Monday, June 18, 2018

MAADHIMISHO YA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA MWAKA 2018


Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inawaalika wadau wake wote kutembelea ofisi za hali ya hewa ambazo ziko nchini kote kati ya tarehe 20-22 Juni 2018 ili kutoa maoni na ushauri kuhusu uboreshaji wa huduma za hali ya hewa zitolewazo na Mamlaka.

Kwa Makao Makuu ya Mamlaka iliyopo Ubungo Plaza, Barabara ya Morogoro, Mamlaka itakutana na wadau tarehe 21/06/2018 kati ya saa 3.30 asubuhi hadi saa 9.00 mchana, ghorofa ya tatu chumba namba 309. Aidha, unaweza kuwasilisha kero na maoni kwa siku zote za maadhimisho kupitia barua pepe met@meteo.go.tz na ofisi za kanda zifuatazo:
Kanda ya Mashariki: Kituo cha Hali ya Hewa, Morogoro, Simu: 023-2603794
Kanda ya Ziwa: Kituo cha Hali ya Hewa, Mwanza, Simu: 028-2505338
Kanda ya Kati: Kituo cha Hali ya Hewa, Dodoma, Simu: 026-2351594
Kanda ya Kusini: Kituo cha Hali ya Hewa, Mtwara, Simu: 023-2333847
Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi : Kituo cha Hali ya Hewa, Mbeya, Simu: 025-2503096
Kanda za Nyanda za Juu Kaskazini-mashariki: Kituo cha Hali ya Hewa, KIA, Simu: 0272554224
Kanda ya Magharibi: Kituo cha Hali ya Hewa, Tabora, Simu: 026-2604258
Ofisi ya Hali ya Hewa Zanzibar, Simu: 024-2231958
Ofisi ya Hali ya Hewa, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa, JNIA, Simu: 022-2110290

Kwa taarifa zaidi wasiliana na Ofisi ya hali ya hewa iliyopo karibu nawe au Ofisi ya Masoko na Uhusiano wa Umma kwa namba +255 22 2460706-8. Kauli mbiu: Kuimarisha Ushirikishwaji wa Jamii katika utoaji Huduma:Vijana washirikishwe kuleta mabadiliko barani Afrika. Imetolewa na: Mkurugenzi Mkuu MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA S.L.P. 3056 DAR ES SALAAM Simu: 255 22 2460706-8 Faksi: 255 22 2460735/2460700 Barua pepe: met@meteo.go.tz Tovuti: www.meteo.go.tz

Thursday, June 14, 2018

TMA YATOA MWELEKEO WA HALI YA HEWA NCHINI KWA KIPINDI CHA MWEZI JUNI – AGOSTI (JJA), 2018Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imetoa mwelekeo wa hali ya hewa nchini kwa kipindi cha mwezi Juni hadi Agosti mwaka 2018. Taarifa hiyo imetoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa, joto, upepo na mvua, ushauri na tahadhari kwa wadau wa sekta mbalimbali wanaotumia taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao.

Mamlaka imeeleza kuwa uwepo kwa hali ya joto la wastani hadi chini ya wastani inatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi. Hata hivyo, hali ya baridi inatarajiwa katika maeneo ya miinuko ya nyanda za juu Kaskazini mashariki (Arusha, Kilimanjaro na Manyara), Nyanda za juu kusini Magharibi (hususani mkoa wa Njombe) pamoja na maeneo ya miinuko ya mkoa wa Tanga (hususan wilaya za Lushoto na Bumbuli).

Kuhusu hali ya mvua na upepo taarifa hiyo imeeleza kuwa maeneo mengi yanatarajiwa kuwa makavu kwa ujumla,pamoja na vipindi vifupi vya upepo mkali vinatarajiwa kujitokeza katika baadhi ya maeneo. Aidha, vipindi vya mvua za nje ya msimu vinatarajiwa katika maeneo ya pwani hususan katika wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Juni, 2018 na vipindi kadhaa kwa mwezi Julai, 2018.

Wananchi wameendelea kushauriwa  kufuatilia taarifa za hali ya hewa ili kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kama vile hali ya baridi inayotarajiwa katika maeneo mengi ya nchi hususan maeneo ya miinuko nakuweza kusababisha kudumaa kwa mazao kama vile ndizi pamoja na mazao ya nje ya msimu, na kuathiri mifugo. Vile vile, kutokana na hali ya joto katika bahari ya Hindi kuwa juu ya wastani kiasi, ongezeko la siku zenye tija katika shughuli za uvuvi katika kipindi cha msimu wa JJA zinatarajiwa.

 Kwa taarifa zaidi tembelea: http://www.meteo.go.tz/news/135

Wednesday, June 13, 2018

MAMLAKA YA HALI YA HEWA SIERRA LEONE YAFANYA ZIARA YA MAFUNZO KATIKA OFISI ZA MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA

Ujumbe kutoka Sierra Leone katika ukumbi wa mkutano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano walipokutana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Uchuuzi)  Dkt. Leonard Chamuriho, wajumbe hao waliambatana na wenyeji wao kutoka TMA wakati wa  ziara yao ya mafunzo


Kaimu Mkurugenzi Mkuu-TMA, Dkt. Pascal Waniha akifafanua jambo kwa ujumbe kutoka Sierra Leone, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Bw. Usman Banya (Tai ya Bluu), Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Sierra Leone Bw. Ibrahim S. Kamara na Bw. Moses Baiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Sierra Leone wakati walipokutana na menejiment ya TMA katika ziara yao ya mafunzo.
 
Ujumbe kutoka Sierra Leone katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) Bw. Hamza Johari walipomtembelea katika ofisi yake wajumbe hao waliambatana na wenyeji wao kutoka TMA wakati wa  ziara yao ya mafunzo
 
Ujumbe kutoka Sierra Leone  wakipata maelezo ya uandaaji wa utabiri kutoka kwa Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri, Dkt. Hamza Kabelwa wakati wa  ziara yao ya mafunzo
Ujumbe kutoka Sierra Leone wakipata maelezo ya uandaaji wa taarifa za hali ya hewa hatarishi (severe weather) kutoka kwa mtaalam wa hali ya hewa Bw. Abuubakari wakati wa  ziara yao ya mafunzo
 
 
 
Ujumbe kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Sierra Leone umefanya ziara katika ofisi za TMA, lengo likiwa ni kujifunza namna bora ya utoaji huduma za hali ya hewa kwa jamii ili kuboresha huduma zao. Ujumbe huo uliambatana na  Katibu Mkuu wa Wizara ya uchukuzi anayesimamia huduma za hali  ya hewa nchini Sierra Leone, Mkurugenzi Mkuu kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Sierra Leone na wajumbe wengine wa nne kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga, kitengo cha Maafa na kitengo cha huduma za maji. Wajumbe walipata fursa ya kuonana na Katibu Mkuu wa Uchukuzi na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania.
 

Thursday, June 7, 2018

MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA YATEMBELEWA NA WANAFUNZI KUTOKA MAREKANI KWA MWALIKO WA UNDP.

 

Wanafunzi kutoka Marekani kwa mwaliko wa UNDP wametembelea ofisi za TMA kujionea shughuli mbalimbali za TMA na utekelezaji wa mradi wa kuboresha huduma za hali ya hewa unaosimamiwa na UNDP.
Picha hii imechukuliwa katika studio ya TMA zinazotumika kurekodi utabiri wa hali ya hewa wa kila siku.

MAKALA: MAZINGIRA NA HALI YA HEWA


Na Monica Mutoni


WAKATI huu ambapo tunaadhimisha wiki ya mazingira ni vyema tukakumbuka tulikotoka, wakati wazee wetu wakitumia busara zao kutushauri kutunza mazingira ili yatutunze.

Moja ya msisitizo wao ulikuwa ni pamoja na kutuaminisha kwamba utunzaji wa mazingira ni kupanda miti, lakini umefika wakati na sisi tujiulize kupanda miti ndio utunzaji wenyewe wa mazingira?

Kwa mujibu wa wataalamu wa mazingira, ushauri wa wazee juu ya kupanda miti ni sahihi kabisa, nadharia ambayo pia inaungwa mkono na wataalamu wa hali ya hewa kote duniani ambao wanaamini maeneo yenye misitu mizito, ndiko kunapokuwa na mvua nyingi zaidi.

Wataalam hao wanatolea mfano wa misitu mikubwa duniani ikiwemo misitu ya Congo ambapo wanasema pamoja na kupata mvua nyingi maeneo hayo  yanakuwa na hewa safi kulinganisha na maeneo ambayo hayana misitu kwani miti ina tabia ya kuondoa hewa chafu kwenye anga na kuongeza hewa safi.

Kwa maana hiyo, kama waaminivyo wataalamu hatuna budi kufahamu kuwa kuna uhusiano mkubwa kati ya mazingira kwa maana ya uwepo wa misitu na mabadiliko ya hali ya hewa.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ni taasisi inayoshughulikia masuala ya hali ya hewa nchini na kuiwakilisha nchi kikanda na Kimataifa. Taasisi hii imepewa jukumu la kutoa huduma za hali ya hewa kupitia sheria ya hali ya hewa Na. 6 ya mwaka 1977. Mamlaka hii pia hutoa tahadhari ya hali mbaya ya hewa kila inapotarajiwa kuwepo na huwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kutumia taarifa za hali ya hewa.

Kwa kuzingatia  matumizi sahihi ya huduma za hali ya hewa tutaweza kupunguza athari za uharibifu wa mazingira.

TMA inasema takwimu za hali ya hewa zilizokusanywa kwa kipindi cha miongo kadhaa iliyopita zinaonesha dhahiri kuwa uharibifu wa mazingira umechangia kwa kiasi kikubwa kusababisha mabadiliko ya hali ya hewa nchini na duniani kwa ujumla. 

Mfano mkubwa wa viashirikia hivyo ni kuongezeka kwa joto na kupungua kwa mvua  katika maeneo mbalimbali nchini  kama ilivyooneshwa kwenye mwenendo wa mvua wa kitaalamu katika vielelezo vya maeneo mbalimbali nchini.

Kwa vielelezo hivi, ni wazi kuwa joto limeendelea  kuongezeka miaka ya karibuni katika  mkoa wa Dar es Salaam na Kilimanjaro ukilinganisha na miaka iliyopita.
Aidha, kiwango cha mvua kinapungua kwa kiasi fulani ukilinganisha na miaka ya nyuma kama inavyoonekana kwa mkoa wa Kilimanjaro.

Picha Na. 1:  Kupungua kwa mvua katika mkoa wa Kilimanjaro


Picha Na;2: Ongezeko la joto kwa mkoa wa Kilimanjaro kuanzia mwaka 1972 hadi 2016

Picha Na. 3: Ongezeko la joto kwa mkoa wa Dar es salaam kuanzia mwaka 1953-2015
Hata hivyo, pamoja na kupungua kwa mvua, kumekuwa pia na vipindi vifupi vya  vya mvua kubwa zenye athari kwa watu na mali zao.

Wanasayansi ya hali ya hewa wanasema kuwa uharibifu wa mazingira unaosababisha mabadiliko ya hali ya hewa umeleta changamoto kubwa kwenye kuandaa utabiri wa hali ya hewa kwani hata vile viashiria vya awali vinapotea.

Utafiti uliofanywa na Mamlaka ya Hali ya Hewa katika baadhi ya maeneo hapa nchini unaonyesha kuwa viashiria vinavyotumiwa  na wazee wa jadi kufanya utabiri wa msimu wa mvua vinapotea kutokana na uharibifu wa mazingira. Viashiria hivyo ni pamoja na uwepo wa wadudu, ndege, mimea na vinginevyo. Viashiria vinavyotumiwa na wazee wa jadi vimeonekana vikishabihiana kwa kiasi kikubwa na sayansi na hivyo kuwepo maelezo ya kisayansi kuhusu utabiri wa jadi.

Picha Na. 4: Eneo la jangwani likiwa limezungukwa na maji yaliyotokana na vipindi vifupi za mvua kubwa katika msimu wa mvua za VULI 2017

Ni vyema tukatambua umuhimu wa kutumia taarifa za hali ya hewa hasa zile zilizoandaliwa na wanasayansi wa hali ya hewa, kwa maana ya TMA kwa kuwa kutokana na kuongezeka kwa vifaa vya hali ya hewa, mafunzo kwa watumishi na kujitoa kwao kufanya kazi kwa bidii wamefanikiwa kuboresha utabiri unaotolewa kwa kiasi kikubwa.

TMA hutoa taarifa, ushauri na takwimu ili kumwezesha mwekezaji kuwekeza aina ya nishati katika eneo husika ili kuepuka uharibifu wa mazingira mfano wa taarifa hizo ni kasi na mwelekeo wa upepo, nguvu ya upepo, vipindi vya jua na hali ya mawingu.

Takwimu za upepo kutoka vituo vya hali ya hewa nchi nzima zinaweza kusaidia uwekezaji wa faida wa nishati ya umeme inayozalishwa kwa kutumia upepo ambayo ni nishati mbadala , nishati hii itasaidia kupunguza matumizi ya mkaa nchini, nishati hii pia ni rafiki wa mazingira. Ni vyema ukajua takwimu za hali ya hewa zinasemaje ili kuwekeza kwa faida, mfano mikoa wa Singida, Dodoma n.k

Kwa upande wa takwimu za jua, ambazo zinapatikana katika vituo vya TMA nchi nzima, zitasaidia maamuzi sahihi katika miradi mikubwa ya uwekezaji wa nishati ya jua, kama inavyoonekana kuenea nchini kwa sasa, hii pia ni nishati mbadala na rafiki kwa mazingira yetu.

Takwimu za mvua zinazopatikana katika vituo vya TMA nchi nzima, zitasaidia kutoa muongozo na maamuzi ya kuongeza uwekezaji katika nishati inayozalishwa kutokana na nguvu za maji katika maeneo mbalimbali nchini, hata kujipanga kwa kuweka mbadala pindi unapotambua kiasi cha maji kinachopatikana kwa kipindi husika
Takwimu za mawimbi na upepo wa bahari zitasaidia katika tafiti mbali mbali za  uwekezaji katika eneo la mafuta na gesi ambayo pia ni nishati mbadala na rafiki kwa mazingira.
Sote tunatambua mchango wa TMA katika kutoa huduma za hali ya hewa nchini, tumeshuhudia utabiri na tahadhari za mara kwa mara zikitolewa hivyo kupunguza athari zake.

Hapo nyuma ilikuwa si rahisi kutabiri hali ya hewa na kutambua mabadiliko ya hali ya hewa kwa kipindi kirefu kama vile wiki au mwezi kuachilia mbali utabiri wa mvua za msimu, lakini kutokana na maboresho makubwa ya vifaa vya kiteknolojia watabiri wengi wameongezewa ufanisi.

Shime kwa jamii na Mamlaka husika kutumia huduma za TMA ili kuweza kuwekeza katika njia mbadala za kuiondoa nchi kwenye janga la uharibifu wa mazingira.

Kwa hitimisho, ni dhahiri huwezi kutenganisha mazingira na hali ya hewa. Ukubali, ukatae taarifa za hali ya hewa ni mtambuka kama maji waswahili wanavyosema, maji usipoyanywa utayaoga hivyo pale penye fursa ya kuzipata ng'ang'ania kwa sababu teknolojia ipo imetuwezesha kuzipata tena kwa usahihi wake.

Namalizia kwa kuwaza tu kwa sauti
Kama akitokea mtu wa kuhoji, “kama kupanda miti ndio kupata mvua au hewa safi, mbona Dodoma hakuna miti mingi lakini kuna mvua na ikifika jioni hali ya hewa ni baridi?” Lipi litakuwa jibu lako kwake? Usikose kufuatilia makala hizi ili kujifunza zaidi
Picha Na. 5: Wafanyakazi wa TMA wakishiriki katika zoezi la kupanda miti wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu Dkt. Agnes Kijazi