Sunday, December 20, 2015

MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA (TMA) YAZINDUA MFUMO WA UBORESHAJI WA HUDUMA ZA HALI YA HEWA NCHINI










 

Mamlaka ha Hali ya Hewa Tanzania kwa kushirikiana na kituo cha kimataifa cha utafiti kilichoko Marekani “International Research Institute (IRI) imezindua mfumo utakao wawezesha watumiaji wa huduma za hali ya hewa kupata huduma  hizo kwa urahisi kupitia tovuti ya Mamlaka (www.meteo.go.tz).

Akizindua mfumo huo Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Mamlaka Dkt. Buruhani Nyenzi aliitaka Mamlaka ya Hali ya Hewa kuongeza ufanisi katika  utoaji wa huduma za hali ya hewa.

Aidha, Dkt Nyenzi aliipongeza  Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa jitihada zake za kushirikiana na wataalam kutoka nchi mbalimbali ambazo ni wanachama wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani katika kuboresha huduma za hali ya hewa hapa nchini.  Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Ushauri ya TMA alikishukuru kituo cha kimataifa cha utafiti kilichoko Marekani (IRI) kwa msaada waliotoa hata kuiwezesha TMA kukamilisha mfumo huo na kufikia hatua ya kuzinduliwa rasmi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi alitoa msisitizo kwa wadau kuzingatia matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa ili kuongeza tija na ufanisi katika shughuli za kiuchumi na kijamii na pia kuweza kukabiliana na majanga yatokanayo na hali mbaya ya hewa. Dkt. Kijazi aliwashukuru kituo cha kimataifa cha utafiti (IRI) kutoka Marekani kwa kushirikiana na TMA kwa kipindi cha miaka mitatu katika kuandaa mfumo huo. Vilevile aliwashukuru wadhamini wa uzinduzi wa mfumo huo ambao ni DFID kupitia chuo kikuu cha Columbia kilichoko Marekani.

Uzinduzi huo ulifanyika katika Ukumbi wa Blue pearl tarehe 18 Desemba 2015 nakushirikisha wadau mbalimbali kutoka Wizara na Taasisi za Serikali pamoja na asasi za kiraia.


IMETOLEWA NA: MONICA MUTONI, AFISA UHUSIANO, MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA.

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...