Tuesday, April 22, 2025
WATAALAMU KUTOKA OFISI ZA UMOJA WA AFRIKA (AUC) WATEMBELEA TMA.
Tuesday, April 15, 2025
TMA YAPONGEZWA KWA UBORESHWAJI WA TAARIFA ZA HALI YA HEWA
Morogoro, Tarehe 15/04/2025
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imepongezwa kwa uboreshwaji wa utabiri wa hali ya hewa na taarifa za tahadhari za matukio ya hali mbaya ya hewa nchini. Hayo yamesemwa na Mhe. Dkt. Rozalia Rwegasira, Kaimu Katibu Tawala Mkoa, sehemu ya uchumi na uzalishaji wa mkoa wa Morogoro wakati wa ufunguzi wa Semina ya Mradi wa Kuimarisha Uwezo wa Jamii Kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Hali ya Hewa na matukio ya Hali Mbaya ya Hewa, kwaajili ya Kupunguza Hasara na Uharibifu ,iliyofanyika mkoani Morogoro katika ukumbi wa NSSF, tarehe 15/4/2025.
“Utabiri wa hali ya hewa umeendelea kuboreshwa na tahadhari za mvua kubwa na matukio ya hali mbaya ya hewa zinatolewa kwa wakati na hivyo kuchangia kuokoa maisha ya watu na mali zao. Tunaishukuru na kuipongeza serikali kwa kupitia TMA kwa kazi hii njema”. Alisema Dkt. Rozalia.
Aidha, Dkt. Rozalia alitoa ahadi ya kushirikiana na TMA katika kufanikisha utekelezwaji wa mradi huu kwani utakuwa na faida kubwa na chanya kwa wananchi wa Tanzania.
“Katika kufanikisha utekelezaji wa Mradi huu, kwa niaba ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa tuanaahidi kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha kwamba wananchi wananufaika na taarifa zitakazozalishwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kupitia Mradi huu, ili wadau na wananchi kwa ujumla kuweza kuchukua tahadhari kwa lengo la kupunguza athari zitokanazo na matukio ya hali mbaya ya hewa”.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA ambaye ni Mwakilishi wa Kudumu wa Shirika la Hali ya Duniani (WMO) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang'a aliishukuru Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuwekeza kwenye sekta ya hali ya hewa nchini.
“Nitumie fursa hii kutoa shukurani zangu za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuwekeza na kuisaidia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania katika kuimarisha huduma za hali ya hewa nchini kwa kuweka sera, mikakati na mazingira wezeshi yanachochea ubunifu na umahiri".
Dkt. Chang’a alisisitiza kwamba uwekezaji wa serikali kwenye miundombinu ya hali ya hewa nchini ndio chanzo kikuu cha uboreshwaji wa taarifa za hali ya hewa nchini na kuwasisitiza wananchi kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri na tahadhari zinazotolewa na TMA, na pia kuzingatia sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa namba 2 ya mwaka 2019 na kanuni zake.
Mamlaka ya Hali ya Hewa inatoa shukrani za dhati kwa Tume ya sayansi na teknolojia (COSTECH) kwa kufadhili mradi huu muhimu ambao utaongeza ufanisi katika mchakato wa kukabiliana na mabadiliako ya hali ya hewa na tabianchi nchini.
Tuesday, April 1, 2025
WATAALAMU WAJADILI MCHANGO WAO KATIKA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA HALI YA HEWA NA TABIANCHI
Wataalamu Wabobezi katika sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi wamekutana jijini Arusha katika kongamano la siku moja kwa lengo la kujadili mchango wao katika kukabiliana na mabadiliko hayo, tarehe 31 Machi 2025.
Kongamano hilo limeandaliwa mahsusi kwa ajili ya kuongeza uelewa kuhusu shughuli za Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC); Ripoti zitakazoandaliwa katika mzunguko wa saba wa IPCC (AR7) kuhusu tathmini ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi na fursa za kushiriki katika mchakato huo, ikijumuisha uandishi, uteuzi wa wataalamu na mapitio ya ripoti za IPCC. Vilevile kongamano hilo lilihamasisha wanasayansi hasa vijana, watendaji, wakufunzi na wanafunzi kufuatilia na kushiriki katika mchakato mzima wa shughuli za IPCC hasa katika mzunguko wake wa saba ulioanza mwaka 2023 na unatarajiwa kumalizika kati ya mwaka 2029 na 2030.
Kongamano limeratibiwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela, likijumuisha wataalamu wa sayansi ya mabadiliko ya hali ya hewa na tasnia zinazohusiana kutoka Tanzania na Afrika Mashariki.
Mgeni rasmi katika ufunguzi wa kongamano hilo alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya TMA Mhe. Jaji Mshibe Ali Bakari ambaye kupitia hotuba yake alisisitiza ushiriki wa wataalamu wengi kutoka Afrika Mashariki katika mchakato wa IPCC.
“Ni matumaini yangu kuwa kupitia makongamano kama haya ya uhamasishaji wa wanasayansi kujihusisha katika kufanya tafiti zinazokidhi matakwa ya IPCC, wataalam wengi zaidi kutoka Afrika Mashariki wataweza kutoa mchango wao kikamilifu katika utayarishaji wa ripoti za tathmini ya Saba ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi ya IPCC (IPCC AR7). Alisema Jaji. Mshibe
Naye, Dkt. Ladislaus Chang’a, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu Mwenyekiti wa IPCC alielezea namna ambavyo ripoti za IPCC zimekuwa na mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi kimataifa na katika nchi moja moja.
“Ripoti ya IPCC ya AR7 inayoandaliwa inatarajiwa kuwa ya kina na itakuwa na jukumu muhimu katika mustakabali wa hatua za kuchukua dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa natabianchi kwa kuzingatia taarifa za kisayansi zilizohakikiwa vyema ambapo zina mchango mkubwa katika kuongeza ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi kikanda na Duniani kote”. Aliongeza Dkt. Changa.
Featured Post
DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.
Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...
-
DODOMA; Tarehe 19 Agosti, 2024; Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imekutana na wadau kutoka sekta mbalimbali nchini ili kujipanga na...
-
Dar es Salaam, 22 /0 8 /202 4 ; Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa msimu wa mvua za VULI 202 4 kwa maeneo yanayopat...
-
Dar es Salaam, Tarehe 30/01/2025 Katika kuboresha ufanisi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA),Taasisi ya Uongozi imetoa mafunzo ya sik...