Dar es Salaam, Tarehe 31 Oktoba, 2024
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi utabiri wa mvua za msimu kwa maeneo yanayopata mvua mara moja kwa mwaka. Maeneo hayo ni mikoa ya Kigoma, Katavi, Singida, Dodoma, Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe, Lindi, Mtwara, Ruvuma na Kusini mwa Morogoro katika kipindi cha miezi ya Novemba, 2024 hadi Aprili, 2025.
Akitoa utabiri huo kwa vyombo vya habari katika ukumbi wa Ubungo Plaza, Kaimu Mkurugenzi Mkuu, TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a alisema mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa katika maeneo ya mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Songwe, Singida na Dodoma; kaskazini na mashariki mwa mkoa wa Lindi, na kaskazini mwa mikoa ya Mbeya na Iringa. Aidha, mvua za Wastani hadi Juu ya wastani zinatarajiwa katika mikoa ya Njombe, Ruvuma, Mtwara, maeneo ya kusini na magharibi mwa mkoa wa Lindi, kusini mwa mikoa ya Mbeya, Iringa na Morogoro.
“Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Oktoba, 2024 katika mkoa wa Kigoma na kusambaa katika maeneo mengine yanayopata mvua za Msimu mwezi Novemba, 2024 na mwisho katika mkoa wa Ruvuma Disemba, 2024. Kipindi cha nusu ya pili ya msimu (Februari – Aprili, 2025) kinatarajiwa kuwa na mvua nyingi ikilinganishwa na nusu ya kwanza (Novemba, 2024 – Januari, 2025)”. Alifafanua Dkt. Chang’a.
“Vipindi vifupi vya mvua kubwa vinatarajiwa kujitokeza hata katika meneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani”.Aliongeza Dkt. Chang’a
Aidha, Dkt. Chang’a alisema, Mamlaka imeendelea kuandaa utabiri wa maeneo madogo madogo, ambapo kwa msimu huu jumla ya wilaya zote 63 zimeandliwa utabiri wake. Lengo la Mamlaka ni kuendelea kuboresha huduma zake kwa wadau ili kuchochea na kuimarisha mchango na matumizi ya taarifa za hali ya hewa katika kuongeza tija na ufanisi kwenye shughuli za kiuchumi na kijamii
Akieleza athari zinazoweza kujitokeza, Dkt. Chang’a alisema vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi pamoja na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao na miundombinu ya kilimo, hususan katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani, kina cha maji katika mito na mabwawa kinatarajiwa kuongezeka, hali inayoweza kusababisha mafuriko, hasa katika maeneo yanayoathiriwa na mafuriko.