katibu tawala wa Wilaya ya Nyamagana Bibi Mayala amewataka wanahabari kutumia fursa ya mafunzo ya El Nino na athari zake katika msimu wa VULI katika kuboresha elimu kwa jamii kuhusu athari za El Nino nchini. Bibi Mayala aliyasema hayo wakati akifungua warsha ya wanahabari iliyofanyika Jijini Mwanza, tarehe 02 Februari 2016. Aidha, aliwapongeza TMA kwa jitihada zao kubwa za kuelimisha wanahabari kwa kuwa vyombo vya habari ni sekta muhimu katika kufikisha taarifa za hali ya hewa kwa wananchi.

Katika warsha hiyo Dkt. Kijazi ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa TMA alisema  warsha hiyo ni muhimu kwani itawawezesha wana habari kuwa na uelewa mkubwa wa taarifa za hali ya hewa na hivyo kuzisamabaza kwa usahihi zaidi. Aidha aliwashukuru wana habari kwa kuhuduria warsha hiyo na ushirikiano wanaoutoa katika kuhakikisha kwamba taarifa zinazotolewa na TMA zinawafikia wadau kwa wakati.  Dkt. Kijazi aliwashukuru wafadhili wa warsha hiyo ambao ni Serikali ya Norway kupitia Shirika la Hali ya Hewa ulimwenguni.

Kwa upande wa wanahabari, Bi. Theopista Nsanzugwanko kutoka gazeti la Habari Leo alisema semina hii itasaidia waandishi wa habari kuweza kujifunza masuala mbalimbali kuhusu mifumo ya hali ya hewa na kuwezesha kuandika  habari kwa usahihi na kusaidia jamii kutumia vema taarifa za hali ya hewa. Pia itawezesha jamii kupata elimu ya kukabiliana na madhara ya mvua za El Nino ili kupunguza madhara kwa jamii ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za tahadhari kwa usahihi zaidi.

TMA imekuwa ikiandaa warsha mbalimbali kwa wadau mbalimbali wakiwemo wanahabari katika mwendelezo wa utoaji elimu ya sayansi ya hali ya hewa pamoja na kudumisha ushirikiano baina ya Mamlaka na watumiaji wa taarifa za hali ya hewa ambao ni wadau kutoka sekta mbalimbali. Warsha hiyo imejumuisha wanahabari kutoka vyombo mbali mbali vya habari hapa nchini ambao wako Dar es Salaam na Mwanza.

IMETOLEWA NA MONICA MUTONI; AFISA UHUSIANO, MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA.

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...