Tarehe ya 23 Machi kila
mwaka Shirika la Hali ya Hewa Duniani kwa kushirikiana na wadau mbali-mbali
huadhimisha siku ya hali yahewa Duniani.
Maadhimisho haya ni kumbukumbu ya siku ya kuanzishwa kwa Shirika la Hali ya
Hewa Duniani tarehe 23 Machi, 1950. Katika kusherehekea siku hii Shirika la
Hali ya Hewa Duniani hutoa kauli-mbiu inayotumika na nchi zote wanachama. Kauli-mbiu ya mwaka huu ni “Uelewa wa Hali ya Hewa kwa maamuzi stahiki”
(Climate
Knowledge for Climate Action). Kauli mbiu hii inalenga kutambua umuhimu wa kuhusisha
masuala ya hali ya hewa katika shughuli
za maendeleo za kijamii na kiuchumi hususan katika kipindi hiki cha mabadiliko ya
hali ya hewa (climate change). Maarifa ya hali ya hewa ambayo
yamejengeka katika miongo kadhaa iliyopita ni mchango mkubwa sana na rasilimali
kubwa katika kufanya maamuzi stahiki ya matumizi ya taarifa za hali ya hewa.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilianzishwa kwa sheria
ya wakala wa serikali Na. 30 ya mwaka 1997 na kuzinduliwa rasmi mwezi Desemba
1999. Mamlaka inafanya kazi zake kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya
Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na inaiwakilisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Shirika hilo. Tanzania kupitia TMA inaadhimisha
siku hii ya hali ya hewa duniani kwa kusherehekea mafanikio yaliyofikiwa na WMO
tangu kuanzishwa kwake na Mafanikio ya uboreshaji wa huduma za hali ya hewa
hapa nchini.
Miongoni mwa majukumu ya TMA ni pamoja
na kufanya shughuli za uangazi, kukusanya na kuhifadhi data na takwimu za hali ya hewa, kutoa utabiri
wa hali ya hewa na usambazaji wa taarifa za hali ya hewa hapa nchini na nje ya
nchi. TMA pia inaiwakilisha Tanzania katika masuala ya hali ya hewa kimataifa
na pia Mamlaka inashirikiana na wadau wengine hapa nchini na katika
kanda ya Afrika mashariki na kusini mwa Afrika ili kuboresha utabiri wa hali ya
hewa wa msimu ambao ni muhimu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Tunaposherekea siku ya hali ya hewa Duniani, Mamlaka
ya Hali ya Hewa Tanzania inajitahidi kutoa huduma za
hali ya hewa za kuaminika, zinazotolewa
kwa wakati, zenye viwango vya usahihi vinavyokubalika
na katika lugha rahisi na ya kueleweka ili kukidhi mahitaji ya jamii ikiwa ni pamoja na
watoa maamuzi na hivyo kuchangia katika maendeleo ya Taifa. Mfano mzuri wa
matumizi ya taarifa za hali ya hewa
katika kufanya maamuzi ni katika sekta ya kilimo na usafiri wa Anga.
Uelewa wa kuanza, kuisha na urefu wa msimu wa mvua ni muhimu katika kufanya
maamuzi ya shughuli za kilimo kama vile, wakati gani wa kupanda na kuvuna, pia
aina gani ya mazao yanaweza kupandwa , wakati gani wa kunyunyizia dawa na namna
gani ya kuhifadhi mazao. Katika Usafiri
wa anga taarifa za hali ya hewa ni muhimu wakati wa kutua, kupaa na usafiri wa
ndege inapokuwa angani. Aidha, taarifa za hali ya hewa zinatumika kibiashara na
wamiliki wa ndege katika kujua kiasi cha mafuta yanayohitajika na kiasi cha mzigo
unaoweza kubebwa katika safari husika.
Maeneo mengine
ambayo taarifa za hali ya hewa ni za muhimu ni katika ujenzi, mipango miji
pamoja na utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi. Taarifa za hali ya hewa husaidia wahandisi na
maafisa mipango miji kuainisha maeneo ya kuweka miundombinu mbalimbali ikiwemo
ya mifumo ya maji safi na maji taka,
ujenzi wa madaraja n.k. Takwimu za vimbunga na mfumo wa upepo katika
ukanda wa Pwani ni muhimu sana katika shughuli zinazoendelea za utafiti na
uchimbaji wa mafuta. Idadi ya siku ambazo mvua itanyesha na hali ya joto ya
mahali husika ni muhimu katika sekta ya utalii. Taarifa za matukio ya hali
mbaya ya hewa kama vile mafuriko na ukame, upepo mkali pamoja na mvua ya mawe
na kujua eneo litakalo athirika ni muhimu sana katika mipango mbalimbali ya
maendeleo.
Hii ni baadhi ya mifano michache tu ambapo uhitaji na
uelewa wa huduma za hali ya hewa hauepukiki. Katika kuhakikisha kuwa jamii yetu
inafikiwa na huduma hizi muhimu za hali ya hewa, Mamlaka ya Hali ya Hewa
Tanzania (TMA) husambaza taarifa hizi kwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari
na mitandao ya kijamii kama vile, Facebook, Twitter, YouTube.
Kutokana na kuongezeka uelewa wa sayansi ya hali ya
hewa, utabiri wa hali ya hewa umeendelea kuongezeka viwango vya usahihi na
hivyo nashauri sekta zote za kiuchumi na kijamii hapa nchini kuendelea kutumia
taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya hali ya hewa katika kupanga mipango yao ya muda mfupi na
mrefu. Endapo utabiri wa hali ya hewa utolewao na TMA utazingatiwa na kutumiwa
kwa makini utasaidia sana katika kupunguza athari za majanga yanayosababishwa
na hali mbaya ya hewa . Adha, ikumbukwe
kwamba, kuna uwezekano mkubwa wa kuokoa maisha na kupunguza hasara ya upotevu
wa mali kwa kuwa na matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa.
TMA imepata cheti cha ubora cha kimataifa (ISO 9001:2008) katika
utoaji wa huduma bora za hali ya hewa
kwa usafiri wa anga. Cheti hiki kilipatikana mwaka 2011 na hii ni sifa kwa nchi
yetu hasa ikikumbukwa kuwa Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza kupata cheti hicho
kwa nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara. Mipango iko mbioni kuhakikisha huduma
zitolewazo na TMA katika sekta zote zinasajiliwa na shirika la viwango
duniani. Hivyo tunaposherehekea siku ya
hali ya hewa Duniani naendelea kuwashauri watanzania wenzangu katika sekta zote
za kiuchumi na kijamii kutumia taarifa za hali ya hewa kwa maendeleo endelevu
ya taifa letu. Nawatakia maadhimisho mema ya siku
ya hali ya hewa duniani mwaka huu wa 2015
“Uelewa wa Hali ya Hewa kwa maamuzi stahiki”
No comments:
Post a Comment