Hali
ya kupatwa kwa jua ni tukio la aina yake linatokea pale ambapo miali ya jua
hupungua hadi kutoonekana tena na kusababisha sehemu ya uso wa dunia kuwa giza
wakati wa mchana. Muda wa kufunikwa kabisa ni dakika chache tu katika eneo husika.
Kupatwa
kwa jua kunatokea wakati dunia, mwezi na jua vinapokaa kwenye mstari mmoja
mnyoofu wakati mwezi unakuwa kati ya dunia na jua. Hali hiyo inapotokea
kunajengeka kivuli cha mwezi kwenye uso wa dunia. Kivuli hicho hufunika
sehemu tu ya uso wa dunia. Kutokana na hali hiyo kupatwa
kwa jua kwa maeneo yaliyo mengi kunaonekana kwa watu wengi kama kupungua kwa
mwanga wa jua.
2.Maelezo ya Kisayansi
Wanasayansi
wanaelezea kupatwa kwa jua kama tukio linalotokea na kuonekana katika namna
tofauti tofauti mfano; ni kupatwa kwa
jua kikamilifu hali ambayo hutokea pale miali ya jua inapotea kabisa katika
eneo husika kwa kipindi kifupi. Hali hii inapotokea eneo husika linakosa kabisa
mwanga wa jua na kuwa giza.
Aina ya
pili ni kupatwa kwa jua kisehemu; hii hutokea wakati eneo kubwa linapopata upungufu
wa mwanga wa jua hali ambayo hupungua kadiri mtu anavyokuwa mbali na kitovu cha
mstari wa kupatwa kwa jua. Kiwango cha upungufu wa mwanga wa jua hutegemea
umbali mtu alipo kutoka kwenye kitovu cha kivuli kamili.
Aina
nyingine ni kupatwa kwa jua kipete;
hali hii inapotokea mwezi huzuia mwanga wa jua kufika kwenye dunia kwa vile huweka
duara la kivuli cha mwezi kwenye dunia na hivyo mwanga wa jua huonekana kama pete. Inatarajiwa kuwa aina
hii ya kupatwa kwa jua ndiyo itakayojitokeza
tarehe 1 Septemba 2016 katika baadhi ya maeneo ya Bara la Afrika. Kwa
hapa nchini hali hiyo inatarajiwa kujitokeza katika sehemu kubwa ya maeneo ya mikoa
ya Nyanda za juu kusini magharibi na maeneo ya kusini mwa nchi. Hata hivyo,
watu katika maeneo mengine ya nchi yaliyokaribu na ukanda huo wanatarajiwa kuona kupatwa kwa jua kisehemu yaani upungufu wa
mwanga wa jua kwa dakika kadhaa, imetabiriwa takriban kakika tatu (3). Jua linatarajiwa kupatwa wakati wa asubuhi
kati ya saa tatu asubuhi na saa sita.
3. Athari zake kwa Hali ya Hewa.
Kwa
ujumla hakuna athari zozote kubwa zinazotarajiwa kutokana na hali hiyo. Hata hivyo, upo uwezekano wa kupungua kwa
viwango vya joto katika maeneo ambapo kupatwa kwa jua Kipete kutajitokeza. Kwa kuwa tukio hilo la kupatwa kwa jua
huchukua muda wa dakika chache tu hali ya joto itapungua kwa haraka katika
kipindi kifupi na baadae kuongezeka kurudi katika hali yake ya kawaida. Viwango
vya kupungua kwa joto vitatofautiana kulingana na umbali kutoka eneo la kupatwa
kwa jua
4. Upekee wa tukio la kupatwa kwa jua
Tukio
hili hutokea au kujirudia mara chache sana katika eneo husika. Inakadiriwa kuwa
inaweza kuchukua kati ya miaka 350 hadi 400 kwa hali hiyo kujitokeza tena
katika eneo litakapotokea mwaka huu 2016. Hii ndio sababu kwa watu wa eneo
husika na wanasayansi hili ni tukio la
muhimu na kumbukumbu muhimu ya maisha.
Mamlaka ya hali ya hewa inaendelea
kufuatilia na itatoa taarifa za mabadiliko yoyote yanayoweza kujitokeza katika
hali ya hewa kulingana na tukio hili la kupatwa kwa jua.
Dk. Agnes L. Kijazi
MKURUGENZI MKUU
No comments:
Post a Comment