Dodoma, Tarehe 10 Januari, 2025
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imekutana na wadau kutoka sekta mbalimbali nchini ili kujadili Utabiri wa Mvua za Msimu wa MASIKA 2025. Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa mikutano wa PSSSF, Dodoma tarehe 20 Januari 2025.
Akifungua mkutano huo Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Mhe. Jaji Mshibe Ali Bakari aliwataka wadau kufuatilia na kuzitumia taarifa za hali ya hewa za TMA.kwa kuwa ni sahihi kwa asimia kubwa.
“ Ninawataka wadau wote nchini kufuatilia na kuzitumia ipasavyo taarifa za hali ya hewa za TMA ambazo kwa asilimia kubwa zimekuwa ni sahihi kwa mustakabali wa maslahi mapana ya Taifa letu”
Mhe. Jaji Mshibe aliongelea kuhusu changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa ikihusisha athari mbalimbali zinazoendelea kujitokeza hapa nchini ikiwemo ukame,mvua kubwa,ongezeko la joto ambalo limeathiri shughuli za uvuvi na upatikanaji wa samaki.
Aidha, Mhe.Jaji Mshibe Ally Bakari aliiagiza TMA kuendelea na utaratibu wa kuwakutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali kupitia mikutano hiyo ikiwa ni maandalizi ya mapema kabla ya kutoa utabiri wa hali ya hewa kwa msimu husika.
Awali wakati akimkaribisha mgeni rasmi, Kaimu Mkurugenzi Mkuu, TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wadau wa maendeleo kwa kuendelea na uwekezaji katika miundo mbinu ya hali ya hewa.
“Tunaishukuru Serikali na wadau wa maendeleo kwa kuendelea na uwekezaji katika miundombinu ya hali ya hewa hapa nchini kupitia mpango wa bajeti na programu mbalimbali za maendeleo na kuiwezesha Mamlaka kuongeza usahihi na ubora wa utabiri wa hali ya hewa.
Aidha,Dkt. Chang’a aligusia kuhusiana na ongezeko kubwa la joto duniani lililovunja rekodi kwa ongezeko la nyuzi joto 1.550c ikiwa ni ongezeko kubwa kutokea katika historia ya dunia, japo kwa hapa nchini liliongezeka kwa nyuzi joto 0.70c.