Monday, March 24, 2025

TMA YAADHIMISHA SIKU YA HALI YA HEWA DUNIANI KWA KUTOA ELIMU NCHINI










• Serikali yaipongeza kwa utendaji kazi wake

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani (WMD) Machi 23, 2025 kwa kutoa elimu katika maeneo mbalimbali nchini pamoja na kusheherekea miaka 75 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO).

Katika siku hiyo, Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Mwakiposa Kihenzile alitoa ujumbe kwa umma akimwakilisha Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa na kupongeza kazi nzuri inayofanywa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kwa kutoa huduma bora.

“Katika Siku hii ya Hali ya Hewa Duniani, Serikali inapongeza kazi nzuri inayofanywa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) katika utoaji wa huduma za hali ya hewa zilizoboreshwa sana, ikiwa ni pamoja na utoaji wa tahadhari wakati wa matukio ya hali mbaya ya hewa”. Alisema Mhe. Kihenzile.

Mhe. Kihenzile alieleza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha huduma za hali ya hewa kwa kuwekeza katika miundombinu ya kisasa zaidi na kuendelea kuwajengea uwezo wataalamu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt. Ladslaus Chang’a amesema Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imechukua hatua za kimkakati kupitia teknolojia za kisasa kama akili mnemba (AI) kuboresha utabiri na tahadhari za hali mbaya ya hewa.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Kwa Pamoja Tushughulikie Pengo la Utoaji wa Tahadhari”.

Wednesday, March 19, 2025

MRADI WA HUDUMA ZA TAHADHARI ZA HALI MBAYA YA HALI YA HEWA WAZINDULIWA RASMI TANZANIA






















Tarehe 19/03/2025

Naibu Waziri wa Wizara ya Uchukuzi, Mhe. David KIhenzile (Mb) akimwakilisha Waziri wa Uchukuzi amezindua rasmi Mradi wa Huduma za Tahadhari za Hali mbaya ya Hewa (Early Warning for All- EW4ALL), Jijini Dodoma, tarehe 19 Machi 2025.Mradi huo unafadhiliwa na  nchi ya Denmark ukiwa na lengo la kuhakikisha kuwa kila mtu anafikiwa na huduma za tahadhari hivyo kulindwa dhidi ya matukio ya hali mbaya ya hewa ifikapo mwishoni mwaka 2027.

Katika hotuba yake, Mhe. Kihenzile alisema “Uboreshwaji wa huduma za tahadhari dhidi ya hali mbaya ya hewa ni muhimu sana hasa kwa nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania, kwani uchumi wa nchi hizi unajengwa zaidi na sekta za kijamii na kiuchumi zinazotegemea sana hali ya hewa, na kwa kuzingatia athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi ambayo yamesababisha matukio ya hali mbaya ya hewa kuwa ya mara kwa mara na ya hatari zaidi, hivyo kuwepo kwa mradi huu ni tija kwa Taifa letu”.Alisema Mhe. Kihenzile.

Aidha, Mhe. Kihenzile aliongeza kuwa katika kufikia malengo ya mradi nchini, ushirikiano kati ya washirika wote wanaotekeleza mradi huu unahitajika. “Nitoe rai muendelee kuwa na mtazamo wa pamoja na kuhakikisha kuwa shughuli zinazotekelezwa zinafanyika kwa ufanisi ili kufikia matokeo na malengo yaliyokusudiwa. Ni muhimu kuboresha usambazaji wa taarifa za tahadhari kwa njia zenye tija hasa kwa gharama nafuu ili kuhakikisha kuwa watu wote, wakiwemo wanaoishi maeneo ya vijijini, wanafikiwa na taarifa hizi”. Alisisitiza Mhe. Kihenzile.

Mwakilishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Kanali. Selestine Masalamado alisema Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu ina jukumu kubwa la kuratibu masuala mbalimbali katika ngazi ya kitaifa ambapo moja ya majukumu yake ni kuratibu hatua za kukabiliana na majanga mbalimbali yakiwemo majanga yatokanayo na matukio ya hali mbaya ya hewa.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Mwakilishi wa Kudumu wa Shirika la Hali ya Duniani (WMO) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dk.Ladislaus Chang'a alisema Ripoti ya Tathmini ya Sita ya Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC) imeainisha bayana kuwa matukio ya hali mbaya ya hewa ikiwemo Mvua kubwa, Joto kali, Upepo mkali, Mafuriko, Ukame na Vimbunga yameongezeka na yanatarajiwa kuendelea kuongezeka kwa idadi na ukubwa kadri ambavyo joto linaongezeka, na kusababisha majanga makubwa.

Aidha, Dkt. Chang’a aliongezea kuwa “Leo  hii tutatoa ripoti yetu ya tathmini ya hali ya Klaimatolojia kwa mwaka 2024 iliyoandaliwa na TMA na pia wasilisho maalaumu litafanywa katika warsha maalumu itakayofanyika leo na kesho sanjali na uzinduzi huu”.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi alisema WMO itaendelea kushirikiana na TMA pamoja na wadau wengine katika kuhakikisha lengo linafikiwa na kuhakikisha watanzania wote wanafikiwa na huduma za tahadhari za hali mbaya ya hewa.

Balozi wa Denmark alielza kuwa Tanzania ni moja kati ya nchi tano za Afrika ambazo zimechaguliwa kutekelza mradi huu kwa ufadhili wa Denmark, na hii ni kutokana na ushirikiano wa muda mrefu uliopo baina ya Tanzania na Denmark katika masuala ya huduma za hali ya hewa.

Mradi huu unatekelezwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kushirikiana na Washirika wengine katika ngazi ya Kitaifa na ya Kimataifa ambao ni Ofisi ya Waziri Mkuu – Idara ya Usimamizi wa Maafa, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupunguza Hatari za Majanga (UNDRR), Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Shirika la Mawasiliano la Kimataifa (ITU), Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania (TRCS), na Shirikisho la Kimataifa la Msalaba Mwekundu (IFRC).

Monday, March 10, 2025

UWEPO WA KIMBUNGA “JUDE” KATIKA ENEO LA RASI YA MSUMBIJI


 Dar es Salaam, 10 Machi 2025:

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatoa taarifa ya uwepo wa kimbunga “JUDE” katika Bahari ya Hindi eneo la Rasi ya Msumbiji.

Uchambuzi wa mifumo ya hali ya hewa unaonesha kuwa kimbunga hicho kitaingia nchi kavu katika eneo la Msumbiji mchana wa leo tarehe 10 Machi 2025 na kupungua nguvu yake. Hata hivyo, Kimbunga “JUDE” kinatarajiwa kurejea tena baharini na kuimarisha nguvu yake katika kipindi cha kati ya tarehe 13 hadi 15 Machi 2025.

Aidha, kutokana na mwelekeo na umbali wake Kimbunga “JUDE” hakitarajiwi kuwa na athari za moja kwa moja hapa nchini. Hata hivyo, uwepo wa kimbunga hicho katika eneo la Rasi ya Msumbiji unatarajiwa kuchagiza mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na kusababisha ongezeko la mvua katika maeneo mbalimbali. Vilevile, uwepo wa kimbunga hicho unaendana sambamba na kuanza kwa msimu wa mvua za Masika, 2025 katika maeneo yapatayo misimu miwili ya mvua kwa mwaka kama ilivyotabiriwa awali na taarifa kutolewa kwa Umma mnamo tarehe 31 Januari 2025.

USHAURI: Watumiaji wa bahari na jamii kwa ujumla wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam wa kisekta.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga “JUDE” na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila inapobidi.

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...