Wednesday, July 10, 2019

MHE. PROF. KABUDI: WIZARA ITAENDELEA KUTOA USHIRIKIANO KATIKA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA WMO

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akisalimiana na kupata maelezo mafupi kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt. Agnes Kijazi kuhusu majukumu ya nafasi yake ya umakamu wa tatu wa Rais wa WMO, Ofisi za wizara, Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka Wizarani na TMA, Ofisi za wizara, Dar es Salaam
Ujumbe kutoka TMA (juu) na Ujumbe kutoka Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki  (chini) wakisikiliza maelezo kutoka kwa Mhe. Prof Kabudi, Ofisi za wizara, Dar es Salaam

‘Nakuahidi kuwa Wizara itaendelea kutoa ushirikiano wote katika kutekeleza majukumu yako ndani ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO)’. Alisema Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakati alipokutana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Agnes Kijazi.

Katika mazungumzo hayo, Prof. Kabudi alisema Dkt. Kijazi amekuwa mfano kwa Tanzania na Afrika hususani kwa wanawake na kuahidi kutoa ushirikiano wenye lengo la kuhakikisha anafanikisha utekelezaji wa majukumu yake katika nafasi ya Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO na hivyo kuiwakilisha nchi vyema.

Mhe. Prof Kabudi aliendelea kuelezea umuhimu wa kujiendeleza kielimu kwa watumishi wote wa Serikali ili kuweza kujijengea uwezo wa kupambana na watumishi au wagombea wengine kutoka mataifa mbalimbali hususan mataifa yaliyoendelea kwenye nafasi za juu za kidunia.

Aidha, Mhe. Waziri alimtaka Mkurugenzi wa TMA kuendelea kuboresha huduma za hali ya hewa nchini kwa vile ni huduma muhimu sana kwa sekta zingine kama kilimo, uvuvi, mipango n.k, akitolea mfano wa kazi nzuri iliyofanyika ya kutoa tahadhari za mara kwa mara za mvua kubwa na kimbunga Kenneth ambazo zilisaidia Serikali kuchukua hatua stahiki

Naye, Dkt. Kijazi aliishukuru Wizara kwa namna walivyofanikisha mchakato mzima wa uchaguzi hadi kupatikana kwa nafasi ya umakamu wa Tatu wa Rais wa WMO na aliahidi kuendelea kupeperusha bendera ya Tanzania vizuri, kwavile ameona jinsi diplomasia ya Tanzania inavyokubalika kimataifa.

‘Kwa vile moja ya jukumu langu kubwa nililopatiwa kusimamia ni eneo la kujengeana uwezo (capacity building), nitahakikisha mawazo ya nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania yanawasilishwa na kufanyiwa kazi kwa maendeleo ya sayansi ya hali ya hewa na hivyo kuboresha huduma za hali ya hewa’. Alizungumza Dkt. Kijazi

Aidha, aliishukuru Serikali, kupitia Wizira wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kumuani na kukubali kujitosa katika kinyanga’nyiro hicho. Aliiomba Serikali iendelee kufanya hivyo kwa wengine ili kukuza diplomasia ya Tanzania duniani.

IMEANDALIWA NA;
OFISI YA UHUSIANO
MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA (TMA)

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...