Tuesday, August 13, 2019

TANZANIA YAPOKEA UENYEKITI WA KAMATI YA SEKTA NDOGO YA HALI YA HEWA NA KUCHAGULIWA KUWA MWENYEKITI WA UMOJA WA TAASISI ZA HALI YA HEWA ZA NCHI ZA SADC

Washiriki wa mikutano ya Kamati ya SADC Sekta ya Hali ya Hewa “(SADC Subsectoral Committee on Meteorology (SCOM) na Umoja wa Taasisi za Hali ya Hewa za nchi wanachama wa SADC  (SADC MASA) iliyofanyika kuanzia tarehe 5 hadi 9 Agosti 2019 Jijini, Windoek, Namibia.
Meneja wa Mahusiano ya Hali ya Hewa Kimataifa wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Ndugu Wilbert Timiza Muruke akitoa salamu za Tanzania kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi katika Mkutano wa Kamati ya SADC Sekta ya Hali ya Hewa “(SADC Subsectoral Committee on Meteorology (SCOM), Jijini, Windoek, Namibia


Wakati Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli akielekea kupokea Uenyekiti wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), Tanzania kupitia Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dkt. Agnes Kijazi amekabidhiwa Uenyekiti wa Kamati ndogo ya Sekta ya Hali ya Hewa ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) “SADC Sub-Sectoral Committee on Meteorology (SADC SCOM) kwa kipindi cha mwaka mmoja. 

Aidha, Tanzania kupitia Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Dkt. Agnes Kijazi amechaguliwa bila kupingwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Umoja wa Taasisi za Hali ya Hewa za nchi za SADC “SADC Meteorological Association of Southern Africa (SADC-MASA)” kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka huu wa 2019.  Bwana Wilbert Timiza Muruke  ambaye amemwakilisha Dkt. Kijazi amekabidhiwa nafasi hizo katika Mikutano ya SADC-SCOM na SADC-MASA iliyofanyika kwa kufuatana Jijini Windhoek, Namibia kuanzia tarehe 5 hadi 9 Agosti, 2019. 

Kama ilivyo kawaida baada ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kukabidhiwa Uenyekiti wa SADC, Sekta zingine zote zinakuwa chini ya uenyekiti wa Tanzania, hivyo kwa upande wa Sekta ya Hali ya Hewa, tayari TMA imekwishakabidhiwa Uenyekiti wa kamati hiyo ya SADC Sekta ya hali ya hewa (SADC SCOM) kutoka kwa Taasisi ya Hali ya Hewa ya Namibia. Aidha, Uenyekiti wa Tanzania kuongoza umoja wa Taasisi za Hali ya Hewa za SADC (SADC MASA) utadumu kwa miaka miwili, ambapo Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya hali ya hewa ya Lesotho amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa SADC MASA. Kabla ya kupokea nafasi hiyo ya kuwa Mwenyekiti wa MASA, Dkt. Kijazi alikuwa Makamu mwenyekiti na Bwana Franz Uirab kutoka Namibia alikuwa Mwenyekiti.

Akipokea dhamana hizo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Meneja wa Mahusiano ya Hali ya Hewa Kimataifa, Ndugu Wilbert Timiza Muruke ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu katika Mikutano hiyo, alishukuru kwa nafasi hizo na kumpongeza aliyekuwa Mwenyekiti wa SADC SCOM na SADC MASA ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Hali ya Hewa ya Namibia, Bwana Franz Uirab kwa mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha uongozi wake. Ndugu Muruke kwa niaba ya Mwenyekiti, Dkt. Kijazi aliahidi kutoa na kuomba ushirikiano wa taasisi za hali ya hewa za nchi wanachama wa SADC, ili kuendeleza mafanikio yaliyofikiwa na kutekeleza malengo yaliyowekwa ya kuboresha zaidi huduma za hali ya hewa, ziweze kuchangia ipasavyo katika uchumi wa viwanda kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii katika ukanda wa SADC. Hii ikiwa pia ni dhamira ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuelekea kupokea uenyekiti wa SADC ya kuleta mapinduzi ya viwanda na ubunifu hasa kwa kuwalenga vijana katika nchi Wanachama wa SADC. 

Mikutano hii imefanyika kulingana na ratiba ya mikutano na vikao vya kisekta ya SADC, na imejadili masuala mbalimbali ya uendelezaji wa sekta ya hali ya hewa katika eneo la SADC pamoja na kupitia hatua za utekelezaji wa maamuzi ya Mkutano wa Mawaziri uliopita. Aidha mapendekezo mapya yatakayowasilishwa katika mkutano ujao wa Mawaziri wenye dhamana na sekta za uchukuzi, TEHAMA na hali ya hewa utakaofanyika mwezi Septemba Jijini Dar es Salaam yametolewa. Mapendekezo haya ni pamoja na kuwahimiza nchi wanachama wa SADC kuendelea kuboresha miundombinu ya upimaji wa hali ya hewa ikiwa ni pamoja na kutekeleza mkataba wa Minamata ambao unahitaji nchi wanachama kuondokana na matumizi ya zebaki katika sekta mbalimbali, Nchi wanachama kuhakikisha wanaendelea kuboresha huduma na kupata cheti cha ubora cha kimataifa na kukitunza hususan katika utoaji wa huduma za hali ya hewa zitolewazo kwa usafiri wa anga (ISO 9001: 2015). Tanzania kupitia TMA tayari imeshapata cheti hicho mwaka 2017. Katika Mikutano hii miwili Tanzania imewakilishwa na Bwana Wilbert Timiza Muruke, Mtaalamu Mwandamizi wa hali ya hewa na  Meneja wa Mahusiano ya Hali ya Hewa Kimataifa (aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu) na Ndugu Mathew Ndaki, Mtaalamu wa hali ya hewa na afisa katika Ofisi ya Mahusiano ya Hali ya Hewa Kimataifa ya TMA.

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...