Tuesday, May 22, 2018

NDITIYE AITAKA TMA IJITANGAZE UMUHIMU WAKE KIUCHUMI NA KIJAMII


Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (katikati) akizungumza na Bodi na Menejimenti ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania wakati alipotembelea makao makuu ya mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi hiyo Dkt. Buruhani Nyenzi na kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo Dkt. Hamza Kabelwa
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kwanza kushoto) akipatiwa taarifa ya hali ya hewa kwa usafiri wa anga na Meneja wa Utabiri wa Hali ya Hewa Bwana Samwel Mbuya wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania wakati alipotembelea makao makuu ya mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye ameilekeza Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kujitangaza umuhimu wake katika nyanja ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi na taifa kwa ujumla. Mhandisi Nditiye ameyasema hayo alipotembelea makao makuu ya TMA na kuzungumza na bodi ya Mamlaka hiyo, menejimenti na wafanyakazi kwa lengo la kutambua majukumu yao na kufuatilia utekelezaji wake ili kufikia malengo ya Serikali ya kuwatumikia wananchi. 

Akizungumza na Bodi, menejimenti na wafanyakazi, Mhandisi Nditiye amewaeleza kuwa TMA ni chombo muhimu sana kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya taifa letu na wananchi kwa ujumla kwa kuwa sekta ya usafiri wa anga, majini, ujenzi wa majengo mbalimbali, miundombinu ya barabara na reli, afya, kilimo na mazingira vyote vinategemea taarifa za hali ya hewa kutoka kwenye Mamlaka hii. “Mtambue kuwa hakuna ndege inayoweza kutua wala kuruka bila kupata taarifa kutoka kwenu, vile vile mkandarasi anayejenga reli ya kisasa ya SGR nae anategemea taarifa zenu kwa kiasi kikubwa, hivyo mtambue ninyi ni muhimu na mjitangaze,” amesema Mhandisi Nditiye.

Amesisitiza kuwa ni vema mjitangaze ili wananchi na wadau mbalimbali wafahamu majukumu na umuhimu wa taasisi yenu kwa kuwa uchumi wa taifa hili unategemea taarifa zenu ambapo wananchi wengi wamezoea kusikia na kuwaona mkitoa taarifa za tahadhari za hali ya hewa zinazohusiana na majanga na matukio mengine yanayohusiana na utabiri wenu angali ninyi mna taarifa muhimu zaidi na tofauti na mtazamo wa wananchi walio wengi.

Amefafanua kuwa wananchi wanaziamini taarifa zenu za hali ya hewa kwa kuwa kwa kiasi kikubwa yale mnayotabiri na kuwaeleza ndiyo yanayotokea iwe ni mvua kubwa, upepo mkali au joto kali kama ilivyo sasa. “Nimetembea na kukagua mitambo, vifaa vya kisasa na namna wanavyofanya kazi na nimebaini kuwa taarifa zinazotolewa hapa zimekusanywa kutoka vituo mbali mbali vya hali ya hewa nchini ambapo hapa makao makuu wataalamu wanazichakata, kusambaza kwa wahusika na kuhifadhiwa, na zinaonesha kuwa ni taarifa za uhakika kwa kiwango cha asilimia 87.5 ambapo imeongezeka kutoka asilimia 82.1 kwa miaka mitatu iliyopita,” amesema Mhandisi Nditiye.

Mwenyekiti wa Bodi ya TMA Dkt. Buruhani Nyenzi wakati akiwasilisha taarifa yake kwa Mhandisi Nditiye amesema kuwa Mamlaka hii ni muhimu kwa ustawi na maendeleo ya taifa letu na wananchi kwa ujumla kwa kuwa utoaji wa taarifa na huduma za hali ya hewa nchini zimewezesha uokoaji wa maisha ya watu na mali zao; kuepuka au kupunguza athari na hasara zinazosababishwa na matukio ya hali ya hewa; kuongeza tija na mafanikio katika shughuli za kiuchumi kama vile kilimo, ufugaji, uvuvi; kuwa na miundombinu imara kama vile barabara, madaraja; kuongeza ufanisi katika sekta za usafiri na mawasiliano; kuchangia katika sekta za ujenzi na uendeshaji wa viwanda nchini na kukuza pato la taifa. 

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt. Hamza Kabelwa amemueleza Mhandisi Nditiye kuwa wahitaji wa taarifa za hali ya hewa kutoka kwa taasisi na wadau mbalimbali ambao wanahitaji kwa ajili ya kutekeleza shughuli za kiuchumi na kijamii wamekuwa wengi na teknolojia ya utabiri wa hali ya hewa na utoaji wa taarifa zake umebadilika ambapo inatulazimu kuhuisha Sheria Na. 6 ya Hali ya Hewa ya Mwaka 1978 na kukamilisha Sera ya Taifa ya Hali ya Hewa ili ziweze kwenda na wakati pamoja na kuboresha chuo cha Hali ya Hewa Kigoma kwa kuwa ndio chuo pekee nchini kinachotoa elimu ya awali na ya kati ya hali ya hewa.

Ameongeza kuwa TMA imepatiwa cheti cha ubora wa utoaji huduma na Shirika la Viwango la Kimataifa (ISO) kwa kutoa huduma kwa sekta ya anga nchini. Pia, inashirikiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa jangwa la Afrika (SADC), Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO) na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) kwa kubadilishana taarifa za hali ya hewa, mabadiliko ya hali ya hewa yanayohitaji ushirikiano wa kimataifa, na kuendeleza na kutunza mtandao wa vituo vya uangazi wa hali ya hewa ili kukidhi makubaliano ya kimataifa ya kubadilishana taarifa hizo. 

Dkt. Nyenzi amemshukuru Mhandisi Nditiye na kumueleza kuwa TMA inafarijika kusikia kuwa anafahamu kwa undani umuhimu wa utabiri wa hali ya hewa nchini, hivyo ni imani yake kuwa ataisamimia vema ili ifikie malengo.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano



Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...