Thursday, February 12, 2026

SERIKALI YATENGA BILIONI 13 KUWEZESHA UJENZI WA OFISI ZA TMA.

 









SERIKALI YATENGA BILIONI 13 KUWEZESHA UJENZI WA OFISI ZA TMA.


Naibu Waziri wa Wizara ya Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile, ametembelea ujenzi wa ofisi za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) zilizopo Sinza Simu 2000, jijini Dar es Salaam. Ujenzi huu, unaofadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, unalenga kuongeza ufanisi wa utoaji wa taarifa sahihi za hali ya hewa.


Akizungumza katika ziara hiyo,Naibu Waziri wa Uchukuzi,Mhe.David Kihenzile amesema Serikali ya Awamu ya Sita imetenga takribani shilingi bilioni 13 kwa ajili ya ujenzi wa  ofisi za TMA. Miradi hiyo inahusisha ujenzi wa jengo la kisasa la Kanda ya Mashariki na Utoaji Tahadhari za Hali ya Hewa pamoja na kituo cha tahadhari za Tsunami nchini,pamoja na Kituo cha Taifa cha Uhakiki wa Vifaa vya Hali ya Hewa (National Meteorological Calibration Centre) kitakachosaidia kukagua na kuboresha vifaa vya hali ya hewa.


Mhe. Kihenzile amesema majengo yote mawili, yaliyoanza kujengwa mwaka 2023 na 2025, yanatarajiwa kukamilika kabla ya mwisho wa mwaka huu. Ameeleza kuwa miradi hiyo itaongeza ufanisi katika utoaji wa taarifa za hali ya hewa na kuwawezesha wataalamu kufanya kazi katika mazingira bora na ya kisasa.


Kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi,Mhe.David Kihenzile (MB), ametoa rai kwa Bodi na Menejimenti ya TMA kusimamia miradi hiyo kwa weledi, uzalendo na kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa ubora uliokusudiwa.Aidha aliipongeza TMA kwa kumchagua mkandarasi wa ndani, Chuo cha DIT (Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam), kutekeleza miradi hiyo akieleza kuwa hatua hiyo inachochea maendeleo ya wataalamu na taasisi za ndani.


Pia,Naibu Waziri amewahimiza TMA kutoa taarifa kwa wakati ili kuwasaidia wananchi katika shughuli za kila siku zikiwemo usafiri, kilimo na matumizi ya bahari na amewahimiza wananchi kuendelea kuamini na kutumia taarifa rasmi za hali ya hewa kutoka TMA.

Thursday, February 5, 2026

TMA YATOA UTABIRI WA MSIMU WA MVUA ZA MASIKA 2026 KWA MAENEO YANAYOPATA MVUA MARA MBILI KWA MWAKA.

 


Dar es Salaam, Tarehe 05/02/2026;


Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi utabiri wa msimu wa mvua za Masika 2026 kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka. Akizungumza wakati wa mkutano na vyombo mbalimbali vya habari katika ukumbi wa Ubungo Plaza, tarehe 05/02/2026, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi Dkt. Ladislaus Chan’ga alisema maeneo mengi ya nchi yanayopata misimu miwili ya mvua yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.

 

 “Mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi ikihusisha Pwani ya Kaskazini pamoja na baadhi ya maeneo ya Magharibi mwa ukanda wa Ziwa Viktoria (mikoa ya Kagera na Geita) pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, isipokuwa maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki na baadhi ya maeneo ya ukanda wa Ziwa Viktoria (mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara na Simiyu) mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani zinatarajiwa”. Alisema Dkt. Chang’a.

 

Katika taarifa hiyo ilielezea kuwa Mvua za Masika zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Februari na ya kwanza ya mwezi Machi , 2026 katika maeneo ya kanda ya Ziwa Victoria; na wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Machi katika maeneo ya pwani ya kaskazini; na wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Machi,  2026 katika maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki, Mvua hizo zikitarajiwa kuisha wiki ya nne ya mwezi Mei na wiki ya kwanza ya mwezi Juni 2026 katika maeneo mengi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka huku ongezeko la mvua likitarajiwa katika kipindi cha mwezi Aprili 2026.


Akizungumzia athari zinazoweza kujitokeza, Dkt. Chang’a alisema vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi pamoja na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao katika baadhi ya maeneo, hususan yanayotarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani. Kina cha maji katika mito, mabwawa na hifadhi ya maji ardhini kinatarajiwa kupungua hususan katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani. Magonjwa ya mlipuko yanaweza kujitokeza kutokana na uchafuzi wa maji, hivyo kushauri watumiaji wa tarifa hizo kuzingatia ushauri wa wataalamu katika sekta zao.


Angalizo la matukio ya hali mbaya ya hewa ikiwemo vipindi vya mvua kubwa lilitolewa hata katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani huku watumiaji wa taarifa hiyo wakishauriwa kufuatilia taarifa za utabiri wa saa 24, siku 10, mwezi na tahadhari kama zinavyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).

 

Kwa taarifa zaidi tembelea; https://www.meteo.go.tz/uploads/documents/sw-1770290524-Taarifa%20ya%20Mwelekeo%20wa%20Mvua%20za%20Masika%202026.pdf



Tuesday, February 3, 2026

WADAU SEKTA YA HALI YA HEWA WAJADILI UTABIRI WA MASIKA 2026.

Dodoma, tarehe 2 Februari 2026:

Wadau kutoka sekta mbalimbali nchini wamekutana kujadili utabiri wa msimu wa Masika 2026 na kutoa ushauri wa kisekta katika Mkutano wa 25   wa Wadau wa Sekta ya Hali ya Hewa katika msimu wa Masika uliofanyika tarehe 2/2/2026, Jijini Dodoma. Mkutano huo ni mwendelezo wa ushirikishwaji wa wadau katika utoaji wa taarifa za hali ya hewa kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini. 

Mgeni Rasmi kwenye mkutano huo, Mh. Jaji  Mshibe Ali Bakari ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya TMA  alisema





























“msimu wa Vuli mwaka 2025 ulitawaliwa  na vipindi virefu vya ukavu katika maeneo mengi ya nchi, usahihi wa utabiri ulikuwa kwa asilimia 94.1, ikiwa ni kiwango kikubwa sana, natoa wito kwa wananchi waendelee kuiamini TMA, wazingatie taarifa zinazotolewa na kuzitumia katika shughuli zao za kila siku".  

Aidha, alisisitiza kuwa majadiliano ya mvua za Masika kwa mwaka 2026, yazingatie kwa kina athari zinazoweza kujitokeza pamoja na kutoa ushauri wa hatua stahiki za kuchukua kwa ajili ya matumizi ya taarifa hizo katika sekta mbalimbali zinazochangia ukuaji wa uchumi.

Awali, akimkaribisha Mgeni Rasmi, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Changa, alisema "katika kupunguza pengo la uelewa wa tahadhari za hali ya hewa, Mamlaka imeendelea na juhudi za kushirikisha wadau, katika kuandaa taarifa zinazolenga kuchochea matumizi sahihi ya huduma za hali ya hewa nchini"

Dkt. Changa aliongeza kuwa TMA imeendelea kufanya shughuli zake kwa ubora unaoendana na viwango vya kitaifa na kimataifa na kuifanya Tanzania kuwa moja ya  nchi zinazoaminika kwa utoaji wa huduma bora za hali ya hewa duniani. Kupitia viwango hivyo,Tanzania imechaguliwa kuandaa  Mkutano wa Nne wa Kimataifa wa Watalaam Bingwa wa Hali ya Hewa Duniani, mwezi Juni 2026.

Kwa upande wa wadau, walitoa pongezi na shukrani kwa TMA kwa ushirikiano wanaoendelea kupata katika kuwasilisha taarifa za hali ya hewa kwa jamii. "Naipongeza TMA kwa kuandaa mkutano huu wa wadau wa hali ya hewa.Sisi ili tuweze kufanya kazi zetu ni lazima tupate taarifa zinazotusaidia katika mipango yetu ya kazi ili kulinda usalama wa wananchi na mali zao".Alisema Kaimu Mkurugenzi  wa Kamisheni Ya Maafa, Ofisi ya Makamu wa Rais wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Ndg. Muhidin Ali Muhidin 

Mamlaka inatarajia kutoa utabiri wa msimu wa Masika 2026, tarehe 5/2/2026.

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...