Saturday, May 24, 2025

SULUHU MGAWANYO WA MAPATO WA HUDUMA ZA USAFIRI WA ANGA NCHINI YAPATIKANA.

 









Dar es Salaam; Tarehe 23 Mei 2025;

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) pamoja na Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) wafanikisha upatikanaji wa suluhu ya mgawanyo wa mapato yatokanayo na huduma za usafiri wa anga nchini.

Suluhu hiyo imepatikana kupitia kusainiwa kwa mkataba wa makubaliano ya pamoja baina ya wakuu wa taasis hizo katika ukumbi wa mikutano wa TAA uliopo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, tarehe 23 Mei 2025.

Mkataba huo unafuatia kuundwa kwa mfumo wa kielektroniki (Ankara Jumuishi) utakaosaidia kuimarisha uwazi, ufanisi na tija katika mgawanyo wa mapato yatakayokuwa yamekusanywa kwa kuingizwa moja kwa moja kwenye taasis husika kulingana na asilimia zilizokubalika. Mfumo unatarajiwa kuanza kutumika kuanzia tarehe 1 Julai 2025.

Wakizungumza katika zoezi la utiaji saini, Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Abdul Mombokaleo alieleza kuwa mfumo huo wa kielektroniki utarahisisha mgawanyo wa mapato na kuwezesha kila taasis kupata mgao wake kwa wakati ili kusukuma gurudumu la maendeleo ya nchi yetu. Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a aliwashukuru viongozi wenzake kwa kufanikisha kukamilika kwa mfumo huo na kusisitiza kuwa mfumo huo utachangia sana kuongeza tija na ufanisi katika utendaji kwa kupunguza muda na nguvu kubwa iliyokuwa inatumika kufuatilia mapato yatokanayo na huduma zitolewazo na kila taasis

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Mhandisi Peter Ulanga alipongeza muitikio kutoka pande zote wa kutekeleza maelekezo ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanya mifumo ya taasis za serikali kusomana, naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Bw. Daniel Malanga alipongeza hatua iliyofikiwa sababu itaboresha utoaji huduma ndani ya viwanja vya ndege nchini.




TMA NA CRDB ZAWANOA MAAFISA UGANI MBEYA, NJOMBE, IRINGA NA SONGWE








Wataalamu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) kwa kushirikiana na Benki ya CRDB kupitia mradi wa Tanzania Agriculture Climate Adaptation Technology Deployment Project (TACATDP) wamewajengea uwezo Maafisa Ugani wa namna bora ya kutafsiri na kutumia taarifa za hali ya hewa hususani katika shughuli za kilimo.

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo Meneja wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi (TMA) Bw. Elias Elipiki, alisema mafunzo hayo yanawalenga Maafisa Ugani kwani wao ni daraja kati ya TMA na wakulima, hivyo mafunzo haya yanalenga kutoa elimu  ya namna sahihi ya kutafsiri taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka na kuwawezesha wakulima kufanya mipango sahihi juu ya shughuli za kilimo kwa msimu husika.

Aidha, Meneja Uhusiano kutoka CRDB ambaye pia ni msimamizi wa utoaji wa mikopo inayozingatiwa uhifadhi wa mazingira katika mradi wa (TACATDP) Bw. Karim Kindole,  alisema CRDB na TMA wana ushirikiano katika kuwajengea uwezo Maafisa Ugani namna ya kudhibiti na kuwasaidia wakulima kupata taarifa sahihi za mabadiliko ya hali ya hewa.

Naye, Afisa Kilimo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali Bw. Sostenesi Silayo, aliwashukuru TMA na CRDB kwa kuwapa nafasi Maafisa Ugani kupata elimu ambayo wataitumia katika kuwashauri wakulima kulima kilimo sahihi kutokana na hali ya hewa husika na kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao mengi.

Thursday, May 22, 2025

TMA YATOA RASMI UTABIRI WA MSIMU WA KIPUPWE 2025.

 




Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi mwelekeo wa hali ya hewa kwa msimu wa Kipupwe unaoanzia Mwezi Juni hadi Agosti (JJA) 2025. Katika taarifa hiyo imeelezea mwelekeo wa hali ya joto na upepo unatarajiwa kujitokeza na kutoa ushauri kwa sekta mbalimbali juu ya hatua za kuchukua katika kukabiliana na matarajio hayo.

 

Akizungumza na waandishi wa habari Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a alieleza kuwa vipindi vya baridi kali vinatarajiwa kujitokeza mwezi Julai katika baadhi ya maeneo na hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi, aliendelea kusema kuwa upepo wa wastani unatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi huku vipindi vifupi vya upepo mkali vikitarajiwa katika maeneo ya ukanda wa pwani ya bahari ya Hindi kwa kipindi cha miezi ya Juni na Julai 2025.

 

Hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi. Hata hivyo, hali ya baridi ya wastani hadi baridi kali inatarajiwa katika maeneo ya mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Singida pamoja na maeneo ya magharibi mwa mkoa wa Dodoma. Vipindi vya baridi zaidi vinatarajiwa kujitokeza katika mwezi Julai huku vipindi vya mvua za nje ya msimu vikitarajiwa katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria, ukanda wa mwambao wa pwani pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.’ Alizungumza Dkt. Chang’a

 

’Aidha, napenda kuwajulisha kuwa Msimu wa Kipupwe 2025 unatarajiwa kutawaliwa na upepo wa wastani utakaovuma kutoka Kusini Mashariki kwa maeneo mengi ya nchi, na vipindi vichache vya upepo mkali utakaovuma kutoka kusini (upepo wa kusi) hususan katika kipindi cha miezi ya Juni na Julai 2025 katika maeneo ya ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi na maeneo ya nchi kavu’ Alifafanuo Dkt. Chang’a.

 

Akitoa ushauri kwa sekta mbalimbali hapa nchini, Dkt. Chang’a alisema tahadhari za kiafya zinapaswa kuchukuliwa ili kulinda jamii dhidi ya magonjwa yanayoweza kusababishwa na baridi au vumbi, kwa wafugaji wanashauriwa kutumia maji na malisho kwa uangalifu, wakulima wakishauriwa kulima mbogamboga na mazao ya mizizi katika maeneo yenye unyevu au kwa maeneo yanayotarajiwa kupata vipindi vya mvua katika kipindi cha msimu wa Kipupwe. Kwa watumaiji wa bahari wanashauriwa kuendelea kufuatilia taarifa za hali ya hewa za kila siku kwa kuzingatia tahadhari na angalizo za hali mbaya ya hewa zitakazotolewa na Mamlaka, huku sekta ya madini, ujenzi na uchukuzi zikitarajiwa kunufaika zaidi na hali inayotarajiwa.

 

Kwa taarifa zaidi tembelea: https://www.meteo.go.tz/publications/single/575

 

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...